Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma

Jaji kiongozi wa Tanzania

Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania (katikakati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa stashahada ya sheria

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Thursday, December 14, 2023

SERIKALI YA WANACHUO YAPATA MAFUNZO ELEKEZI

 Na Rosena Suka, IJA

Kaimu Mkuu wa Chuo na Naibu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Taaluma, Tafiti na Ushauri, Bw. Goodluck Chuwa leo tarehe 14 Desemba, 2023 amefungua mafunzo elekezi ya siku moja kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo wa IJA (IJASO) kwa mwaka wa masomo 2023/2024 yaliyofanyika Chuoni Lushoto.

Kwenye ufunguzi huo  Bwana Chuwa amewaeleza viongozi hao  kwamba lengo kuu la mafunzo hayo elekezi ni kuwajengea uwezo kwenye utekelezaji wa  majukumu yao ya uongozi kwa kufuata miongozo ya sheria, taratibu na kanuni za chuo na taifa kwa ujumla. 

Bwana Chuwa aliendelea kwa kusema viongozi hao wamebeba dhamana kubwa ya kuwahudumia wanachuo wenzao  kwa sababu wao ni kiungo  katika kuwafikisha maelekezo yote yanayotolewa na Menejimenti kwenda kwa wanachuo na kutoa mrejesho kutoka kwa wanaowangoza kuja kwenye menejimenti bila kuongeza au kupunguza uhalisia.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Fatihiya Massawe aliwasisitiza viongozi hao wa wanachuo kutendea haki nyadhifa walizonazo kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili waliowachugua kwani serikali ya wanachuo ni chombo muhimu katika musitakabali wa Chuo.

Prof. Masawe aliwakumbusha viongozi hao kusimamia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuonyesha mfano bora kwa wanachuo wenzao.

Katika semina hiyo elekezi viongozi hawa wamepitishwa katika mada mbalimbali zilizotolewa na watoa mada kutoka katika taasisi za umma Wilayani Lushoto ambao ni Mwakilishi kutoka Taasisi ya Kupambana na Rushwa (PCCB), Mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi na Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).  Mada nyingine zilitolewa na vitengo na Idara vya ndani ya Chuo ambavyo ni Mkaguzi wa ndani, Mhasibu Mkuu,Mdhibiti ubora, Msajili na Mshauri wa Wanachuo.

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kina utaratibu wa kutoa mafunzo elekezi kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kila mwaka mara tu serikali hiyo inapowekwa madarakani.


Kaimu Mkuu wa Chuo na Naibu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Taaluma, Tafiti na Ushauri, Bw. Goodluck Chuwa akifungua Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO


Naibu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Fatihiya Massawe akiwaelekeza Viongozi wa Serikali ya Wanachuo katika  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO


Inspecta wa Polisi kutoka Wilaya Lushoto Karim Bruno akiwasilisha mada kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO

Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Vya Taifa Wilayani Lushoto (NIDA) Bwana Francis Daniel akiwasilisha mada kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO


Mwakilishi kutoka Taasisi ya Kupambana na Rushwa  Wilayani Lushoto (PCCB) Bwana Norbert Massaba akiwasilisha mada kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO


Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO wakifuatilia mada

Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO wakifuatilia mada

Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO wakifuatilia mada

Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO wakifuatilia mada


Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO wakifuatilia mada











Friday, November 24, 2023

IJA NI TANURI LINALOPIKA WAHITIMU BORA

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekipongeza Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kutoa wahitimu waliopikwa katika tanuri la vielelezo vya ubora  na ufanisi wa huduma kwakuwa na uwezo wa kukabiliana na kumudu mabadiliko yoyote katika soko la ajira. Rai hiyo aliitoa leo tarehe 24 Novemba, 2023 wakati wa mahafali ya 23 kwa wahitimu 831 wa ngazi mbalimbali wa  Chuo Cha Uongozi wa Mahakama yaliyofanyika Chuoni Lushoto.

