Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 29 Novemba, 2021 amefungua mafunzo elekezi ya siku tano kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ambapo amekisisifia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa mchango mkubwa kinachofanya na kujenga taaluma bora kwa watumishi wa Mahakama na wananchi wengine kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tano yanayowashirikisha viongozi hao, Mhe.
Siyani amebainisha kuwa Chuo kwa kushirikiana na Kitengo cha mafunzo cha
Mahakama ya Tanzania wamekuwa wakifanya kazi nzuri kwa kutoa mafunzo mbalimbali
elekezi na endelevu kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania.
“Kama ilivyo kwa
wengine, mimi nina imani kuwa chuo hiki kweli ni kitovu na kisima cha elimu
bora. Kimsingi, chuo hili kina uwezo wa
kujenga taaluma na kufanya leo hii tuna
Wasajili ambao kesho ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Kwa
hiyo, mimi niwapongeze sana na nifikishie salamu zangu kwa Mkuu wa Chuo,” Jaji
Kiongozi alimweleza Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe, ambaye pia ni
Naibu Mkuu wa IJA, Mipango, Fedha na Utawala.
Amesema kuwa mafanikio
katika utoaji wa mafunzo elekezi ya awali na mafunzo endelevu ya kimahakama ni
mojawapo ya matunda ya kazi nzuri yanayofanywa na IJA kwa kuzingatia Sera ya
Mafunzo ya Mahakama ya mwaka 2019 ambayo inakitambua Chuo hicho kama kitovu au
kisima cha utoaji mafunzo kwa watumishi wa Mahakama, lakini vile vile utafiti
wenye lengo la kuongeza tija na kuboresha utendaji wa Mahakama ya Tanzania.
Jaji Kiongozi aliwakumbusha
washiriki kuwa mafunzo ambayo yameandaliwa kwa ajili yao yamelenga kuwapa mbinu
na nyenzo sahihi za kuweza kukabili changamoto mbalimbali za kiutendaji. “Hivyo
muwe wazi kuuliza maswali na kuchangia uzoefu kila mmoja kwa namna ambayo
mnaona italeta matokeo chanya katika utendaji kazi wenu. Shabaha ya kila mmoja
wetu iwe ni utoaji wa haki na kuliletea maendeleo taifa letu na kutekeleza kwa
vitendo Mkataba wa Huduma kwa Mteja,” amesema.
Mhe. Siyani alitumia nafasi
hiyo kuwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa wapo katika kipindi cha
mapinduzi ya nne ya viwanda na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma amekuwa akisisitiza watumishi wa Mahakama kujinoa zaidi kwenye eneo la
TEHAMA ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia hivi sasa.
Amebainisha kuwa miongoni
mwa mada zitakazotolewa katika mafunzo hayo inahusu TEHAMA, hivyo ni imani yake
kupitia mada hiyo washiriki wote watapata nafasi ya kujifunza juu ya nafazi zao
katika usimamizi wa mashauri kwa njia za kielektroniki. Aliwaomba kutumia fursa
hiyo kupata kitu cha nyongeza katika eneo hilo na kwamba kila mmoja wao awe
mfuasi wa karibu wa TEHAMA kama dunia inavyowataka hivi sasa.
“Tambueni kwamba
tunakoelekea hakutakuwa na nafasi kwa Msajili au Mtendaji asiye na uelewa wa TEHAMA katika Mahakama yetu. Hiyo ni
dhahiri kwa sababu ninyi ni wasimamizi wa mifumo ikiwemo ya TEHEMA na bila
shaka msimamizi bora ni yule anayefahamu anachokisimamia,” aliwaambia viongozi
hao wa Mahakama ya Tanzania.
Awali akitoa neno la
ukaribisho, Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe alisema kuwa mafunzo
yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama siyo ya kwanza
kutolewa hapo Chuoni, kwani IJA imekuwa ikitoa mafunzo elekezi (Induction) kwa
wahesimiwa Majaji wote wapya wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mafunzo ya
awali na elekezi kwa Majaji wote wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar
wanapoteuliwa kwenye wadhifa huo na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani
pamoja na Rais wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Prof.
Massawe, vilevile IJA imekuwa ikiendesha mafunzo elekezi kwa Mahakimu wote mara
wanapoajiriwa kujiunga kwa mara ya kwanza na utumishi wa Mahakama kwa lengo la
kuwajengea uwezo wa kutenda haki kwa wote na kwa wakati kwa kuzingatia misingi
ya sheria na uadilifu.
“Hii ni mara ya kwanza
mafunzo ya namna hii yametolewa kwa Naibu Wasajili na hata kwa Watendaji.
Tunapenda kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kulisimamia hili. Tunaamini
mafunzo haya elekezi ni mwanzo tu wa mafunzo endelevu ambayo washiriki hawa
wataendelea kupata kama watumishi wa Mahakama. Chuo kinaahidi kitaendelea
kutayarisha programu za mafunzo kulingana na uhitaji kadri watakavyoendelea
kutekeleza majukumu yao na kubaini changamoto katika maeneo ya uhitaji wa
mafunzo,” alisema.
Katika mafunzo hayo, mada
mbalimbali zitawasilishwa na waezeshaji waliobobea katika maeneo mbalimbali,
akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Jaji Mkuu Mstaafu
,Mohamed Chande Othman, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January
Msoffe, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati na watendaji
wengine waandamizi wa Mahakama.
Miongoni mwa mada
zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo zinajumuisha Uongozi wa Kimkakati, Stadi
za Uongozi na Uwezo wa Kukabili Mabadiliko, Wajibu wa Mahakama, Utamaduni wake
na Uhusiano wake na Mihimili Mingine ya Dola, Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama
na Uboreshaji unaofanywa na Mahakama, Maadili ya Watumishi wa Umma na Maadili
ya Kimahakama, Usimamizi wa fedha na Manunuzi ya Umma pamoja na Usimamizi wa
Nyaraka.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akifungua mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajiri na Watendaji wa Mahakama yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe,
ambaye pia ni Naibu Mkuu wa IJA, Mipango, Fedha na Utawala akitoa neno la
ukaribisho kabla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tano yanayowashirikisha
Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ambayo yanafanyika katika Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). ,Mafunzo hayo yamefunguliwa leo tarehe 29
Novemba, 2021 na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Siyani.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisistiza jambo alipokuwa anatoa mada katika mafunzo hayo.
Sehemu
ya Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania (juu na picha za chini)
wakifuatilia mada iliyokuwa inatolewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.
Elisante Ole Gabriel.