Mhe. Wilbard Chuma Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe 18/07/202 amefungua rasmi mafunzo elekezi kwa watumishi wapya 58 wa Mahakama Tanzania. Mafunzo hayo yanaendeshwa na kufanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). Hili ni kundi la kwanza kati ya waajiriwa 227 waliofanyiwa usaili na kuajiriwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama hivi karibuni ambapo kuna kada mbalimbali kama Mahakimu, Maafisa Utumishi, Maafisa TEHAMA, Makatibu Mahususi, Watunza Kumbukumbu Wasaidizi na Madereva.
Akitoa
hotuba ya ufunguzi, Mhe. Chuma alianza kwa kuwapongeza waajiriwa hao wapya kwa
kuwaeleza kuwa ajira waliyopata hawakupata kama hisani ila imepatikana kutokana
na ubora waliouonesha wakati wa usaili hivyo wanapaswa kuwa waaminifu, waadilifu
na wachapakazi kwa kuzingatia mikataba ya ajira, viapo na sheria za nchi katika utumishi wao.
Mhe.
Chuma aliendelea kwa kuwasisitiza
Watumishi hao wapya wa Mahakama kwa kumnukuu Jaji Mkuu wa Mahakama wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe Mei 31, 2021 katika hotuba yake aliyoitoa
wakati akifungua rasmi Mafunzo elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani,
Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Mahakama Kuu Zanzibar hapa Chuoni kwa kusema
watumishi wa Mahakama wanatakiwa kuwa na uadilifu na maadili ili wafanye kazi
kwa kuzingaia Katiba na masharti ya viapo.
“Watu husahau kuwa mara nyingi sheria
sio mbaya bali ni nafsi, maadili na tabia za wanaotekeleza sheria hizo. Hivyo
nawakumbusha kila jalada utakalokuwa ukilitolea uamuzi ukumbuke kuwa linagusa
watu halisi, linagusa uhuru wao, biashara zao, mali zao na familia zao.
Kumbukeni kuwa wananchi kupitia katiba wametupa sisi Majaji mamlaka ya utoaji
haki lakini wananchi wamebaki na haki zao zote za msingi” alinukuu.
Mhe.
Chuma aliendelea kwa kuwakumbusha watumishi hao kuwa maadili ni kiini cha haki,
na hivyo wakati wa kutekeleza jukumu la utoaji haki na wanatakiwa kuzingatia
maadili ya kazi na kutoa maamuzi kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria, kanuni,
taratibu na miongozo iliyopo.
Mhe.
Chuma aliwaeleza watumishi hao wapya
kuwa malengo ya mhimili wa Mahakama yatafikiwa iwapo watakuwa na nia
moja na ushirikiano baina yao na watumishi wengine watakaowakuta kwenye vituo
vya kazi watakavyopangiwa. Alieleza kwamba ushirikiano huo utasaidia
kufanikisha jitihada zinazoendelea za maboresho ya Mahakama ya Tanzania. Mhe.
Chuma aliwasisitiza watumishi hao kuwa na ushirikiano na wadau wengine kwa
kuchukua mawazo mazuri na bora kutoka kwenye taasisi au idara zingine kwa
kuyafanyia kazi au kuyafikisha mahali panapostahili ili yalete mabadiliko kwa
kuwa kazi ya kulijenga taifa ni wote.
Mhe.
Chuma aliendelea kwa kuwasisitiza watumishi hao kuwa dhana ya uhuru wa mahakama
haina maana ya kuvunja sheria kwa kuwa kanuni hii ya kikatiba inaenda sanjari
na kanuni ile ya Utawala wa Sheria. Hivyo, amewataka Mahakimu kuwa ni wajibu wao kufanya kazi zao
chini ya kivuli cha uhuru wa Mahakama, kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa
sheria za nchi na sio kwa kuzivunja. Aliendelea kwa kuwaasa watumishi wengine ambao
sio mahakimu wakawasaidie maafisa wa Mahakama wa ngazi mbalimbali
katika kufikia azma ya kutenda na kutoa haki kwa mujibu wa sheria ili wasiwe
chanzo cha malalamiko au kusababisha uvunjifu wa amani kutokana na utendaji
kazi ambao unakiuka misingi ya utu na
katiba.
Mafunzo haya yanafanyika kwa makundi matatu ambapo
kundi la kwanza la Mahakimu Wakazi na Maafisa Kumbukumbu Wasaidizi yamenza leo tarehe 18 Julai ,2022. Makundi mengine ya kada nyingine yatafuata na
kutegemea kumalizika 12 Agosti, 2022.
IJA
inajukumu la kuwajengea uwezo watumishi wote wa mahakama kwa lengo la kuboresha
utendaji kazi wao pia kwa mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali
yanayotoa huduma za utoaji haki
nchini. Pamoja na mafunzo hayo
Chuo kimebobea katika kutoa mafunzo ya Stashahada na Astashahada ya sheria.
Vilevile Chuo kinafanya shughuli za kutoa ushauri wa kitalaamu, machapisho na
tafiti mbalimbali.
1.