Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma

Jaji kiongozi wa Tanzania

Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania (katikakati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa stashahada ya sheria

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Wednesday, August 31, 2022

JAJI MKUU WA TANZANIA ASISITIZA MAADILI KWA MAJAJI

 Na Rosena Suka IJA

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 30 Agosti, 2022 alifungua mafunzo elekezi yanayowaleta pamoja Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wapya 21 na wengine wanne wa Mahakama Kuu Zanzibar ambapo amewahimiza kuzingatia maadili wanapotekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi.

Mhe. Prof. Juma aliwataka Majaji hao kusoma na kujadili miongoni mwao Kanuni za Maadili za Maafisa Mahakama iliyochapishwa tarehe 20 Novemba, 2020 kupitia Tangazo la Serikali Namba 1001 la mwaka 2020 ambazo zitawasaidia kubaki ndani ya matarajio ya kimaadili.

“Uwezo na Maadili ni nguzomuhimu ya kuaminiwa na kuaminika kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Uwezo, Ujuzi na Maarifa yenu yatajenga Imani na kuaminiwa kwenu kwa namna ambavyo mtafanya maamuzi yenu kwa haki, kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo, Mila na Desturi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Jaji Mkuu akawakumbusha kuwa pamoja na maadili ya Viongozi wa Umma; Majaji wa Mahakama Kuu, Majaji wa Rufani, Wasajili, Mahakimu, na Wasaidizi wote wa Majaji, wanaongozwa na Kanuni za Maadili za Maafisa wa Mahakama (Code of Conduct and Ethics for Judicial Officers, 2020).

Amesema uongozi wa Mahakama ukishirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), umeweka utaratibu wa Mafunzo elekezi ya awali kwa wote walioapishwa kuwa Majaji wakiwemo wale wanaojiunga na utumishi wa Mahakama kwa mara ya kwanza.

“Mafunzo elekezi yanalenga kuwatayarisha kutumikia nafasi ya Jaji. Mafunzo elekezi yanawakaribisha rasmi katika Utumishi wa Mahakama wenye maudhui, tamaduni, mitizamo na uzoefu uliojengeka muda mrefu ambazo itawawekea misingi imara ya kuwasaidia katika utoaji wa huduma za kimahakama,” amesema.

Jaji Mkuu amebainisha pia kuwa mafunzo hayo elekezi yanalenga kuwajengea msingi wa kuifahamu Mahakama, kufahamu mwelekeo wa Mhimili wa Mahakama ndani ya maudhui ya mwelekeo wa nchi ya Tanzania ndani dunia inayoizunguka.

Akaseama kuwa kwa upande wake Mhimili wa Mahakama utafaidika na uwezo, uzoefu, ujuzi na umahiri wa Majaji hao waliojijengea kutoka maeneo waliyopitia, hivyo mchanganyiko huo utakuwa wa faida kubwa kwao binafsi, kwa Mahakama na pia kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Jambo moja muhimu ambalo litajitokeza katika Mafunzo haya elekezi ni dhamira dhahiri ya Mahakama ya Tanzania kuwaingiza kuwa sehemu ya waboreshaji wa huduma za utoaji haki kupitia Mipango Mkakati na Programu za Maboresho,” Mhe. Prof. Juma alisema.

Amesema kuwa Maboresho ya Mahakama yanayoendelea hivi sasa yamewajengea watumishi wa Mahakama utamaduni mpya, mitazamo mipya na mwelekeo mpya wa utoaji wa huduma za haki kwa kumlenga na kumridhisha mwananchi (Citizen-Centric Judicial Modernization and Justice Service Delivery).

“Ninawasihi muwe sehemu ya dhana hii ya utoaji wa huduma za haki kwa kumlenga na kumridhisha mwananchi. Mafunzo haya elekezi yanawatayarisha Majaji wapya kuifahamu Dira ya Mahakama ya Tanzania—Timely and Accessible Justice for All,” Jaji Mkuu alisema.

Aidha, Mhe. Prof. Juma akabainisha kuwa katika kumlenga na kumridhisha mwananchi, Jaji sio idadi bali umuhimu wake kwa mwananchi ni huduma bora za haki, ujuzi, ufanisi, na uwazi wa huduma za utoaji haki kwani wananchi wanafuata huduma mahakamani, wala hawaji kumtembelea Jaji, wanafuata huduma za utoaji haki.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma  akifungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu Zanzibar uliofanyika tarehe 30 Agosti, 2022 katika Ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto,(IJA)  Mhe. Dkt. Gerald Ndika na kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Mustapher Siyani






Picha ya chini na ya juu ni Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani)


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar mara baada ya kufungua mafunzo elekezi. Wengine walioketi mbele ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Mustapher Siyani (wa tatu kulia),Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Gerald Ndika (wa tatu kushoto), Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Faustine Kihwelo (wa pili kushoto), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu (wa pili kulia), Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa kwanza kushoto) na Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Wakili Genoveva Katto.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji Wanawake wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar mara baada ya kufungua mafunzo elekezi kwa Majaji.

