Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse
Chigamoy Owiny-Dollo leo tarehe 25 Mei, 2022 amefanya ziara ya kutembelea Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na kujionea shughuli mbalimbali zinafanywa na Chuo.
Katika ziara yake, Mhe. Owiny-Dollo
ameambatana na Maafisa 12 kutoka nchini Uganda ambao miongoni mwa aliombatana nao ni Jaji Kiongozi wa Uganda Mhe. Dkt. Flavian Zeija, Msajili ya Mahakama ya
Uganda, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa JTI Uganda, Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya JTI Uganda, Msajili waTaasisi ya JTI Uganda na viongozi wa International
Development Law Organization Uganda(IDLO).
Akiongea akiwa kwenye ziara hiyo,
Mhe. Owiny-Dollo alisema kuwa lengo la ziara yao ni kwa ajili ya
kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kuwandaa Maafisa Mahakama ambao wamepangiwa
majukumu mapya na kujifunza jinsi ya kuijengea uwezo Taasisi ya Mafunzo ya
Kimahakama ya nchini Uganda (JTI) pia kujenga ushirikiano katika masuala
mbalimbali yanayohusu vyuo na jinsi ya kuiwezesha Mahakama ya Uganda
kufanikisha katika maboresho yake kiutendaji.
Mhe. Owiny-Dollo aliendelea
kwa kusema kuwa mafunzo ya kuwandaa Maafisa wa Mahakama wanaopewa majukumu
mapya ni muhimu katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo huduma bora ya utaoji haki
kwa wananchi.
Alisema wanataka kupata uzoefu
ambao utawasaidia yeye na ujumbe kutoka Chuo cha Mahakama cha Uganda
kuwawezesha watumishi wanaopewa majukumu mapya kupata mafunzo ambayo yatasaidia
katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Maafisa wa Mahakama walioandaliwa
kwa kupewa mafunzo mazuri wataelewa vema majukumu yao na mambo ambayo anatakiwa
kufanya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kupata haki wanapokuwa
na mashauri” alisema
Alipokuwa akiwakaribisha wageni hao, Mwenyekiti wa Baraza
la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika alionyesha
furaha yake kwa kuushuru ugeni huo kwa kusema kwamba ujio wao ni fursa muhimu
ambapo wataitumia kwa kujifunza mambo mbalimbali na kubadilishana uzoefu jinsi vyuo
vya Mahakama vinavyofanya kazi.
Naye Mkuu wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Dkt. Paul
Kihwelo alipokuwa anaelezea historia ya Chuo kilianzishwa kwa Sheria ya Bunge,
Sheria Namba 3 ya 1998. Kilianza kazi yake tarehe 23 Oktoba, 2000 na kilikuwa
kinatoa Cheti na Diploma ya Kozi za Sheria. Uzinduzi rasmi ulifanywa na Rais
Benjamin Mkapa tarehe 3 Agosti 2001. Pamoja
na historia hiyo Mkuu wa Chuo alieleza lengo la madhumuni ya kuanzishwa kwa
Chuo ilikuwa ni kujengea uwezo watumishi wa Mahakama.
Ziara hiyo ni sehemu ya
ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Uganda na ujirani mwema
kati ya nchi hizi mbili. Sambamba na kutembelea maeneo mbalimbali ya Chuo,
Wageni hawa wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vilivyopo
katika Wilaya ya Lushoto.