Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma

Jaji kiongozi wa Tanzania

Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania (katikakati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa stashahada ya sheria

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Tuesday, December 21, 2021

IJA YATOA MAFUNZO KWA MADALALI NA WASAMBAZA NYARAKA ZA MAHAKAMA

 Na Innocent Kansha – Mahakama.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa amewakumbusha washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuwa mafunzo hayo yameanzishwa mahsusi kwa lengo la kuweka utaratibu rasmi wa kurasimisha namna ya kuwapata Madalali pamoja na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kitu ambacho hakikuwepo hapo awali.

Akifungua mafunzo ya siku 14 ya awamu ya nane toka kuanzishwa kwake mwaka 2018, leo tarehe 6 Disemba 2021 katika Ukumbi wa Shule ya Sheria kwa vitendo jijini Dar es salaam Bw. Chuwa  alisema, ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama wenye sifa, Muhimili kupitia Mpango Mkakati wake wa kwanza wa mwaka 2015/2016 – 2019/2020 na Mradi wa Uboreshaji wa Mahakama kupitia mradi wa huduma zinazomlenga mwananchi, iliandaa kanuni ziitwazo Kanuni za Uteuzi, Gharama, Malipo na Nidhamu za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama, Tangazo la Serikali Namba 363 la 2017 (The Court Brokers and Process Servers (Appointment, Remuneration and Disciplinary) Rules, GN. 363 of 2017).

Kwa kuzingatia jina la kanuni linavyosomeka kanuni hizo zinahusu uteuzi, gharama, malipo na nidhamu za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama ambapo mchakato huo ulikamilika mwaka 2017 baada ya kupata kanuni hizo ambazo zilitolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, aliongeza Bw. Chuwa.

“Kwa kuanzishwa mafunzo haya na kufuatiwa kwa kutungwa kwa kanuni hizo, hivi sasa Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama zimekuwa ni kada mbili tofauti na hivyo mtu ana uwezo wa kuchagua moja kati ya kada hizo na ndiyo maana baadhi ya washiriki wa mafunzo haya wanasomea kada zote wakati kuna baadhi wanasomea kada moja tu”, alifafanua Kaimu Mkuu huyo.

Kaimu Mkuu huyo aliongeza kuwa, lengo kuu la mafunzo hayo ni kuboresha utoaji huduma kwa jamii, kuongeza weledi na kuhakikisha kuwa Mahakama inakuwa na Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wenye maadili, mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi. Ili kuweza kufikia huko ni muhimu sana kuwa na utulivu wa kutosha na kuzingatia yale yote yaliyopangwa katika ratiba ya mafunzo hayo, ushiriki kamilifu ndiyo utakaowafikisha kwenye utoaji wa huduma bora.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa mujibu wa Kanuni ambapo kupitia kanuni hizo mtu yeyote mwenye nia ya kufanya kazi ya udalali na Usambazaji Nyaraka za Mahakama anapaswa kupata mafunzo hayo.

Akiongelea ubora wa mafunzo Bw. Chuwa alisema, kuanzishwa kwa mafunzo hayo ni mojawapo ya sehemu ya maboresho makubwa yanayoendelea katika muhimili wa Mahakama. Ili kuondoa malalamiko mengi yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi na moja ya eneo lenye kulalamikiwa sana ni ukosefu wa uadilifu wakati wa utekelezaji wa majukumu ambapo kwa kufanya hivyo kutawawezesha Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata kanuni zilizopo.

Akiwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo Bw. Chuwa alisema, Madalali wa Mahakama ni wadau muhimu sana katika utekelezaji wa jukumu la utoaji haki kwa wananchi. Endapo mtafanikiwa kuhitimu mafunzo yenu na kusajiliwa mtakuwa maafisa wa Mahakama ambao mtapewa jukumu la kutekeleza amri halali za Mahakama. Jukumu hilo msipolitekeleza vyema mtalalamikiwa kwa kutokuwatendea haki wananchi na kwa hiyo ni dhahiri kuwa Mahakama pia itakuwa imelalamikiwa.

Niwasihi kuwa baada ya kupata mafunzo haya mkazingatie kanuni na maadili mtakayofundishwa katika kutelekeleza majukumu yenu. Nafahamu kuwa mtajifunza mambo mengi sana katika kipindi hiki cha wiki mbili, yakiwemo masuala ya maadili katika fani ya udalali na usambazaji nyaraka za Mahakama, “kila fani ina maadili yake, wale watakaopata nafasi ya kufanya kazi ya udalali au usambazaji nyaraka za Mahakama ni muhimu kuzingatia maadili ya kazi hiyo”, alitilia mkazo Kaimu Mkuu huyo.

