Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, amewataka majaji
walioteuliwa na kuapishwa hivi karibuni kumwogopa Mungu na kutimiza
majukumu yao kwa kufuata Sheria, Katiba na kwa kuzingatia maadili na
viapo vyao.
Mhe. Jaji Mkuu alitoa wito huo Mei 31, 2021 alipokuwa akifungua mafunzo
elekezi kwa majaji hao, saba wa Mahakama ya Rufani, 21 wa Mahakama
Kuu ya Tanzania na watatu kutoka Mahakama Kuu ya Zanzibar,
yanayofanyika katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Aliwakumbusha majaji hao kuwa katika Karne ya 21, idadi ya sheria
zimeongezeka huku kasi za marekebisho ya sheria hizo nazo ikiwa
zimeongezeka, hivyo Jaji anapaswa kujiridhisha kama kuna marekebisho
ya sheria inayohusu jambo lililo mbele yake.
“Tukumbuke kuwa sheria zimejiingiza sana katika shughuli za kila siku za
kiuchumi, kibiashara, kijamii, kisiasa na kugusa maisha ya kawaida ya
wananchi wengi zaidi. Kwa hiyo, majaji, kama watafsiri wa mwisho wa hizo
sheria nyingi, mnatakiwa kuwa watu wa Mungu ili kuhakikisha kuwa
mamlaka ambayo wananchi wamejibakizia kwa mujibu wa Katiba
hayaingiliwi na Mihimili mitatu ya Dola,”alisema.
Jaji Mkuu alibainisha kuwa utashi wa nafsi ya jaji, ubinadamu wake na
ubuntu wake lazima uwe wenye kumwogopa Mungu kwa kutambua kuwa
ingawa Katiba na Sheria zimewapa mamlaka makubwa na ya mwisho
katika jambo la utoaji haki, lazima watambue kuwa kuna Mwenyezi Mungu
wa kumwogopa na kuna ubinadamu na ubuntu wa kuheshimu.
“Vinginevyo unaweza kutumia sheria kufifisha haki ambazo wananchi,
kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano, wamejiachia wao wenyewe.
Katiba ni sauti ya wananchi. Katiba imefafanua wananchi wamekopesha
mamlaka gani kwa mihimili ya Dola,” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, wananchi wamebakisha mamalaka yote ambayo
majaji hawatakiwi kuyaingilia kupitia sheria zilizotungwa na Bunge na
kupitia maamuzi ya kimahakama na utekelezaji wa shughuli za serikali.
“Ukweli kuwa wananchi wamebaki na haki zao za msingi umebainishwa
katika utangulizi wa misingi ya Katiba inayotukumbusha sisi majaji na
vingozi wote wa umma kuwa tumekopeshwa mamlaka chache ambayo
tunapaswa kuyatuma kwa manufaa ya wananchi,” alisema.
Prof Juma amekishukuru Chuo cha Uongozi wa Mahakama, kupitia Mkuu
wa Chuo hicho, Dkt Paul Fauatine Kihwelu, kwa kuandaa mafunzo hayo ili
kuwatayarisha majaji hao kufanya kazi ya ujaji wa Mahakama Kuu na
Mahakama ya Rufani kwa ukamilifu.
Aliwakumbusha Majaji hao pia kuwa mafunzo hayo elekezi
yatawatayarisha kuwa sehemu ya Dira na Mpango Mkakati wa Mahakama
na hivyo kuwa sehemu muhimu ya nguzo za mpango mkakati wa
mahakama na sera mbali mbali zinazohusu mahakama.
“Lengo hapa ni kuhakikisha kuwa mnavuka kwa haraka kipindi cha
kujifunza kazi za ujaji na mnaanza mara moja majukumu yenu ya ujaji
mahakamani mara baada ya mnafunzo haya elekezi,” alisema Jaji Mkuu.
Alibainisha pia kuwa Mahakama ya Tanzania inatambua kuwa kadri dunia
inavyopitia mageuzi makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia kupita Mapinduzi
ya Nne ya viwanda, hugusa sana taratibu zilizopo za utoaji haki.
Jaji Mkuu alieleza kuwa kama majaji na mahakimu hawatapata mafunzo
endelevu mara kwa mara watajikuta wanaachwa mbali sana na mageuzi ya
kimaboresho. Hivyo, alisema kuwa Uongozi wa Mahakama ya Tanzania
umetoa kipaumbele kwa mafunzo elekezi na endelevu kwa majaji na
mahakimu ili kuboresha ufanisi, ujuzi, weledi na uwazi.
“Ni matumaini yangu kwa mafunzo haya elekezi yatawasidia kujenga
misingi ya positive attitude (Mtazamo chanya). Mada Mtakazopata katika
maeneo ya maboresho yatalenga kuwajengea mitazamo ya kimaboresho
na kuondoa negative attitudes (Mitazamo Hasi),” alisema.
Jaji Mkuu pia aliwakumbusha Majaji hao kwa ni viongozi katika nchi
maskini yenye wananchi wenye matarajio kuwa kazi ya viongozi ni
kuwaboreshea maisha, husuani utoaji wa haki. Alibainisha kuwa yapo
maeneo mengi ambayo sifa za uongozi za kila mmoja hujipambanua
wakati wa kutoa maamuzi.
Alisema kuwa kazi kubwa ya Jaji ni kusikiza na kupata ushahidi au
kusikiliza hoja ili zimsaidie kutumia sheria na kufikia uamuzi.
“Kumbukeni kuwa kiongozi mzuri mahakamani ni yule anayehakikisha
mahakama yake inatambua kuwa mwananchi aliye mbele yake ana haki
zake zote za msingi kwa mujibu wa Katiba, ikiwa pamoja na haki ya
kusheshimiwa na utu wake kuthaminiwa,” alisema.
Kuhusu maadili, Jaji Mkuu alisema kuwa uadilifu na maadili mema
husafisha nafsi na kuwawezesha kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba na
masharti ya viapo vyao.
Alibainisha kuwa kunapotokea ukiukwaji wa sheria watu wengi hukimbilia
kudai sheria mpya au marekebisho ya sheria iliyopo na kusahau kuwa
sheria sio mbaya, bali nafsi, maadili na hata tabia za wanaotekeleza sheria hizo ndizo mbaya.
0 comments:
Post a Comment