Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameahidi kushirikiana na Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ili kiweze kutekeleza majukumu yake
kikamilifu, ikiwemo kutoa wahitimu bora watakaolisaidia taifa katika maeneo
mbalimbali ya maendeleo.
Prof. Ole Gabriel, ambaye ni Katibu wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama alitoa ahadi hiyo katika ziara ya Tume iliyofanya katika
Chuo hicho hivi karibuni kutembelea maeneo mbalimbali, likiwemo Jengo la Hostel
ya Wavulana ambalo linajengwa kwa kugharamiwa na Mahakama ya Tanzania katika
mpango wa uboreshaji wa majengo chuoni hapo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la
Chuo, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani aliupongeza
uongozi wa Chuo kwa jitihada zake inazozifanya katika kutoa mafunzo yanayolenga
kuwajengea uwezo watumishi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.
Katika ziara hiyo, ambayo ni mwendelezo wa shughuli
mbalimbali zinazofanyika kuelekea siku ya mahafali ya ishirini na moja ambayo
inafanyika tarehe 12 Novemba, 2021, Prof. Ole Gabriel ameambatana na Makamishna
mbalimbali wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Wajumbe wa Tume hiyo pia walipata nafasi ya kukutana
na menejimenti ya Chuo ambapo walifanya majadiliano yaliyolenga kuboresha
huduma zinazotolewa na chuo hicho. Katika kikao hicho, Katibu wa Tume hiyo
ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama alitoa salamu kwa niaba ya wajumbe wa Tume
hiyo.
Prof. Elisante aliiambia Menejimenti kwamba Chuo kina
wajibu mkubwa kwa Mahakama ya Tanzania na Taifa kwa ujumla katika kutoa elimu
ambayo italeta matokeo chanya kwa taifa sio tu kwa kufaulu katika mitihani
mbalimbali bali kutoa wanafunzi waliobora ambao wanaweza kufanya kazi popote na
katika mazingira yoyote.
Mhe. Dkt Paul Kihwelo akiwa na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama akipitishwa katika maeneo mbalimbali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wakati wa ziara ya siku moja |
Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakipata maelezo kuhusu jengo la bweni la wavulana ambalo linajengwa kwa kupitia fedha za mahakama ya Tanzania kutoka kwa Afisa Miliki wa Chuo Bwana George Masanja |
Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Mahakama wakiwa katika picha ya pamoja na wanachuo wa Stashahada ya Sheria mwaka wa pili walipotembelea hivi karibuni katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto |
Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, Baraza la Uongozi wa Chuo wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Chuo walipokuwa kwenye ziara ya siku moja chuoni hapo hivi karibuni |
Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Mahakama na Baraza la Uongozi wa Chuo wakiwa katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto walipokuwa kwenye ziara ya siku moja chuoni hapo hivi karibuni |
0 comments:
Post a Comment