Tuesday, August 9, 2022

IJA YATOA MAFUNZO KWA MAKATIBU MUHTASI WA MAHAKAMA YA TANZANIA

Na Rosena Suka, Lushoto

Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo,  Jaji wa Mahakama ya Rufaa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  leo tarehe 9 Agosti, 2022 amefungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Mahsusi wapatao 56 wa Mahakama ya Tanzania  yanayohusu  Namna Bora ya Uendeshaji wa Ofisi. Mafunzo hayo yanayofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 09 Agosti ,2022 mpaka 13 Agosti, 2022 katika ukumbi wa Mafunzo uliopo Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Akifungua mafunzo hayo Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amewataka Makatibu Muhtasi  kutoa huduma bora zinazoendana na uwekezaji katika majengo ya Mahakama nchini.  Aliendelea kwa kusema  kuwa, Mahakama ya Tanzania iko katika maboresho ambayo yanagusa maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu ya majengo na raslimali watu hivyo mafunzo haya yana lengo la kuwaandaa watumishi hao ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea.

“Hivyo lengo la mafunzo yanayotolewa ni kujaribu kuwajengea uwezo na kubadilisha fikra za watumishi wa Mahakama ili huduma wanazozitoa mahakamani ziendane na ubora wa majengo ambayo yanaendelea kuboreshwa,” amesema.

Mhe. Dkt. Kihwelo aliwasihi watumishi hao kuwa waadilifu na wachapakazi ili kuipa sifa  nzuri  Mahakama ya Tanzania kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kuichafua Mahakama kama matumizi ya lugha mbaya. Pia aliwaomba watumishi hao watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi ni wajibu  kushirikiana na kuonyesha waliochojifunza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick amewaambia washiriki hao kuwa Mahakama imejipanga kuwajengea uwezo watumishi wake katika kada mbalimbali ili kuendana na maboresho yanayoendelea.

Bi. Beatrice Patrick amesema kundi hilo la washiriki wa mafunzo linajumuisha Makatibu Muhtasi 56, ambapo 50 wametoka katika Mahakama mbalimbali za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi,  washiriki  sita wakiwa ni waajiriwa wapya.

Amesema kuwa watumishi hao wanapewa mafunzo hayo kwa lengo la kuwakumbusha majukumu yao ya kazi za Ukatibu Muhtasi, utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi wa ofisi na mawasiliano ya kiofisi,  uzalendo na protokali, mipango ya Mahakama na uboreshaji, huduma kwa mteja, masuala ya saikolojia na ushauri, mwelekeo wa Mahakama kwa sasa katika mapinduzi ya viwanda kuelekea Mahakama Mtandao na matumizi ya TEHAMA.

 


Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akisisitiza jambo alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Muhtasi 56 yaliyoanza kufanyika leo tarehe 9 Agosti, 2022.


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick akizungumza kwa ufupi kumkaribisha Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo kufungua mafunzo hayo.


Sehemu ya Makatibu Muhtasi wanaoshiriki katika mafunzo (picha mbili juu na moja chini) ikifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Mkuu wa Chuo.


Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote wa mafunzo.

Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Mahakiumu wa Mahakama za Lushoto waliohudhuria kwenye ufunguzi wa Mafunzo hayo.



 Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya mafunzo 

Monday, August 1, 2022

KUWENI NA FIKRA CHANYA MNAPOTOA HUDUMA; PROF OLE GABRIEL

 Na Mary Gwera, Mahakama-Lushoto

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Waajiriwa wapya wa Mahakama nchini kubadili fikra hasi kwa kuwa na fikra chanya ili kuondokana na utoaji wa huduma kwa mazoea na badala yake watoe huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

Akizungumza na Watumishi hao leo tarehe mosi Agosti, 2022 mjini Lushoto wakati akifungua mafunzo elekezi ya awali kwa waajiriwa hao, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, Mahakama inatekeleza programu za maboresho yanayomlenga mwananchi. Kwa hivyo, kipaumbele ni kuhakikisha Mahakama inatoa huduma bora zitakazofanya wananchi kuwa na imani na chombo hicho cha haki pamoja na kuwaweka wananchi kuwa karibu na Mahakama.