Bw. Chuwa akatoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo kuwa, wakati mnaendelea na mafunzo wekeni ndani yake pia mijadala huru itakayowasaidia kuboresha utendaji kazi wenu ili kupunguza malalamiko yanayotokana na wananchi kutokupata huduma bora. Msisite kuchangia uzoefu wenu kwa lengo la kuboresha na kuwaeleza wengine kipi kinachotakiwa kufanyika au kueleweka. Kwenu washiriki kosa hata liwe dogo sana katika utekelezaji wa majukumu yenu linaweza kuleta madhara makubwa sana kwa mtu binafsi, Familia, Mahakama na Taifa kwa ujumla.


Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa amewakumbusha washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama (hawapo pichani) kuwa mafunzo hayo yameanzishwa mahsusi kwa lengo la kuweka utaratibu rasmi wa kurasimisha namna ya kuwapata Madalali pamoja na Wasambaza Nyaraka za Mahakama.

Picha ya pamoja ya washiriki wa Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa na meza Kuu mara baada ya Mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Sheria kwa Vitendo Jijini Dar es salaam, (katikati) ni mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa, kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Masjala Kuu, Mhe. Victoria Nongwa na kushoto ni Mhadhiri na mratibu wa mafunzo ya Udalali na Usambazaji Nyaraka za Mahakama – Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bi. Hamisa Mwenegoha.

Picha ya pamoja ya washiriki wa Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa na meza Kuu mara baada ya Mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Sheria kwa Vitendo Jijini Dar es salaam, (katikati) ni mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa, kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Masjala Kuu, Mhe. Victoria Nongwa na kushoto ni Mhadhiri na mratibu wa mafunzo ya Udalali na Usambazaji Nyaraka za Mahakama – Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bi. Hamisa Mwenegoha.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa kwenye chumba cha mafunzo hayo wakimsikiliza mwezeshaji wa mafunzo hayo (hayupo pichani) yatakayo tolewa kwa muda wa wiki mbili Jijini Dar es salaam.

 

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa kwenye chumba cha mafunzo hayo wakimsikiliza mwezeshaji wa mafunzo hayo (hayupo pichani) yatakayo tolewa kwa muda wa wiki mbili Jijini Dar es salaam.


Friday, December 3, 2021

HESHIMUNI KILA MTU BILA KUJALI UMRI, HADHI AU NAFASI YAKE KATIKA JAMII: JAJI KIHWELO

Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo amewataka Naibu Wasajii na Watendaji kuwa waadilifu, wachapa kazi na kuheshimu kila mtu bila kujali umri, hadhi yake au nafasi yake katika Jamii. Aliyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo elekezi yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Dkt. Kihwelo aliwaeleza washiriki hao kuwa hawakupata nafasi hiyo kwa bahati bali walistahili kutokana na sifa zao za  utendaji kazi uliotukuka na kutokuwa na bila shaka watazitumikia nafasi hizo kwa bidii na uadilifu huku wakiheshimu mamlaka, madaraka na majukumu waliyonayo na yale ya wale watakaofanya nao kazi.

Aliendelea kuwasisitiza washiriki hao kuwa wao ni injini ya Mahakama hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu ili walio chini yao wafuate nyayo zao. 

“Ni tegemeo la kila mmoja wetu kuwa nyinyi ndio mtakuwa kioo cha tabia njema na sio kinyume chake” alisema Dkt. Kihwelo.

Hatahivyo, Dkt. Kihwelo aliwaasa viongozi hayo kuwa wasimamizi wazuri wa maadili na nidhamu katika maeneo yao ya kazi na kuongeza kuwa wao ni viongozi hivyo wanapaswa kuwa watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi  yenye kuzingatia hekima na busara kwa faida ya watumishi, wadau, Mahakama na Taifa.

Akitaja sifa kubwa iliyopo Mahakamani kuwa ni Upendo, Udugu na Mshikamano,  aliwatoa wasiwasi kwa kuwaeleza kwamba wasiwe na shaka kwani watapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa watangulizi wao pamoja na wale watakaowakuta vituoni.

 “Naamini ninyi pia mtatoa ushirikiano na niwaase pia kuwa msisite kuwafundisha mambo mapya ambayo hawayajui lakini pia muendelee kuwa wanafunzi wazuri kwani Wahaya wanamsemo usemao Experience is a Good Teacher” aliongeza.