Alisema kuwa kufanyika kwa mahafali ya Chuo ni uthibitisho wa mafanikio makubwa kwa Wanafunzi waliohitimu kupitia juhudi kubwa za Uongozi wa Chuo na wanataaluma. Aliendelea kwa kusema mahafali ni wakati mzuri wa kujitathmini na kutambua kuwa Chuo chetu kimepiga  hatua kubwa katika kutoa elimu bora, Mafunzo Endelevu ya kimahakama, kufanya tafiti na  ushauri elekezi kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa sheria wa  ndani na nje ya nchi. Mahakama ya Tanzania imekuwa ikivunia kuwa na Chuo chenye kutekeleza malengo yaliyokusudiwa.

Aidha,  Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha wahitimu kuwa ni muhimu kufahamu vyema mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yanayogusa Tanzania na Dunia kwenye matumizi ya Tecknolojia ya Habari na Mawasiliano yanayosukumwa na Akili Bandia ambayo yamefanya mabadiliko katika utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia za kisasa.

“Tahadhari muhimu hapa, kila mmoja wenu anatakiwa kubadilika na kujiongezea ujuzi na umahiri katika matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma. Uwezo uliotokana na Astashahada ya Sheria (Certificate), na Stashahada ya Sheria (Diploma in Law) peke yake hautakuwezesha kupata ajira za kiushindani katika Tanzania na Dunia ya Dijitali” alisema Mhe. Prof. Juma.

Pamoja na hayo Mhe. Prof. Juma amefarijika kwa kuona Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto umefikia hatua nzuri ya kukamilisha ujenzi wa jukwaa la ufundishaji wa elimu kwa njia ya ki-elekitroniki (E-LEARNING PLATFORM).  Akaendelea kwa kutaja faida kadhaa zitakazotokana na ufundishaji wa njia hiyo ya ki-elekitroniki ni pamoja na kuwafanya wanafunzi kuhudhuria masomo yao huko huko waliko  huku wakiendelea na kazi zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dkt. Gerald Ndika alisema Chuo kimepata mafanikio makubwa kwenye  kutoa Mafunzo, warsha na makongamano mbalimbali. Pamoja na mafunzo na makongamano yanayofanywa Chuo pia kinafanya tafiti mbalimbali kukidhi mahitaji ya  kuwajengea uwezo wataalamu wetu. Tafiti hizo zimepelekea Chuo kuandaa machapisho mbalimbali kama vile kitabu cha mkusanyiko wa maamuzi ya Mahakama kuhusu unyanyasaji na ukatili wa kingono kwa watoto.  Hii inadhihirisha waziwazi Chuo kinavyoshirikiana na jamii dhidi ya kupinga unyanyasi na kulinda na kutetea haki ya mtoto.

Mhe. Dkt Ndika aliendelea kwa kumhakikishia  Jaji Mkuu wa Tanzania kuwa Chuo kiko kwenye maandalizi ya kufatilia huduma zinaofanywa na wahitimu wake katika maeneo mbalimbali kwa kufanya tathimini mahususi.  Hii imetokana na wahitimu wa Chuo kuhitajika katika maeneo mbalimbali.

Naye Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo katika maelezo yake alimshukuru Mhe Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 20 Septemba 2023 kuridhia mapendekezo ya Kamati ya Raisi ya Utekelezaji (PIC) na kuidhinisha Muundo wa Mgawanyo wa Majukumu ya Chuo ili kuimarisha utendaji kazi.  Katika muundo huo umeanzisha Kurugenzi ya Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu ambayo jukumu lake kubwa litakuwa ni  kuratibu mafunzo ya Kimahakama kwa maafisa wa Mahakama na watumishi wengine wa Mahakama na wadau mbalimbali wa sekta ya sheria nchini.

Jumla ya wanachuo 851 wamehitimu masomo yao ambapo Astashahada ya Msingi ya Sheria (Basic Technician Certificate in Law) jumla ya wahitimu ni 336 ambapo wakike ni 177 na wakiume ni 159, Astashahada ya Sheria (Technician Certificate in Law) jumla ya wahitimu ni 242 ambapo wakike ni 101 na wa kiume ni 141 na kwa upande wa Stashada ya Sheria (Diploma in Law) jumla ya wahitimu ni 273 ambapo wakike ni 137 na wa kiume ni 136. 












Monday, August 14, 2023

Msajili mkuu wa Mahakama ya Tanzania afungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya 37

 

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amefungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo leo tarehe 14/08/2023.

Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yanafanyika hapa Chuoni IJA na yatadumu kwa siku tano hadi tarehe 18/08/2023.