“Kwa dhamira hii, Mahakama inatutaka sote kwa pamoja kubadilika fikra zetu ili kuondokana na kutoa huduma kwa mazoea na badala yake kupitia mafunzo haya mnaelekezwa kuwa kila mmoja wenu katika nafasi yake ahakikishe anadhamiria kuunga mkono juhudi hizi za Mahakama kwa kwenda kutoa huduma bora kwa namna ambayo itawafanya wananchi na jamii kwa ukumla kuwa na imani nanyi na imani kwa Mahakama,” amesema Mtendaji Mkuu.

Prof. Ole Gabriel, amewaeleza pia Watumishi hao kuwa tayari kufanya kazi kwenye maeneo watakayopangiwa bila manung’uniko kwa kuwa ndiko wananchi wanataka kupatiwa huduma.

“Ni matarajio yangu kuwa mtakubaliana na vituo mtakavyopangiwa kwa kuwa huko ndiko kunakohitaji huduma zenu na ndio maana Serikali ilitoa kibali muajiriwe. Niwadokeze tu hapa kuwa, hakuna sehemu nzuri wala mbaya ndani ya Mahakama na badala yake kila Mahakama ipo kwenye maeneo ambayo wananchi wanaishi,” amesisitiza Prof. Ole Gabriel.

Amebainisha kuwa, Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo katika maeneo ambayo ni ya msingi katika kuwaandaa kuwa watumishi wema wenye haiba, tabia, mienendo na maadili ya kimahakama.

Akizungumzia suala la matumizi ya TEHAMA mahakamani, Mtendaji Mkuu amewaeleza Watumishi wao kulipa kipaumbele suala la matumizi ya teknolojia kwakuwa ndio Mahakama inapojielekeza kwa sasa.

“Mtakapokuwa mnajifunza hapa, mtaelezwa kuhusu mifumo mbalimbali ya KITEHAMA ambayo itatumika katika kuboresha utoaji haki na huduma mbalimbali katika Mahakama. Lengo la kuelekezwa hayo ni kuwataka mfahamu kuwa matumizi ya TEHAMA si hiari bali ni jambo la lazima kwa kuwa mtakutana na mifumo ya kiteknolojia na matumizi yake katika kutoa huduma za kimahakama na kugundua kuwa imeshika kasi katika kila kona ya Mahakama,” amesisitiza Mtendaji Mkuu.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu amesema kwamba, lengo kuu la mafunzo hayo ni kubadilisha mitazamo ya Watumishi wapya ili iendane na mitazamo ya Mahakama hatimaye kuwawezesha kufanya kazi inavyotakiwa.

“Kama tunavyofahamu Watumishi hawa wametoka mazingira tofauti tofauti, wamelelewa katika mazingira mbalimbali pamoja na mitazamo tofauti, kwahiyo lengo kubwa la mafunzo haya ni kuwaandaa ili waweze kuendana na kile ambacho Mahakama inatarajia,” amesema Bi. Patricia.

Mafunzo hayo ya siku tano (5) yamehusisha Watumishi wa Kada za Afisa Utumishi/Tawala, Wahasibu, Wakaguzi wa Ndani, Maafisa TEHAMA, Maafisa Ugavi pamoja na Madereva.

Mafunzo hayo ambayo imeelezwa kuwa yatakuwa endelevu kwa Waajiriwa wapya wa Mahakama, ni mwendelezo wa Mafunzo yaliyotolewa kwa kundi la Mahakimu na Wasaidizi wa Kumbukumbu yaliyomalizika tarehe 29 Julai, 2022. Aidha, yanafanyika kwa mara ya kwanza, kwa kuwa kabla ya hapo hakukuwa na mafunzo ya namna hii kwa watumishi hao.

Mada zinazotarajiwa kutolewa katika Mafunzo hayo ni pamoja na Muundo na tamaduni za kimahakama, Mpango Mkakati wa Mahakam ana Mpango wa Uboreshaji Huduma za Mahakama, Huduma kwa wateja, Maadili ya Utumishi wa Umma na wa Mahakama, Ubunifu katika kazi na nyingine.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo alipokuwa akifungua rasmi Mafunzo elekezi kwa Waajiriwa wapya wa Mahakama ya Tanzania yanayofanyika leo tarehe Mosi Agosti, 2022 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.



           Washiriki wa wakifuatilia zoezi la Ufunguzi wa Mafunzo wa elekezi.


4.     Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Elia Baha akitoa neno la utangulizi katika zoezi la ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Mahakama. Aliyeketi wa pili kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo, Bw. Halid Magenda, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Morogoro, wa kwanza kulia ni Mhe. Rose Ngoka,  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto na wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo Mahakama ya Tanzania, Bi Patricia Ngunguru


5.     Hakimu Mfawidhi wa Wilaya Lushoto, Mhe. Rose Ngoka akitoa neno la ukaribisho         katika zoezi la ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Mahakama.



5.     Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Elia Baha akitoa neno la utangulizi katika zoezi  la ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Mahakama.