Kwa upande wake Mhe. Happines Ndesamburo akitoa shukrani kwa niaba ya Naibu Wasajili kwa kuushukuru uongozi mzima wa mahakama kwa kuwawezesha kwa mara ya kwanza wasajili hao kupata mafunzo hayo elekezi.

Mhe. Ndesamburo alieleza kuwa mafunzo haya yatakuwa ni nyenzo muhimu katika utendaji wao wa kazi za kila siku ili kufikia dira na dhima ya mahakama ya utoaji haki kwa wote na kwa wakati. 

Aliongeza kuwa mafunzo waliyopata yamewaandaa vyema na kuahidi kwamba watakapokuwa kwenye vituo vyao vya kazi watatoa huduma za  kiwango cha juu na kuhakikisha kwamba wateja wao watatoka wakiwa wameridhika.  

Kwa upande wa Watendaji wa Mahakama Bw. Tutubi Mangazeni Mtendaji wa Mahakama Kuu Tanga akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watendaji wa mahakama walioshiriki mafunzo hayo alisema kuwa mafunzo haya yamekuwa ya umuhimu sana kwao kwani yamewajengea uwezo na kujifunza mambo mengi ambayo walikuwa hawayafahamu.

Bw. Mangazeni alitoa pendekezo kwa uongozi wa Chuo kwamba kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo ni vyema naibu wasajili na watendaji wa mahakama ambao hawajapata mafunzo hayo wapewe fursa ya kupata mafunzo kama hayo  ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi.

Mafunzo haya ya siku tano kwa naibu wasajili na watendaji wa mahakama yalifunguliwa na Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mnamo tarehe 29 Novemba, 2021 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja  na Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wa mwaka 2018/19-2022/23.

Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo akifunga rasmi mafunzo elekezi kwa naibu wasajili na watendaji wa mahakama yaliyofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 29 Novemba mpaka 03 Desemba, 2021

Mhe. Happiness Ndesamburo Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufaa na mshiriki  akitoa neno la shukurani kwa niaba ya washiriki wa upande wa Naibu Wasajili

Bw. Tutubi Mangazeni Mtendaji Mahakama kuu Tanga mshiriki  akitoa neno la shukurani kwa niaba ya washiriki wa upande wa Watendaji wa Mahakama

Picha ya juu na chini ni baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi ya Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama wakipokea vyeti vyao baadha kumalizika kwa mafunzo hayo ya siku tano.





Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akiwa katika picha cha pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi ya Naibu Wasajili na Watendani wa Mahakama. 

Thursday, December 2, 2021

KLABU YA HerForShe YASHIRIKI MAADHIMISHO YA UKIMWI


Desemba 1 kila mwaka ni siku ambayo dunia huadhimisha Siku ya UKIMWI. Nchini Tanzania kauli mbiu ya maadhimisho ya siku hiyo yalikuwa “Zingatia Usawa, Tokomeza Ukimwi, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko”.

Kitaifa maadhimisho haya yalifanyika mkoani Mbeya wakati kwa upande wa mkoa wa Tanga yalifanyika wilaya ya Muheza na katika ngazi ya wilaya ya Lushoto yalifanyika katika kata ya Mwangoi, jimbo la Mlalo.  Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lushoto Bi Ikupa Mwasyoge.

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kilishiriki katika maadhimisho hayo kupitia klabu ya HeForShe. HeForShe ni klabu ya wanachuo iliyoanzishwa na mwaka 2016 na Mkuu wa Chuo, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo Jaji wa Mahakama ya Rufani. Klabu hii ilianzishwa kwa lengo la kuhamasisha masuala ya kijinsia Chuoni. Klabu hii inatumia mtoto wa kiume katika kuinua nafasi ya mtoto wa kike.  Klabu inafanya shughuli mbalimbali za uhamasishaji na kutoa elimu katika shughuli nyingi zinazofanyika wilayani Lushoto hususani katika mashule na maadhimisho.

Akizungumza na wananchi katika maadhimisho hayo, Bi. Ikupa aliwakumbusha wananchi mambo mbalimbali ambayo bado yanapelekea ongezeko la maambukizi mapya ambayo ni pamoja na vitendo vya ukatili vinavyofanyika katika jamii, mila potofu za kurithi wake na vijana wengi kujihusisha na ngono isiyo salama.