Katika hotuba yake ya Ufunguzi Mhe. Chuma ambae ndiye alikuwa mgeni Rasmi  amewataka Mahakimu hao kwenda kusaidia kuondoa mrundikano wa mashauri katika Mahakama za mwanzo kama ambavyo Sera ya Mahakama ya Tanzania inavyotaka.

“Mpaka sasa bado Mahakama za Mwanzo zinaendelea kuongoza katika umalizaji wa Mashauri na kutokuwa na mrundikano wa mashauri, kwa hiyo tunategemea ongezeko lenu litaendelea kupunguza mzigo wa kazi wa kila hakimu na hatimaye kuendeleza sera ya Mahakama ya Tanzania kutaka kusiwe na mashauri yanayozidi miezi sita,” amesema Mhe. Chuma.

Pia Mhe. Chuma amewataka mahakimu wakazi hao wapya kujifunza matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano(TEHAMA) ili waweze kutekeleza vema majukumu yao hasa wakati huu Mahakama ya Tanzania ikiwa imejielekeza katika eneo hilo la Teknolojia.

“Karne hii ya 21 imetawaliwa na matumizi ya Teknolojia katika kuwahudumia wananchi, jifunzeni matumizi ya mifumo ya TEHAMA inayoendeshwa na Mahakama ili msipate ugumu mnapotekeleza majukumu yenu,” amesisitiza Mhe. Chuma.

Vile vile, Mhe. Chuma amewasisitiza washirika hao kuwa wanapotekeleza majukumu yao, basi hawana budi kuzingatia misingi ya haki za binadamu, maisha ya watu na ustawi wa Usalama wa nchi.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda amezungumzia muhimu wa mafunzo hayo kwa kubainisha kwamba yanalenga kuwapatia Mahakimu hao miongozo itakayowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Kimsingi umuhimu wa mafunzo haya ni kwa ajili ya kuwapatia muongozo Mahakimu wapya ambao wanaenda kuanza majukumu yao katika Mahakama za mwanzo, ukiwemo utoaji wa haki ambao ndio jukumu kubwa la Mahakimu hawa,” amesema Mhe. Dkt. Kisinda.

Ameongeza kuwa Mahakimu watapewa miongozo, maelekezo na miiko mbalimbali ambayo inahusiana na majukumu ya kule wanapokwenda kusimamia utoaji wa haki.

Nao baadhi ya Washiriki wa Mafunzo hayo akiwemo  Mhe. Aden William Ruvurahende ambae ni Hakimu Mkazi mpya amebainisha faida ya mafunzo hayo kwao wao washiriki.

“Kwa kweli suala hili la mafunzo kwetu sisi ni la muhimu sana kwa sababu ni mwanzo wa kujua majukumu yetu, na fursa ya kufahamu miongozo na kanuni  ya kimahakama  ili itusaidie kwa ajili ya utendaji haki pale tunapokwenda kuwahudumia wananchi,” amesema Mhe. Ruvurahende.

 Kuhusiana na mlundikano wa mashauri amebaininisha: “Kuhusiana na mrundikano wa mashauri Mahakamani, ni changamoto kwetu sisi ila tunakwenda kusaidia kutatua suala hilo.”

Nae Mshiriki Mhe. Salma Athuman Mwamende anabainisha kuwa Mahakama itarajie weledi, ufanisi, na uwajibikaji kutoka kwao.

 



Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akihutubia wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.


Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akizungumza wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.



Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma(katikati) wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.

Wa pili kushoto ni  Mhe. Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda, wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Bi. Patricia Ngungulu, wa kwanza kulia ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Kavumo Mndeme.




Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma(katikati) akiwa katika picha na baadhi ya baadhi ya Washiriki wa Mafunzo Elekezi ambao ni Wahe. Mahakimu Wakazi wapya wa mahakama za Mwanzo katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).

Wa pili kushoto ni  Mhe. Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda, wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu, wa kwanza kulia ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Kavumo Mndeme.




Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo Elekezi ambao ni Wahe. Mahakimu Wakazi wapya wa mahakama za Mwanzo wakiwa katika mafunzo hayo katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).





