Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma

Jaji kiongozi wa Tanzania

Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania (katikakati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa stashahada ya sheria

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Tuesday, December 21, 2021

IJA YATOA MAFUNZO KWA MADALALI NA WASAMBAZA NYARAKA ZA MAHAKAMA

 Na Innocent Kansha – Mahakama.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa amewakumbusha washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuwa mafunzo hayo yameanzishwa mahsusi kwa lengo la kuweka utaratibu rasmi wa kurasimisha namna ya kuwapata Madalali pamoja na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kitu ambacho hakikuwepo hapo awali.

Akifungua mafunzo ya siku 14 ya awamu ya nane toka kuanzishwa kwake mwaka 2018, leo tarehe 6 Disemba 2021 katika Ukumbi wa Shule ya Sheria kwa vitendo jijini Dar es salaam Bw. Chuwa  alisema, ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama wenye sifa, Muhimili kupitia Mpango Mkakati wake wa kwanza wa mwaka 2015/2016 – 2019/2020 na Mradi wa Uboreshaji wa Mahakama kupitia mradi wa huduma zinazomlenga mwananchi, iliandaa kanuni ziitwazo Kanuni za Uteuzi, Gharama, Malipo na Nidhamu za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama, Tangazo la Serikali Namba 363 la 2017 (The Court Brokers and Process Servers (Appointment, Remuneration and Disciplinary) Rules, GN. 363 of 2017).

Kwa kuzingatia jina la kanuni linavyosomeka kanuni hizo zinahusu uteuzi, gharama, malipo na nidhamu za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama ambapo mchakato huo ulikamilika mwaka 2017 baada ya kupata kanuni hizo ambazo zilitolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, aliongeza Bw. Chuwa.

“Kwa kuanzishwa mafunzo haya na kufuatiwa kwa kutungwa kwa kanuni hizo, hivi sasa Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama zimekuwa ni kada mbili tofauti na hivyo mtu ana uwezo wa kuchagua moja kati ya kada hizo na ndiyo maana baadhi ya washiriki wa mafunzo haya wanasomea kada zote wakati kuna baadhi wanasomea kada moja tu”, alifafanua Kaimu Mkuu huyo.

Kaimu Mkuu huyo aliongeza kuwa, lengo kuu la mafunzo hayo ni kuboresha utoaji huduma kwa jamii, kuongeza weledi na kuhakikisha kuwa Mahakama inakuwa na Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wenye maadili, mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi. Ili kuweza kufikia huko ni muhimu sana kuwa na utulivu wa kutosha na kuzingatia yale yote yaliyopangwa katika ratiba ya mafunzo hayo, ushiriki kamilifu ndiyo utakaowafikisha kwenye utoaji wa huduma bora.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa mujibu wa Kanuni ambapo kupitia kanuni hizo mtu yeyote mwenye nia ya kufanya kazi ya udalali na Usambazaji Nyaraka za Mahakama anapaswa kupata mafunzo hayo.

Akiongelea ubora wa mafunzo Bw. Chuwa alisema, kuanzishwa kwa mafunzo hayo ni mojawapo ya sehemu ya maboresho makubwa yanayoendelea katika muhimili wa Mahakama. Ili kuondoa malalamiko mengi yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi na moja ya eneo lenye kulalamikiwa sana ni ukosefu wa uadilifu wakati wa utekelezaji wa majukumu ambapo kwa kufanya hivyo kutawawezesha Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata kanuni zilizopo.

Akiwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo Bw. Chuwa alisema, Madalali wa Mahakama ni wadau muhimu sana katika utekelezaji wa jukumu la utoaji haki kwa wananchi. Endapo mtafanikiwa kuhitimu mafunzo yenu na kusajiliwa mtakuwa maafisa wa Mahakama ambao mtapewa jukumu la kutekeleza amri halali za Mahakama. Jukumu hilo msipolitekeleza vyema mtalalamikiwa kwa kutokuwatendea haki wananchi na kwa hiyo ni dhahiri kuwa Mahakama pia itakuwa imelalamikiwa.