Bi. Ikupa alisisitiza kuepuka kuwanyanyapaa watu wenye maambukizi.  Pia aliendelea kuwashawishi wananchi kujitokeza kupima na wale wote watakaopimwa na kukutwa na maambukizi kujitahidi kutumia dawa kwa uaminifu ili kuimarisha afya zao na kuwa na uwezo wa kuendelea na majukumu yao ya kila siku.

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kupitia klabu ya HeForShe inaungana na jamii ya wananchi wote wa Lushoto katika kukemea vikali mambo yote yanayopelekea maambukizi ya UKIMWI.



Baadhi ya wanaklabu ya HerForShe wakionyesha igizo la kuelimisha jamii kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI yaliyofanyika kiwilaya katika kata ya Mwangoi, Jimbo la Mlalo Wilayani Lushoto.

Wednesday, December 1, 2021

WATUMISHI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUTOA ELIMU YA MAHAKAMA KWA WANANCHI – JAJI CHANDE

Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman amewataka Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama Tanzania kutoa elimu kwa wananchi juu ya utendaji kazi wa mahakama na kuacha kuwa na hisia hasi kwani Mahakama ndicho chombo cha mwisho katika utoaji haki.

Akitoa mada kwa viongozi hao wakati wa mafunzo elekezi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Novemba 30, 2021, Mhe. Othman aliwapongeza kwa kuteuliwa na kuwakumbusha kuwa mwananchi wa kawaida anatamanani kuona shauri lake linamalizika mapema ili ajue hatma yake.

Mhe. Othman aliendelea kwa kuwaasa Naibu Wasajili na Watendaji hao  kuzingatia maadili na kuiishi miiko ya Mahakama na kutokuwa na makundi maofisini kwani wao wanaenda kutatua migogoro na sio kutengeneza.

Aidha, Mhe. Othmani aliwasisitiza viongozi hao kuwa na maono mazuri juu ya maendeleo ya Mahakama ili kurudisha imani kwa jamii juu ya utendaji wa shughuli za Mahakama ya Tanzania na kuleta mabadiliko ya kweli. Mhe. Othman alitumia wasaa huo kusisitiza uwajibikaji, kujenga utamaduni wa kufikika na kutoa maamuzi kwa wakati na kwa weledi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

 “ Kila mmoja wenu ni Kiongozi atumie maarifa yake kuisaidia Taasisi na kumsaidia Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi”.

Mhe. Othman aliendelea kwa kusema kuwa uboreshaji mkubwa na ufanisi umetokana na kuanzishwa Tume huru ya Utumishi wa Mahakama na pia kutenganisha kada mbili za taaluma ya watendaji na wasajili, kwa maana ya Watendaji kushughulika na masuala ya utawala na fedha na Wasajili kushughulikia masuala ya utaratibu wa mashauri mahakamani.

Jaji Mkuu huyo mstaafu aliwaelezea washiriki hao kuwa matokeo chanya ya uboreshaji wa huduma za mahakama yameonekana katika utendaji kazi ambapo hivi sasa kuna mahakama  inayotembea, mfumo wa kieletroniki wa utowaji wa haki  ikiwemo kusajili mashauri kwa njia ya mtandao.

Mafunzo haya  ni yale yaliyofunguliwa na Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mnamo tarehe 29 Novemba, 2021 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja  na Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama wa miaka mitano wa mwaka 2018/19-2022/23.



Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akiwasilisha mada ya Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania kwenye mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Picha ya baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Pichani  washiriki wa mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama kwenye picha  wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Monday, November 29, 2021

CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO CHAPONGEZWA KUWA NI KISIMA CHA UTOAJI MAFUNZO KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 29 Novemba, 2021 amefungua mafunzo elekezi ya siku tano kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ambapo amekisisifia Chuo cha Uongozi wa  Mahakama Lushoto (IJA) kwa mchango mkubwa kinachofanya na kujenga  taaluma  bora kwa watumishi wa Mahakama na wananchi wengine kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tano yanayowashirikisha viongozi hao, Mhe. Siyani amebainisha kuwa Chuo kwa kushirikiana na Kitengo cha mafunzo cha Mahakama ya Tanzania wamekuwa wakifanya kazi nzuri kwa kutoa mafunzo mbalimbali elekezi na endelevu kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania.

