WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA ATAMBUA MCHANGO WA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO KATIKA KUTOA MAFUNZO KWA WADAU WA UTOAJI HAKI NCHINI.
Waziri wa Katiba na Sheria,
Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi ametambua mchango wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama- Lushoto katika kutoa mafunzo ya utoaji haki nchini.
Waziri Kabudi ameongea hayo
alipokuwa akihutubia kwenye mahafali ya Ishirini na Moja ya Chuo hicho
yaliyofanyika tarehe 12 Novemba, 2021 Chuoni Lushoto.
Waziri Kabudi alisisitiza kuwa
umuhimu wa Chuo kuwa kitovu cha kutoa mafunzo sio tu kwa Mhimili wa Mahakama,
bali pia kwa Taasisi za Umma zinazohitaji elimu endelevu inayolenga kuboresha
utoaji haki na usawa katika jamii.
Waziri Kabudi amewaomba
wahitimu katika mahafali hayo kutumia hatua waliyofikia kuwa chachu ya
kujiendeleza zaidi kwenye elimu kwani ulimwengu wa sasa unahitaji zaidi watu
wenye ujuzi na maarifa ya kutosha.
Waziri Kabudi aliendelea kwa
kusema kuwa tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho, mhimili wa Mahakama ndiyo mnufaika
mkubwa wa zao la kitaaluma la Chuo hicho kwani mhimili huu umeweza kuendeleza
watumishi wake pamoja na kuajiri mahakimu na watumishi wengine kutoka katika
Chuo hiki. Aliongeza kwa kusema pamoja na hayo yote Chuo pia kimekuwa
kikiratibu na kufanya mafunzo endelevu ya kujengea uwezo watumishi mbalimbali
wa mahakama.
Waziri Kabudi aliongeoza
maandamano na kutunuku stashahada na astashahada kwa wahitimu wa Chuo hicho
pamoja na kutaja mambo sita ambayo yameipaisha Tanzania duniani na kuibuka kuwa nchi ya mfano wa kuigwa
inapoelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wake.
Mambo yaliyotajwa na Waziri Kabudi
ni pamoja na misingi iliyoachwa na baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere ya kuondoa ukabila nchini na kuifanya Tanzania kuwa taifa badala ya
mkusanyiko wa makabila, taifa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya muda
uliotazamiwa yaani mwaka 2025, uwezo wa taifa kudumisha na kuenzi tunu ambazo
ni amani,umoja,mshikamano,utu,haki,heshima ya mwanadamu, uhuru na demokrasia.
Mambo mengine aliyotaja Waziri ni uthubutu wanchi yetu kuendesha miradi mikubwa
kwa kutumia rasilimali na fedha zake za
ndani, uwezo wa taifa kuzifanya rasilimali zilizokuwa za Watanzania
ikiwemo kuvunja mikataba mibovu ambayo haikuwa na tija kwa taifa na jambo la
mwisho lililotajwa na Mhe. Prof. Kabudi ni ukomavu wa kisiasa na ukatiba katika
taifa letu.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi
wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mheshimiwa Dkt. Gerald A. M. Ndika
amesema Chuo kimekabidhiwa majukumu ambayo ni kutoa mafunzo, kufanya tafiti na
kutoa huduma za kitaalamu majukumu ambayo Chuo kinamudu kuyatekeleza kwa
ufanisi.
“Sera ya mafunzo ya mahakama
ya mwaka 2019 imebainisha kuwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ni kitovu na wakala wa mafunzo na utafiti wa Mahakama
Tanzania na kutokana na hilo tumeendelea kuboresha utendaji kazi wa Chuo ikiwemo
kurugenzi ya mafunzo endelevu ya kimahakama” amesema Dkt. Ndika.
Kwa upande wake, Jaji wa
Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ametaja changamoto
zinazokikabili Chuo ikiwepo ufinyu wa bajeti,kutopewa kibali cha kuajiri, uchakavu
wa miundombinu na uchache wa mabweni ya wanachuo.
Mkuu huyo wa Chuo aliendelea
kwa kusema kuwa uchakavu wa miundombinu unatokana na majengo ya chuo kuwa
makongwe ambapo yanalazimika kukarabatiwa ili kutumika kwa usalama.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Kihwelo
alieleza kwamba pamoja na changamoto zilizopo Chuo kimeendelea kufanya majukumu
yake ya kitaaluma kama Chuo kilivyokusudiwa kuyafanya. Na pia aliupongeza
uongozi mzima wa Mahakama ya Tanzania kwa kukiamini Chuo.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto,
Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akizungumza wakati wa sherehe
hizo. |
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho. |
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati
waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa chama cha wanafunzi
waliowahi kusoma katika chuo hicho. |
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati
waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wahitimu wa Astashahada ya
Sheria. |
Mmoja wa Wahitimu wa Stashahada ya Sheria ambaye ni
mshindi wa masomo kadhaa akipokea zawadi ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma aliyotoa kwa washindi wote katika masomo. |
0 comments:
Post a Comment