Jaji mstaafu ambae pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheira, Mhe. January Msoffe akiwasilisha mada kwa Washiriki wa Mafunzo Elekezi ambao ni Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akihutubia wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.


Sunday, August 6, 2023

Naibu Waziri: IJA ni Chuo muhimu kwenye mambo ya haki






Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema kuwa Chuo cha Uongozi wa MahakamaLushoto(IJA) ni Chuo muhimu katika kuwajenga watu wanaosimamia masuala ya haki hapa nchini.
Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul amesema hayo leo Jumamosi tarehe 05/08/2023 wakati akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya IJA,  Halmashauri Tendaji ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti(RAAWU) tawi la Lushoto pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, hapa Chuoni wilayani Lushoto.
Amesema kuwa Chuo cha IJA kinapotoa maarifa kwa watu wa kada mbalimbali, basi kinasaidia katika masuala ya haki, akibainisha kuwa wananchi mbalimbali bado wanakabiliwa na ukosefu wa haki.
"IJA ni Chuo muhimu, nimefurahi kuona kumbe tuna Taasisi nzuri hapa," amesema Naibu Waziri na kuongeza,
"Sisi ambao tuna husika na wananchi moja kwa moja kama wabunge, madiwani na wenyeviti ni mashahidi kwamba wananchi wetu bado wana ukosefu wa haki zao hasa masuala ya kisheria, kwa hiyo nina imani ninyi mkiwapa maarifa watu wanaokuja kusoma hapa mnakuwa mnasaidia kwenye eneo la haki."
Pia Naibu Waziri huyo wa Katiba na Sheria ameongeza kuwa amejifunza masuala mengi ya Chuo cha IJA na 
kuhusu changamoto za Chuo Cha IJA, amebainisha kuwa atakwenda kuzifanyia kazi pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria na viongozi wengine.
"Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria alikuja hapa akapokea changamoto zenu, nami niwaambie tutakwenda kuzifanyia kazi na kazi yetu sisi ni kuwa kiungo ili kuona mnafanya kazi vizuri," amebainisha Mhe. Naibu Waziri.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha IJA ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F.Kihwelo amesema kuwa Chuo ni kitovu cha elimu na Utafiti kwa upande wa Mahakama na kwamba kimeendelea kuzalisha watu muhimu kwenye eneo la usimamizi wa haki.
Awali katika ziara hiyo, Mhe. Naibu Waziri huyo wa Katiba na Sheria alitembelea maeneo kadhaa ya Chuo, ikiwemo Maktaba, Hosteli ya Wanaume ya Benjamini Mkapa pamoja na viwanja vya michezo vya Chuo.
Katika hatua nyingine, Uongozi wa Chuo umempatia Mhe. Naibu Waziri zawadi za vitu mbalimbali yakiwemo machapisho ya Chuo.







 Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Pauline Gekul akisaini Kitabu cha wageni Ofisini kwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) alipofanya ziara Chuoni IJA.



Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul(katikati) akizungumza jambo wakati akiwa katika Maktaba  ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA)..

Kulia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo na kulia ni Mkutubi wa Chuo cha IJA, Bw, Jackson Chacha.



Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (kushoto) akiwa na   Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo(kulia) mara baada ya kukagua Hosteli ya wanaume ya Benjamin Mkapa alipofanya ziara hapa Chuoni IJA.



Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo(kulia) akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Pauline Gekul(hayupo pichani) aliyetembelea Chuo cha IJA hivi karibuni.


Wajumbe wa Halmashauri Tendaji ya Chama cha wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, habari na utafiti(RAAWU) Tawi la Lushoto wakimsikiliza Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul  alipofanya ziara Chuoni IJA.



Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo(kushoto) akimkabidhi machapisho ya Chuo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul alipofanya ziara hapa Chuoni IJA.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akizungumza na Wajumbe wa Menejimeti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) na Halmashauri Tendaji ya Chama cha wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, habari na utafiti(RAAWU) Tawi la Lushoto na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, alipofanya ziara hivi karibuni hapa Chuoni IJA.




Monday, June 12, 2023

Jaji Mkuu afungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani

 Na: Yusufu Ahmadi IJA Lushoto


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 12/6/2023 amefungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji sita(6) wapya wa Mahakama ya Rufani na mwingine mmoja ambae hakupatiwa mafunzo hapo awali.