 “Kama ilivyo kwa wengine, mimi nina imani kuwa chuo hiki kweli ni kitovu na kisima cha elimu bora. Kimsingi, chuo hili kina uwezo wa kujenga  taaluma  na kufanya leo hii tuna Wasajili  ambao kesho ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Kwa hiyo, mimi niwapongeze sana na nifikishie salamu zangu kwa Mkuu wa Chuo,” Jaji Kiongozi alimweleza Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe, ambaye pia ni Naibu Mkuu wa IJA, Mipango, Fedha na Utawala.

Amesema kuwa mafanikio katika utoaji wa mafunzo elekezi ya awali na mafunzo endelevu ya kimahakama ni mojawapo ya matunda ya kazi nzuri yanayofanywa na IJA kwa kuzingatia Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya mwaka 2019 ambayo inakitambua Chuo hicho kama kitovu au kisima cha utoaji mafunzo kwa watumishi wa Mahakama, lakini vile vile utafiti wenye lengo la kuongeza tija na kuboresha utendaji wa Mahakama ya Tanzania.

Jaji Kiongozi aliwakumbusha washiriki kuwa mafunzo ambayo yameandaliwa kwa ajili yao yamelenga kuwapa mbinu na nyenzo sahihi za kuweza kukabili changamoto mbalimbali za kiutendaji. “Hivyo muwe wazi kuuliza maswali na kuchangia uzoefu kila mmoja kwa namna ambayo mnaona italeta matokeo chanya katika utendaji kazi wenu. Shabaha ya kila mmoja wetu iwe ni utoaji wa haki na kuliletea maendeleo taifa letu na kutekeleza kwa vitendo Mkataba wa Huduma kwa Mteja,” amesema.

Mhe. Siyani alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa wapo katika kipindi cha mapinduzi ya nne ya viwanda na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekuwa akisisitiza watumishi wa Mahakama kujinoa zaidi kwenye eneo la TEHAMA ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia hivi sasa.

Amebainisha kuwa miongoni mwa mada zitakazotolewa katika mafunzo hayo inahusu TEHAMA, hivyo ni imani yake kupitia mada hiyo washiriki wote watapata nafasi ya kujifunza juu ya nafazi zao katika usimamizi wa mashauri kwa njia za kielektroniki. Aliwaomba kutumia fursa hiyo kupata kitu cha nyongeza katika eneo hilo na kwamba kila mmoja wao awe mfuasi wa karibu wa TEHAMA kama dunia inavyowataka hivi sasa.

“Tambueni kwamba tunakoelekea hakutakuwa na nafasi kwa Msajili au Mtendaji asiye na uelewa wa TEHAMA katika Mahakama yetu. Hiyo ni dhahiri kwa sababu ninyi ni wasimamizi wa mifumo ikiwemo ya TEHEMA na bila shaka msimamizi bora ni yule anayefahamu anachokisimamia,” aliwaambia viongozi hao wa Mahakama ya Tanzania.

Awali akitoa neno la ukaribisho, Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe alisema kuwa mafunzo yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama siyo ya kwanza kutolewa hapo Chuoni, kwani IJA imekuwa ikitoa mafunzo elekezi (Induction) kwa wahesimiwa Majaji wote wapya wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mafunzo ya awali na elekezi kwa Majaji wote wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar wanapoteuliwa kwenye wadhifa huo na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani pamoja na Rais wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa Prof. Massawe, vilevile IJA imekuwa ikiendesha mafunzo elekezi kwa Mahakimu wote mara wanapoajiriwa kujiunga kwa mara ya kwanza na utumishi wa Mahakama kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutenda haki kwa wote na kwa wakati kwa kuzingatia misingi ya sheria na uadilifu.

“Hii ni mara ya kwanza mafunzo ya namna hii yametolewa kwa Naibu Wasajili na hata kwa Watendaji. Tunapenda kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kulisimamia hili. Tunaamini mafunzo haya elekezi ni mwanzo tu wa mafunzo endelevu ambayo washiriki hawa wataendelea kupata kama watumishi wa Mahakama. Chuo kinaahidi kitaendelea kutayarisha programu za mafunzo kulingana na uhitaji kadri watakavyoendelea kutekeleza majukumu yao na kubaini changamoto katika maeneo ya uhitaji wa mafunzo,” alisema.

Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali zitawasilishwa na waezeshaji waliobobea katika maeneo mbalimbali, akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Jaji Mkuu Mstaafu ,Mohamed Chande Othman, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January Msoffe, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati na watendaji wengine waandamizi wa Mahakama.

