Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Monday, March 21, 2022

WANAWAKE IJA WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE KWA KUTEMBELEA WAFUNGWA

Watumishi wanawake wa Chuo cha uongozi wa Mahakama Lushoto katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani kama ilivyo ada, mapema leo machi 8, 2022 wametembelea wafungwa wa Gereza la Wilaya ya Lushoto na kutoa msaada wa mahitaji ya kibinadamu wa vifaa mbalimbali vikiwemo taulo za usafi kwa Wanawake, Sabuni za kufulia na kuogea, dawa za meno na miswaki, mafuta ya kupaka na dawa za mbu.

 Akikabidhi msaada huo, mwenyekiti wa watumishi wanawake wa chuo alisema kuwa, lengo la kwenda gerezani hapo ni kuwafariji na kuwatia moyo ili wasikate tamaa kwani hakuna binaadamu aliye mkamilifu hivyo na kuongeza kuwa, pamoja na kuwa wako katika kutumikia adhabu zao ni vyema kuwakumbuka na kuwakumbusha kuwa wao ni sehemu ya jamii na inawathamini kama walivyo binaadamu wengine.


Baada ya zoezi la kutembelea wafungwa, wanawake wa IJA walipata nafasi ya kukaa pamoja na Uongozi wa Chuo kwenye tafrija fupi iliyoandaliwa na Chuo kwenye hotel ya Mullers Lodge iliyoko Wilayani Lushoto.  Akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Chuo kwenye ufunguzi wa tafrija hiyo, Mhadhiri Dkt. Ismail Hokororo aliwapongeza wanawake hao kwa kujitokeza na kuenzi maadhimisho ya siku ya Wanawake na kusema kuwa Chuo kinatambua na kuthamini  mchango wa Mwanamke katika jamii na  kipo  tayari kuwasikiliza na kutoa ushirikiano unaostahili pale utakapohitajika  na kuwahakikishia mazingira mazuri ya kufanya kazi yanayozingatia usawa kwa maendeleo ya mwanamke.


Dkt. Hokororo aliendelea kusema kuwa Menejimenti ya Chuo inaunga mkono jitihada zote zinazoibuliwa na wanawake zinazolenga kujenga umoja, uzalendo, mshikamano kwa ustawi wa chuo na Taifa kwa ujumla.

“Nyote ni mashahidi wa jitihada zinazoendelea katika kuboresha uwiano wa kiutumishi kwa wanawake na wanaume chuoni, hasa katika maeneo yale yaliyo chini ya mamlaka ya Menejimenti ya Chuo” alisema Dkt. Hokororo.


Dkt. Hokororo aliwatia moyo wanawake hao kuendelea kushirikiana na kubadilisha uzoefu huku wakiandaa mipango endelevu kwa mustakabali wa Maendeleo ya Wanawake na jamii kwa ujumla.

Katika kuadhimisha siku hiyo pia wanawake wa IJA walipitishwa kwenye mada mbili ambazo ziliandaliwa na Chuo kwa ajili ya kuwapa uelewa zaidi juu ya masuala ya siku ya wanawake ambazo zilikuwa ni mada ya Nafasi ya Mwanamme katika kumkomboa mwanamke na mada ya pili iliyohusu Umuhimu wa Wanawake Kujiunga Pamoja.

 

Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani hufanyika Machi 8 kila mwaka, kiwilaya maadhismisho haya yamefanyika katika kijiji cha Gare ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria na kutoa salamau zao kuhusu masuala mbalimbali ya haki na usawa kwa jinsia na pia kusisitiza juu ya umuhimu wa kuhesabiwa sambamba na dhima ya mwaka huu isemayoKizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu: Tujitokeze kuhesabiwa’’. Dhima hii inaenda sambamba na mpango wa serikali wa kuendesha zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi septemba, 2022 nchini.


Dkt. Joseph Hokororo Ismail, Mhadhiri wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akitoa Salamu za Siku ya wanawake kwa niaba ya Mkuu wa Chuo, pembeni kwake ni Mwenyekiti wa watumshi wanawake wa Chuo Bi. Mariamu George.


Picha ya pamoja ya baadhi ya watumishi wanawake wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto waliohudhuria kwenye tafrija fupi iliyoandaliwa na Uongozi wa Chuo kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya wanawake ulimwenguni.


PICHA ZA CHINI NI PICHA MBALIMBALI ZA MATUKIO YA SIKU YA WANAWAKE 









0 comments:

Post a Comment