Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma

Jaji kiongozi wa Tanzania

Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania (katikakati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa stashahada ya sheria

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Friday, June 24, 2022

IJA YASAINI MKATABA WA USHIRIKIANO NA TAASISI YA PAMS FOUNDATION

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kimeingia makubaliano ya Ushirikiano na Taasisi ya PAMS Foundation wenye lengo la kuwajengea uwezo maafisa wa Mahakama wa namna bora ya kuendesha mashauri yahusuyo makosa dhidi ya wanyamapori pamoja na makosa mengine ya uhalifu wa kimataifa (international serious crimes).

Makubaliano hayo yanalenga pia kuijengea uwezo IJA katika eneo la utafiti kwenye maeneo ya makosa makubwa ya kimataifa ikiwemo makosa ya ujangili wa wanyama pori na misitu.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo tarehe 23/06/2022 jijini Dar es Salaam kati ya Jaji Dkt. Paul Faustin Kihwelo, Jaji wa Rufani na Mkuu wa Chuo pamoja na Bi Krissie Clark, Mkurugenzi Mtendaji na miongoni mwa waasisi wa PAMS Foundation yenye Makao yake makuu jijini Arusha.

PAMS Foundation ni shirika lisilo la kiserikali  lenye dhamira ya kuwawezesha wale wote wanaolinda wanyamapori na misitu.




Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PAMS Foundation, Bi. Krissie   Clark (kushoto), wakibadilishana mkataba huo


Mkurugenzi wa Operationi na Mafunzo, Bw.Samson Kassala( wa kwanza kushoto)na na  Mkurugenzi wa Intelijensia na Uchambuzi,(wa pili kushoto) Bw.Elisifa  Ngowi wakisaini mkataba huo. 


Mkurugenzi wa Operationi na Mafunzo, Bw.Samson Kassala( wa kwanza kushoto)na na  Mkurugenzi wa Intelijensia na Uchambuzi,(wa pili kushoto) Bw.Elisifa  Ngowi wakifuatilia utiaji saini huo. 




Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto , Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (kulia) akimpatia machapisho mbalimbali ya Chuo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PAMS Foundation, Bi. Krissie   Clark (kushoto).


Wednesday, June 15, 2022

IJA YAENDESHA MAFUNZO YA NAMNA BORA YA UTOAJI WA ADHABU NA UTEKEZAJI WA AMRI ZA MAHAKAMA

 Na Ibrahim Mdachi – IJA Lushoto

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania chini ya ufadhili wa Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Tanzania zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (BSAAT) kimeendesha mafunzo ya siku tatu kwa Mahakimu 43 kuhusu namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama. Mafunzo hayo yalianza tarehe 13 Juni, na kuhitimishwa tarehe 15 Juni, 2022 Chuoni hapo.

Akifungua mafunzo hayo rasmi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma  aliwataka Mahakimu kuzingatia mwongozo wa adhabu na kujiepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kujenga jamii inayojali haki kwa kila mmoja na kuwafanya wananchi waendelee kuwa na imani na Mahakama.

Alitanabaisha pia kuwa kimsingi mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na uelewa wa mwongozo wa utoaji adhabu ambao ni miongoni mwa nyenzo za maafisa wa Mahakama katika mchakato wa utoaji wa adhabu kuwa halali na usiotiliwa shaka na wadaawa wanaohusika katika mashauri mahakamani wakiwemo washtakiwa, waathiriwa, wapelelezi, mawakili wa utetezi, waendesha mashtaka na umma kwa ujumla.

Mhe. Chuma alisema kuwa ni matarajio ya Mahakama ya Tanzania kupitia mafunzo hayo washiriki watapata uelewa wa mwongozo wa utoaji adhabu, hivyo kutumika ipasavyo katika mashauri hasa ya rushwa, uzoefu utakaopatikana utafikishwa kwa maafisa wengine wa Mahakama ambao hawakufanikiwa kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Mratibu wa Programu ya BSAAT ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha  akitoa maelezo mafupi kuhusu mradi huo alisema kuwa, program hiyo inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kwa kushirikana na Umoja Ulaya (EU) na kuratibiwa na Ofisi ya Rais, Ikulu ilianza kutekelezwa mwaka 2018/2019 ikijumuisha taasisi tisa nufaika ambazo ni wadau katika mnyororo wa haki jinai ikiwemo Mahakama kama mdau muhimu katika utiaji wa haki.

Bw. Magoha aliongeza kuwa program hiyo imelenga kupunguza vitendo vya rushwa kama kikwazo cha kupunguza kiwango cha umasikini kwa Watanzania, kuboresha uadilifu, kuboresha uwezo na uratibu wa mfumo wa haki jinai katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na kuongeza imani kwa umma juu ya utendaji kazi wa Mahakama.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo Bw. Goodluck Chuwa alisema kuwa, ni takribana miaka mitano tangu chuo kimeamua kujikita katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuundwa kwake kitahakikisha kuwa kinaendelea kuyaratibu mafunzo mbalimbali kwa weledi mkubwa kwa lengo la kuleta tija kwa Mahakama na wadau wengine wa sheria nchini.

Mafunzo haya  ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021-2025, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja  na Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wa miaka mitano wa mwaka 2018-2023.

                                                           

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma  akifungua mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama kwa Mahakimu 43 kutoka Mikoa Mbalimbali ya Tanzania yanayofanyika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.


 Hakimu Mkazi Mkuu  wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Richard Kabate akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya  namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama.



 Pichani ni baadhi ya washiriki wa mafunzo katika picha ya pamoja na Mhe. Wilbert Chuma, (Mgeni Rasmi) wakiwa ameketi na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya Lushoto, Mhe. Rose Ngoka na Kaimu Mkuu wa Chuo Bw. Goodluck Chuwa (upande wake wa kulia)  na Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha Na Utawala, Prof. Fatihiya Massawe na Naibu Mkurugenzi wa Utawala, Mahakama ya Tanzania na Mratibu wa Mradi wa BSAAT nchini Bwn. Stephen Magoha (Upande wa Kushoto)

 

Picha ya juu na chini ni picha ya washiriki wa Mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama wakiendelea na mijadala mbalimbali katika mafunzo hayo.