Miongoni mwa mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo zinajumuisha Uongozi wa Kimkakati, Stadi za Uongozi na Uwezo wa Kukabili Mabadiliko, Wajibu wa Mahakama, Utamaduni wake na Uhusiano wake na Mihimili Mingine ya Dola, Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama na Uboreshaji unaofanywa na Mahakama, Maadili ya Watumishi wa Umma na Maadili ya Kimahakama, Usimamizi wa fedha na Manunuzi ya Umma pamoja na Usimamizi wa Nyaraka.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akifungua mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajiri na Watendaji wa Mahakama yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.


Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe, ambaye pia ni Naibu Mkuu wa IJA, Mipango, Fedha na Utawala akitoa neno la ukaribisho kabla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tano yanayowashirikisha Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ambayo yanafanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). ,Mafunzo hayo yamefunguliwa leo tarehe 29 Novemba, 2021 na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani.



Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisistiza jambo alipokuwa anatoa mada katika mafunzo hayo.

 

Sehemu ya Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania (juu na picha za chini) wakifuatilia mada iliyokuwa inatolewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.








 


 


 

 

 


 


 

 

Wednesday, November 17, 2021

MAFUNZO KWA WAWEZESHAJI WA MAFUNZO YA MASHAURI YA MTOTO

Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama leo amefungua rasmi mafunzo kwa wawezeshaji 36 wa mafunzo ya haki za watoto kutoka sehemu mbalimbali Tanzania. Mafunzo haya yanafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 15 Novemba mpaka 19 Novemba katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma. Mafunzo hayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) chini ya ufadhili wa Shirika linalohudumia watoto duniani (UNICEF). 
Washiriki wa mafunzo haya ni Majaji kutoka Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Mahakimu wakazi wa ngazi mbalimbali, Waendesha Mashtaka na Maafisa Ustawi wa Jamii. Washiriki hawa watapitishwa katika mada mbalimbali zitakazowawezesha kuwa na uelewa na ujuzi wa pamoja juu ya uendeshaji bora wa mashauri ya mtoto. 

Katika mafunzo haya kutakuwa na mada mbalimbali zitawasilishwa na wawezeshaji mahiri na wabobezi katika masuala ya namna bora ya uendeshaji wamashauri hayo ambao ni Mhe. Sophia Wambura Jaji Mstaafu na Mhe. Matilda Philip Wakili Mstaafu wa kujitegemea. Akiongea katika ufunguzi wa mafunzo haya Mhe. Dkt. Kihwelo aliezea lengo kubwa la mafunzo haya kuwa ni kuwajengea uwezo wadau wanaoendesha mashauri ya mtoto. Kundi hilo linalofundishwa mafunzo hayo pia ni kwa ajili ya kuwaandaa ili waweze kufundisha wengine kwenye masuala ya haki za mtoto anapokuwa mhanga. Hii imekuja kwa ajili ya kuongeza kundi la wawezeshaji baada ya wengi waliofanya mafunzo ya namna hii kustaafu. 

Kwa upande wake mwakilishi kutoka UNICEF, Bi. Victoria Mgonela ameushukuru uongozi wa mahakama na Chuo kwa kulipa uzito wa kipekee suala la uendeshaji wa mashauri ya mtoto na kuahidi kuwa UNICEF itaendelea na mashirikiano hayo.

Mafunzo kama hayo yalishawahi kuendeshwa mwaka 2014 ambapo ilijumuisha majaji 6, Mahakimu wakazi 6, maafisa ustawi wa jamii 2 na watumishi 3 kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania akifungua mafunzo kwa wawezeshaji wa mafunzo ya haki za watoto mafunzo yatafanyika katika ukumbi yanayofanyika katika ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma
Bi. Victoria Mgonela Mwakilishi wa UNICEF akitoa salamu kutoka Shirika la UNICEF nchini Tanzania kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma
Picha ya pamoja ya Majaji wanaoshiriki katika mafunzo ambao ni Mhe. Rehema Sameji, Jaji wa Mahakama ya Rufani (katikati), Mhe. Paul Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani (wa pili kushoto) na Mhe. Issa Maige, Jaji wa Mahakama ya Rufani (wa pili kulia). Wengine ni Mhe. Devotha Kamuzora, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (wa kwanza kushoto na Mhe. John Chaba, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (wa kwanza kulia).
Majaji wanaoshiriki katika mafunzo (ambao wamekaa) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki.
Majaji wanaoshiriki katika mafunzo (ambao wamekaa) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki.
Majaji wanaoshiriki katika mafunzo (ambao wamekaa) wakiwa katika picha ya pamoja na sekretarieti kutoka IJA.
Baadhi ya Washiriki wa mafunzo kwa wawezeshaji wa mafunzo ya haki za watoto wakiwa wanasikiliza mada zinazoendelea katika mafunzo hayo kutoka kwa muwezeshaji Mhe. Sophia Wambura Jaji Mstaafu (hayupo pichani)

Saturday, November 13, 2021

MAHAFALI YA 21 YA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO


WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA ATAMBUA MCHANGO WA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO KATIKA KUTOA MAFUNZO KWA WADAU WA UTOAJI HAKI NCHINI. 