Mafunzo hayo yatachukua siku tano hadi tarehe 16/6/2023 na yameandaliwa na Mahakama na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na yanafanyika hapa IJA Lushoto.

Katika hotuba yake, Jaji Mkuu Prof. Juma amewatoa wito Majaji hao wa Mahakama ya Rufani kufanya kazi katika majopo ili maamuzi yao yasitofautiane..

“Maamuzi yetu yawe na uhakika wa mambo, tunafanya kazi katika majopo, jopo moja lisitoe maamuzi ambayo ni tofauti kabisa na majopo mengine, na hii imetuletea changamoto kubwa sana, Jaji mmoja wa Rufani akiamua tofauti na ule utaratibu wa kisheria, sisi wengine tunajua amekosea, kwa kinatufanya sisi wengine tukwepe uamuzi, sasa ile inakuwa sio vizuri,” amebainisha Jaji Mkuu Prof. Juma.

Pia Mhe. Jaji Mkuu Prof. Juma amewaasa Majaji hao kutafakari kwa kina maamuzi wanayoyatoa kwa kuwa Katiba ya Tanzania imewapa nafasi ya mwisho ya utoaji wa tafsiri ya haki hapa nchini.

“Jambo langu kwenu ni kwamba, ni vizuri siku zote kutafakari uzito wa maamuzi katika nafasi yenu kama Jaji wa Mahakama ya Rufani, kila siku unaposimamia shauri lolote, chukua muda mfupi kidogo, tafakari, kwa sababu Katiba imekupa nafasi ya mwisho katika tafsiri ya haki, ukikosea yale makosa yanakuwa ni makubwa sana na yanachukua muda mrefu kurekebishika,” amesema Jaji Mkuu.

Kwa upande mwingine, Jaji mkuu amewatolea wito Majaji hao kusoma masuala mbalimbali yanayoendelea duniani yakiwemo ya teknolojia badala ya kusoma tu mambo yanayohusu majalada ya Mahakamani, ili wawe na ufahamu mpana utakaowasaidia katika kushughulikia majalada.

Katika mafunzo hayo, Jaji Mkuu ameendesha mada juu ya utamaduni wa Mahakama ikiwa na lengo la kuwafanya Majaji hao wapya watambue taratibu na sheria mbalimbali zinazotumika katika uendeshaji wa mashauri katika Mahakama ya Rufani.

Majaji hao sita wapya waliyoteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hapo Mei 18 mwaka huu ni Mhe.Sam Mpaya Rumanyika, Mhe. Zainab Goronya Muruke, Mhe. Leila Edith Mgonya, Mhe. Amour Said Khamis, Mhe.Dkt Benhajj Shaaban Masoud, Mhe. Gerson John Mdemu na Mhe.Agnes Zephania Mgeyekwa.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama ya Rufani na mwezeshaji wa mafunzo hayo, Mhe. Augustine Mwarija amewaambia Majaji hao kuwa nafasi hiyo waliyopewa waitumie vema kuleta maboresho katika Mahakama ya Rufani.

“Natambua kuwa mlistahili kupata uteuzi huu, sina shaka mtaitumikia kwa uthabiti nafasi hiyo ambayo mmeaminiwa na kupewa, na kama mlikuwa mkiona changamoto yoyote katika mahakama ya Rufani, kwa lengo la kuendeleza maboresho, tambueni sasa ninyi ni sehemu ya kukabiliana na changamoto hizo,” amesema Jaji Mwarija.

Nae Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) Dkt. Paul F. Kihwelo ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, amesema kuwa hayo ni mafunzo Elekezi ya tatu kutolewa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, ya kwanza yakifanyika mwaka 2019 kwa Majaji nane, ya pili mwaka 2021 kwa Majaji sita na ya tatu ni ya mwaka huu 2023 kwa Majaji saba.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa pia na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Tanga, Latifa Mansoor, Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Wilbert Chuma na Viongozi wa ngazi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  akifungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji  wapya wa Mahakama ya Rufani leo tarehe 12/6/2023 yaliyoandaliwa na  Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto 



Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) Dkt. Paul F. Kihwelo ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani akitoa neno ya utangulizi wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yanayoendeshwa na Chuo cha Uongzo wa Mahakama Lushoto



