Taasisi ya Irish Rule of Law International (IRLI) ya nchini Ireland imefanya ziara ya siku moja Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yenye lengo la kuendeleza hatua za utekelezaji wa mkataba wa mashirikiano uliofanywa kati yake na Chuo tarehe 10 Machi, 2022. Ziara hiyo iliyofanyika Julai 13, 2022 ilihusisha viongozi watatu kutoka katika Taasisi hiyo ambao ni Mkurugenzi Mtendaji wa IRLI Bwana Aonghus Kelly, Mratibu wa Programu IRLI, Bwana Sean McHale pamoja na Afisa Uhusiano Mwandamizi IRLI Tanzania na Zambia, Bwana Norville Connolly.
Wakati wa ziara hiyo wageni hawa pia walipata maelezo ya kina ya
shughuli zinazofanywa na Chuo kutoka kwa
Kaimu Mkuu wa Chuo Bwana Goodluck Chuwa.
Bwana Chuwa alianza kwa kuwaeleza historia fupi ya Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto toka kilipoanzishwa na malengo ya uanzishwaji wake. Aliendelea kwa kusema kwamba Chuo kimekuwa,
msaada mkubwa sana kwa Mahakama ya Tanzania na wadau mbalimbali wa sheria
nchini kwa mafunzo na tafiti mbalimbali zinazofanywa na Chuo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa IRLI nchini Tanzania Bwana Aonghus Kelly alitoa maelezo mafupi ya Taasisi hiyo kwa kusema kuwa, Taasisi hiyo inaendesha programu na miradi katika nchi zinazoendelea yenye lengo la kuimarisha ulinzi na upatikanaji wa haki za binadamu, demokrasia na utawala bora na kukuza utawala wa sheria. Aliendelea kwa kusema kuwa, IRLI inafanya kazi na washirika wa ndani kwa kupitia mashirikiano ili kufikia malengo yake. Alieleza kwamba washirika wa IRLI ni pamoja na mashirika ya kiserikali, wanataaluma ya sheria, watumishi wa mahakama, vyama vya wanasheria, wanafunzi wa sheria na asasi za kiraia katika nchi ambazo taasisi hiyo inafanya kazi.
Sambamba na hayo, IRLI na IJA walijadili kuhusu mpango wa kuandaa kitabu chenye mkusanyiko wa mashauri yanayohusu unyanyasaji na ukatili wa kingono kwa mtoto.
Pichani ni wageni wa Taasisi ya IRLI na viongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wakiwa katika Maktaba ya Chuo wakati wa ziara.






0 comments:
Post a Comment