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi ametambua mchango wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto katika kutoa mafunzo ya utoaji haki nchini.

Waziri Kabudi ameongea hayo alipokuwa akihutubia kwenye mahafali ya Ishirini na Moja ya Chuo hicho yaliyofanyika tarehe 12 Novemba, 2021 Chuoni Lushoto.

Waziri Kabudi alisisitiza kuwa umuhimu wa Chuo kuwa kitovu cha kutoa mafunzo sio tu kwa Mhimili wa Mahakama, bali pia kwa Taasisi za Umma zinazohitaji elimu endelevu inayolenga kuboresha utoaji haki na usawa katika jamii.

Waziri Kabudi amewaomba wahitimu katika mahafali hayo kutumia hatua waliyofikia kuwa chachu ya kujiendeleza zaidi kwenye elimu kwani ulimwengu wa sasa unahitaji zaidi watu wenye ujuzi na maarifa ya kutosha.

Waziri Kabudi aliendelea kwa kusema kuwa tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho, mhimili wa Mahakama ndiyo mnufaika mkubwa wa zao la kitaaluma la Chuo hicho kwani mhimili huu umeweza kuendeleza watumishi wake pamoja na kuajiri mahakimu na watumishi wengine kutoka katika Chuo hiki. Aliongeza kwa kusema pamoja na hayo yote Chuo pia kimekuwa kikiratibu na kufanya mafunzo endelevu ya kujengea uwezo watumishi mbalimbali wa mahakama.

Waziri Kabudi aliongeoza maandamano na kutunuku stashahada na astashahada kwa wahitimu wa Chuo hicho pamoja na kutaja mambo sita ambayo yameipaisha Tanzania duniani  na kuibuka kuwa nchi ya mfano wa kuigwa inapoelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wake.

Mambo yaliyotajwa na Waziri Kabudi ni pamoja na misingi iliyoachwa na baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuondoa ukabila nchini na kuifanya Tanzania kuwa taifa badala ya mkusanyiko wa makabila, taifa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya muda uliotazamiwa yaani mwaka 2025, uwezo wa taifa kudumisha na kuenzi tunu ambazo ni amani,umoja,mshikamano,utu,haki,heshima ya mwanadamu, uhuru na demokrasia. Mambo mengine aliyotaja Waziri ni uthubutu wanchi yetu kuendesha miradi mikubwa kwa kutumia rasilimali na fedha zake za  ndani, uwezo wa taifa kuzifanya rasilimali zilizokuwa za Watanzania ikiwemo kuvunja mikataba mibovu ambayo haikuwa na tija kwa taifa na jambo la mwisho lililotajwa na Mhe. Prof. Kabudi ni ukomavu wa kisiasa na ukatiba katika taifa letu.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mheshimiwa Dkt. Gerald A. M. Ndika amesema Chuo kimekabidhiwa majukumu ambayo ni kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa huduma za kitaalamu majukumu ambayo Chuo kinamudu kuyatekeleza kwa ufanisi.

“Sera ya mafunzo ya mahakama ya mwaka 2019 imebainisha kuwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  ni kitovu na wakala wa mafunzo na utafiti wa Mahakama Tanzania na kutokana na hilo tumeendelea kuboresha utendaji kazi wa Chuo ikiwemo kurugenzi ya mafunzo endelevu ya kimahakama” amesema Dkt. Ndika.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ametaja changamoto zinazokikabili Chuo ikiwepo ufinyu wa bajeti,kutopewa kibali cha kuajiri, uchakavu wa miundombinu na uchache wa mabweni ya wanachuo.

Mkuu huyo wa Chuo aliendelea kwa kusema kuwa uchakavu wa miundombinu unatokana na majengo ya chuo kuwa makongwe ambapo yanalazimika kukarabatiwa ili kutumika kwa usalama.