Niwasihi kuwa baada ya kupata mafunzo haya mkazingatie kanuni na maadili mtakayofundishwa katika kutelekeleza majukumu yenu. Nafahamu kuwa mtajifunza mambo mengi sana katika kipindi hiki cha wiki mbili, yakiwemo masuala ya maadili katika fani ya udalali na usambazaji nyaraka za Mahakama, “kila fani ina maadili yake, wale watakaopata nafasi ya kufanya kazi ya udalali au usambazaji nyaraka za Mahakama ni muhimu kuzingatia maadili ya kazi hiyo”, alitilia mkazo Kaimu Mkuu huyo.

Bw. Chuwa akatoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo kuwa, wakati mnaendelea na mafunzo wekeni ndani yake pia mijadala huru itakayowasaidia kuboresha utendaji kazi wenu ili kupunguza malalamiko yanayotokana na wananchi kutokupata huduma bora. Msisite kuchangia uzoefu wenu kwa lengo la kuboresha na kuwaeleza wengine kipi kinachotakiwa kufanyika au kueleweka. Kwenu washiriki kosa hata liwe dogo sana katika utekelezaji wa majukumu yenu linaweza kuleta madhara makubwa sana kwa mtu binafsi, Familia, Mahakama na Taifa kwa ujumla.


Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa amewakumbusha washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama (hawapo pichani) kuwa mafunzo hayo yameanzishwa mahsusi kwa lengo la kuweka utaratibu rasmi wa kurasimisha namna ya kuwapata Madalali pamoja na Wasambaza Nyaraka za Mahakama.

Picha ya pamoja ya washiriki wa Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa na meza Kuu mara baada ya Mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Sheria kwa Vitendo Jijini Dar es salaam, (katikati) ni mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa, kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Masjala Kuu, Mhe. Victoria Nongwa na kushoto ni Mhadhiri na mratibu wa mafunzo ya Udalali na Usambazaji Nyaraka za Mahakama – Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bi. Hamisa Mwenegoha.

Picha ya pamoja ya washiriki wa Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa na meza Kuu mara baada ya Mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Sheria kwa Vitendo Jijini Dar es salaam, (katikati) ni mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa, kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Masjala Kuu, Mhe. Victoria Nongwa na kushoto ni Mhadhiri na mratibu wa mafunzo ya Udalali na Usambazaji Nyaraka za Mahakama – Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bi. Hamisa Mwenegoha.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa kwenye chumba cha mafunzo hayo wakimsikiliza mwezeshaji wa mafunzo hayo (hayupo pichani) yatakayo tolewa kwa muda wa wiki mbili Jijini Dar es salaam.

 

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa kwenye chumba cha mafunzo hayo wakimsikiliza mwezeshaji wa mafunzo hayo (hayupo pichani) yatakayo tolewa kwa muda wa wiki mbili Jijini Dar es salaam.


Friday, December 3, 2021

HESHIMUNI KILA MTU BILA KUJALI UMRI, HADHI AU NAFASI YAKE KATIKA JAMII: JAJI KIHWELO

Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo amewataka Naibu Wasajii na Watendaji kuwa waadilifu, wachapa kazi na kuheshimu kila mtu bila kujali umri, hadhi yake au nafasi yake katika Jamii. Aliyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo elekezi yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Dkt. Kihwelo aliwaeleza washiriki hao kuwa hawakupata nafasi hiyo kwa bahati bali walistahili kutokana na sifa zao za  utendaji kazi uliotukuka na kutokuwa na bila shaka watazitumikia nafasi hizo kwa bidii na uadilifu huku wakiheshimu mamlaka, madaraka na majukumu waliyonayo na yale ya wale watakaofanya nao kazi.

Aliendelea kuwasisitiza washiriki hao kuwa wao ni injini ya Mahakama hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu ili walio chini yao wafuate nyayo zao. 

“Ni tegemeo la kila mmoja wetu kuwa nyinyi ndio mtakuwa kioo cha tabia njema na sio kinyume chake” alisema Dkt. Kihwelo.

Hatahivyo, Dkt. Kihwelo aliwaasa viongozi hayo kuwa wasimamizi wazuri wa maadili na nidhamu katika maeneo yao ya kazi na kuongeza kuwa wao ni viongozi hivyo wanapaswa kuwa watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi  yenye kuzingatia hekima na busara kwa faida ya watumishi, wadau, Mahakama na Taifa.