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani alipokuwa anafungua Mafunzo Elekezi  leo tarehe 12/6/2023 yaliyoandaliwa na  Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto 

 pichani ni Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani wakisikiliza mada iliyokuwa inatolewa na Mwezeshaji katika  Mafunzo Elekezi  yaliyoandaliwa na  Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto 






Wednesday, May 17, 2023

WANANCHI WAIMWAGIA SIFA IJA KWA ELIMU BORA YA SHERIA

 Na: Yusuph  Sungura  IJA  Lushoto

Wananchi mbalimbali wamekipongeza Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) kwa utoaji wa elimu bora ya sheria hapa nchini. Wananchi hao wametoa pongezi hizo walipotembelea banda la IJA katika maonesho ya pili ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi(NACTVET) ya mwaka 2023, yanayoendelea katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Erick Samwel ambae ni mkazi wa Arusha amesema kuwa IJA inatoa elimu bora ya sheria nchini na kwamba kinastahili pongezi kwa kazi hiyo.

"Kuna ndugu yangu alisoma hapo IJA miaka ya nyuma, anasema kuwa chuo hicho kinafundisha sana na kumfanya mwanafunzi awe vizuri sana kwenye sheria," amesema Samwel.

Nae mzazi Martha Shirima aliyefika kwenye banda la chuo cha IJA na binti yake, amesema kuwa wamefika ili kuulizia utaratibu wa kujiunga na chuo hicho kwa kuwa anasikia walimu wanafundisha sana kiasi ambacho mwanafunzi anakuwa mahiri sana.

"Nimekuwa nikisikia kutoka kwa baadhi ya watu wakikisifu sana hiki chuo kwa elimu ya sheria nchini, ndio maana nimekuja hapa na binti yangu ili tupate maelezo zaidi. Hongereni kwa hilo," amesema Martha.

Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi wa IJA Tundonde Mwihomeke amebainisha kuwa IJA ni bora katika utoaji wa elimu ya sheria nchini kwa kuwa walimu wake wamekuwa wakihakikisha mwanafunzi anaelewa zaidi.

"Walimu wa IJa tunahakikisha wanafunzi anaelewa, watu wanasema hatuna blah blah, ni kweli, lengo letu ni kuhakikisha mwanafunzi anapata elimu bora iendane na dunia inavyokwenda," amesimulia mhadhiri huyo msaidizi Tundonde.

Pia ameongeza kuwa kila mwanachuo hupangiwa mhadhiri anaewajibika kumuongoza na kumshauri katika masuala ya taalumu yake.

Nae Afisa Udahili wa chuo cha IJA, Magdalena Mlumbe amesema kuwa chuo kina miundombinu muhimu na ya kisasa ikiwemo maktaba ambayo ina vitabu muhimu katika maarifa ya sheria.

"Chuo chetu kina miundombinu ya kisasa ambayo ni muhimu katika ufundishaji, mathalani kuna maktaba ya kisasa yenye vitabu vya ambavyo si rahisi kuvipata kwenye maktaba zingine," amesema Magdalena.

Vile vile, Magdalena ameongeza kuwa chuo kina miundombinu yote muhimu ikiwemo huduma ya malazi, zanahati na viwanja vya michezo.


Pichani Bi Tundonde Mwihomeke Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akitoa maelezo ya shughuli za Chuo kwa wananchi waliojitokeza katika banda la Chuo wakati wa Maonesho ya Pili ya ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi(NACTVET) ya mwaka 2023.

Pichani Bi Magdalena Mlumbe Afisa Udahili wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akitoa maelezo ya shughuli za Chuo kwa wananchi waliojitokeza katika banda la Chuo wakati wa Maonesho ya Pili ya ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi(NACTVET) ya mwaka 2023.


Pichani Bi Tundonde Mwihomeke Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akitoa maelezo ya shughuli za Chuo kwa wanafunzi waliojitokeza katika banda la Chuo wakati wa Maonesho ya Pili ya ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi(NACTVET) ya mwaka 2023.



Pichani wanafunzi waliotembelea banda la Chuo wakipata maelezo kuhusu shughuli za Chuo wakati wa Maonesho ya Pili ya ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi(NACTVET) ya mwaka 2023.