Hata hivyo Mhe. Dkt. Kihwelo alieleza kwamba pamoja na changamoto zilizopo Chuo kimeendelea kufanya majukumu yake ya kitaaluma kama Chuo kilivyokusudiwa kuyafanya. Na pia aliupongeza uongozi mzima wa Mahakama ya Tanzania kwa kukiamini Chuo.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi akihutubia kwenye mahafali ya 21 ya wahitimu wa Stashahada na astashahada ya sheria wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akiongoza Maandamano kabla ya kuanza kwa sherehe za Mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto leo wilayani Lushoto, Tanga. Waziri Kabudi alikuwa Mgeni rasmi kwenye Mahafali hayo. Kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald


Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa astashahada ya Sheria waliofanya vizuri kitaaluma katika masomo yao wakati wa mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Wahitimu wakitunukiwa Stashahada ya Sheria katika Mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto leo wilayani Lushoto, Tanga. Waziri Kabudi alikuwa Mgeni rasmi kwenye Mahafali hayo.

Wahitimu wakitunukiwa Astashahada ya Sheria katika Mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto leo wilayani Lushoto, Tanga. Waziri Kabudi alikuwa Mgeni rasmi kwenye Mahafali hayo.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akizungumza wakati wa sherehe hizo.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa chama cha wanafunzi waliowahi kusoma katika chuo hicho. 


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wahitimu wa Astashahada ya Sheria. 

Mmoja wa Wahitimu wa Stashahada ya Sheria ambaye ni mshindi wa masomo kadhaa akipokea zawadi ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliyotoa kwa washindi wote katika masomo.

Wednesday, November 10, 2021

ZIARA YA MAKAMISHINA WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameahidi kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ili kiweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu, ikiwemo kutoa wahitimu bora watakaolisaidia taifa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.

Prof. Ole Gabriel, ambaye ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alitoa ahadi hiyo katika ziara ya Tume iliyofanya katika Chuo hicho hivi karibuni kutembelea maeneo mbalimbali, likiwemo Jengo la Hostel ya Wavulana ambalo linajengwa kwa kugharamiwa na Mahakama ya Tanzania katika mpango wa uboreshaji wa majengo chuoni hapo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani aliupongeza uongozi wa Chuo kwa jitihada zake inazozifanya katika kutoa mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo watumishi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.

Katika ziara hiyo, ambayo ni mwendelezo wa shughuli mbalimbali zinazofanyika kuelekea siku ya mahafali ya ishirini na moja ambayo inafanyika tarehe 12 Novemba, 2021, Prof. Ole Gabriel ameambatana na Makamishna mbalimbali wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Wajumbe wa Tume hiyo pia walipata nafasi ya kukutana na menejimenti ya Chuo ambapo walifanya majadiliano yaliyolenga kuboresha huduma zinazotolewa na chuo hicho. Katika kikao hicho, Katibu wa Tume hiyo ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama alitoa salamu kwa niaba ya wajumbe wa Tume hiyo.

Prof. Elisante aliiambia Menejimenti kwamba Chuo kina wajibu mkubwa kwa Mahakama ya Tanzania na Taifa kwa ujumla katika kutoa elimu ambayo italeta matokeo chanya kwa taifa sio tu kwa kufaulu katika mitihani mbalimbali bali kutoa wanafunzi waliobora ambao wanaweza kufanya kazi popote na katika mazingira yoyote.


Mhe. Dkt Paul Kihwelo akiwa na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama akipitishwa katika maeneo mbalimbali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wakati wa ziara ya siku moja 
Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakipata maelezo kuhusu jengo la bweni la wavulana ambalo linajengwa kwa kupitia fedha za mahakama ya Tanzania  kutoka kwa Afisa Miliki wa Chuo Bwana George Masanja 


Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Mahakama wakiwa katika picha ya pamoja na wanachuo wa Stashahada ya Sheria mwaka wa pili walipotembelea hivi karibuni katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto

Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, Baraza la Uongozi wa Chuo wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Chuo walipokuwa kwenye ziara ya siku moja chuoni hapo hivi karibuni
Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Mahakama na  Baraza la Uongozi wa Chuo wakiwa katika picha ya pamoja na  Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama walipokuwa kwenye ziara ya siku moja chuoni hapo hivi karibuni
Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Mahakama na  Baraza la Uongozi wa Chuo wakiwa katika picha ya pamoja na  Sekretarieti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto walipokuwa kwenye ziara ya siku moja chuoni hapo hivi karibuni