Akitaja sifa kubwa iliyopo Mahakamani kuwa ni Upendo, Udugu na Mshikamano,  aliwatoa wasiwasi kwa kuwaeleza kwamba wasiwe na shaka kwani watapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa watangulizi wao pamoja na wale watakaowakuta vituoni.

 “Naamini ninyi pia mtatoa ushirikiano na niwaase pia kuwa msisite kuwafundisha mambo mapya ambayo hawayajui lakini pia muendelee kuwa wanafunzi wazuri kwani Wahaya wanamsemo usemao Experience is a Good Teacher” aliongeza.

Kwa upande wake Mhe. Happines Ndesamburo akitoa shukrani kwa niaba ya Naibu Wasajili kwa kuushukuru uongozi mzima wa mahakama kwa kuwawezesha kwa mara ya kwanza wasajili hao kupata mafunzo hayo elekezi.

Mhe. Ndesamburo alieleza kuwa mafunzo haya yatakuwa ni nyenzo muhimu katika utendaji wao wa kazi za kila siku ili kufikia dira na dhima ya mahakama ya utoaji haki kwa wote na kwa wakati. 

Aliongeza kuwa mafunzo waliyopata yamewaandaa vyema na kuahidi kwamba watakapokuwa kwenye vituo vyao vya kazi watatoa huduma za  kiwango cha juu na kuhakikisha kwamba wateja wao watatoka wakiwa wameridhika.  

Kwa upande wa Watendaji wa Mahakama Bw. Tutubi Mangazeni Mtendaji wa Mahakama Kuu Tanga akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watendaji wa mahakama walioshiriki mafunzo hayo alisema kuwa mafunzo haya yamekuwa ya umuhimu sana kwao kwani yamewajengea uwezo na kujifunza mambo mengi ambayo walikuwa hawayafahamu.

Bw. Mangazeni alitoa pendekezo kwa uongozi wa Chuo kwamba kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo ni vyema naibu wasajili na watendaji wa mahakama ambao hawajapata mafunzo hayo wapewe fursa ya kupata mafunzo kama hayo  ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi.

Mafunzo haya ya siku tano kwa naibu wasajili na watendaji wa mahakama yalifunguliwa na Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mnamo tarehe 29 Novemba, 2021 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja  na Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wa mwaka 2018/19-2022/23.

Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo akifunga rasmi mafunzo elekezi kwa naibu wasajili na watendaji wa mahakama yaliyofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 29 Novemba mpaka 03 Desemba, 2021

Mhe. Happiness Ndesamburo Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufaa na mshiriki  akitoa neno la shukurani kwa niaba ya washiriki wa upande wa Naibu Wasajili

Bw. Tutubi Mangazeni Mtendaji Mahakama kuu Tanga mshiriki  akitoa neno la shukurani kwa niaba ya washiriki wa upande wa Watendaji wa Mahakama

Picha ya juu na chini ni baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi ya Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama wakipokea vyeti vyao baadha kumalizika kwa mafunzo hayo ya siku tano.





Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akiwa katika picha cha pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi ya Naibu Wasajili na Watendani wa Mahakama. 

Thursday, December 2, 2021

KLABU YA HerForShe YASHIRIKI MAADHIMISHO YA UKIMWI


Desemba 1 kila mwaka ni siku ambayo dunia huadhimisha Siku ya UKIMWI. Nchini Tanzania kauli mbiu ya maadhimisho ya siku hiyo yalikuwa “Zingatia Usawa, Tokomeza Ukimwi, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko”.

Kitaifa maadhimisho haya yalifanyika mkoani Mbeya wakati kwa upande wa mkoa wa Tanga yalifanyika wilaya ya Muheza na katika ngazi ya wilaya ya Lushoto yalifanyika katika kata ya Mwangoi, jimbo la Mlalo.  Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lushoto Bi Ikupa Mwasyoge.

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kilishiriki katika maadhimisho hayo kupitia klabu ya HeForShe. HeForShe ni klabu ya wanachuo iliyoanzishwa na mwaka 2016 na Mkuu wa Chuo, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo Jaji wa Mahakama ya Rufani. Klabu hii ilianzishwa kwa lengo la kuhamasisha masuala ya kijinsia Chuoni. Klabu hii inatumia mtoto wa kiume katika kuinua nafasi ya mtoto wa kike.  Klabu inafanya shughuli mbalimbali za uhamasishaji na kutoa elimu katika shughuli nyingi zinazofanyika wilayani Lushoto hususani katika mashule na maadhimisho.

Akizungumza na wananchi katika maadhimisho hayo, Bi. Ikupa aliwakumbusha wananchi mambo mbalimbali ambayo bado yanapelekea ongezeko la maambukizi mapya ambayo ni pamoja na vitendo vya ukatili vinavyofanyika katika jamii, mila potofu za kurithi wake na vijana wengi kujihusisha na ngono isiyo salama.

Bi. Ikupa alisisitiza kuepuka kuwanyanyapaa watu wenye maambukizi.  Pia aliendelea kuwashawishi wananchi kujitokeza kupima na wale wote watakaopimwa na kukutwa na maambukizi kujitahidi kutumia dawa kwa uaminifu ili kuimarisha afya zao na kuwa na uwezo wa kuendelea na majukumu yao ya kila siku.

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kupitia klabu ya HeForShe inaungana na jamii ya wananchi wote wa Lushoto katika kukemea vikali mambo yote yanayopelekea maambukizi ya UKIMWI.



Baadhi ya wanaklabu ya HerForShe wakionyesha igizo la kuelimisha jamii kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI yaliyofanyika kiwilaya katika kata ya Mwangoi, Jimbo la Mlalo Wilayani Lushoto.

Wednesday, December 1, 2021

WATUMISHI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUTOA ELIMU YA MAHAKAMA KWA WANANCHI – JAJI CHANDE

Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman amewataka Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama Tanzania kutoa elimu kwa wananchi juu ya utendaji kazi wa mahakama na kuacha kuwa na hisia hasi kwani Mahakama ndicho chombo cha mwisho katika utoaji haki.

Akitoa mada kwa viongozi hao wakati wa mafunzo elekezi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Novemba 30, 2021, Mhe. Othman aliwapongeza kwa kuteuliwa na kuwakumbusha kuwa mwananchi wa kawaida anatamanani kuona shauri lake linamalizika mapema ili ajue hatma yake.

Mhe. Othman aliendelea kwa kuwaasa Naibu Wasajili na Watendaji hao  kuzingatia maadili na kuiishi miiko ya Mahakama na kutokuwa na makundi maofisini kwani wao wanaenda kutatua migogoro na sio kutengeneza.

Aidha, Mhe. Othmani aliwasisitiza viongozi hao kuwa na maono mazuri juu ya maendeleo ya Mahakama ili kurudisha imani kwa jamii juu ya utendaji wa shughuli za Mahakama ya Tanzania na kuleta mabadiliko ya kweli. Mhe. Othman alitumia wasaa huo kusisitiza uwajibikaji, kujenga utamaduni wa kufikika na kutoa maamuzi kwa wakati na kwa weledi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

 “ Kila mmoja wenu ni Kiongozi atumie maarifa yake kuisaidia Taasisi na kumsaidia Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi”.

Mhe. Othman aliendelea kwa kusema kuwa uboreshaji mkubwa na ufanisi umetokana na kuanzishwa Tume huru ya Utumishi wa Mahakama na pia kutenganisha kada mbili za taaluma ya watendaji na wasajili, kwa maana ya Watendaji kushughulika na masuala ya utawala na fedha na Wasajili kushughulikia masuala ya utaratibu wa mashauri mahakamani.

Jaji Mkuu huyo mstaafu aliwaelezea washiriki hao kuwa matokeo chanya ya uboreshaji wa huduma za mahakama yameonekana katika utendaji kazi ambapo hivi sasa kuna mahakama  inayotembea, mfumo wa kieletroniki wa utowaji wa haki  ikiwemo kusajili mashauri kwa njia ya mtandao.

Mafunzo haya  ni yale yaliyofunguliwa na Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mnamo tarehe 29 Novemba, 2021 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja  na Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama wa miaka mitano wa mwaka 2018/19-2022/23.



Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akiwasilisha mada ya Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania kwenye mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Picha ya baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Pichani  washiriki wa mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama kwenye picha  wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto