Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Wednesday, March 16, 2022

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA ZIARANI IJA

Na: Rosena Suka IJA Lushoto

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wamefanya  ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la ghorofa nne la wavulana lenye thamani ya shilingi za kitanzania billioni 2.64  lenye uwezo wa kulaza wanachuo 320. Mradi huu unasimamiwa na Mahakama ya Tanzania katika mpango wa Maboresho ya Mahakama.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa jengo hilo la bweni la wavulana Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa ufafanuzi wa ujenzi wa jengo hilo kuwa umefanyika katika awamu tatu tofauti ambazo zilisimamiwa na wakandarasi watu watatu kwa nyakati tofauti toka kuanza kwa mradi wa ujenzi huo mwaka 2011.  

Prof. Elisante alitoa maelezo hayo kwa kusema kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo ilikuwa chini ya mkandarasi Beijini Construction Engineering Group ambaye alijenga kuanzia msingi hadi boma. Hatua ya pili ilikuwa ni uwekaji wa mifumo mbalimbli katika jengo hilo chini ya usimamizi wa Mkandarasi Froton Afrika Limited na Mkandarasi aliyepo kwa sasa ni  MS-Works Construction Limited ambaye anaendelea na umaliziaji wa jengo hilo  ambalo litakapokamilika litakuwa na       miundombinu ambayo itawezesha wanafunzi kutoka katika makundi maalum kulitumia.

Pamoja na mengine Prof. Elisante alimalizia kwa kusema kuwa, jengo hilo litakabidhiwa ifikapo Mei, 2022 na linatarajiwa kutumiwa na wanachuo watakaosajiliwa katika mwaka wa masomo 2022/2023 ambapo litapunguza idadi kubwa ya wanachuo wakiume wanaoishi nje ya mazingira ya Chuo.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Tabora Mjini Mhe. Emmanuel Mwakasaka ameipongeza Serikali kwa hatua iliyofikia ya ukamilishwaji wa ujenzi wa Jengo la Bweni la Wavulana la Chuo cha Uongozi wa Mahakama. Hatua ya ujenzi wa bweni hili litakuwa ni mkombozi kwa Chuo kwani litawezesha wanachuo kuweza kuishi ndani ya chuo badala ya kuchanganyika na wenyeji.

“Miradi ya ujenzi wa majengo haya imeenda kwa haraka sana na tumeridhishwa sana na kazi iliyofanyika, pongezi kwa watendaji wote wa Mahakama”, alisema Mhe. Mwakasaka.

Naye, Naibu Waziri, Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Geogrey Pinda (MB) alishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa kutembelea mradi huo na kuahidi kuwa hoja zote zilizotolewa na wajumbe zimepokelewa na zitafanyiwa kazi. Mhe. Pinda pia alitoa mapendekezo kwa Chuo kutumia nafasi waliyonayo kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa mahakama ili kusaidia mabadiliko ya mahakama kwenda sambamba na wataalamu.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri Bw. Goodluck Chuwa ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Chuo kwa kukiwezesha mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa kada mbalimbali wa Mahakama pamoja na wadau wa sheria nchini.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imefanya  ziara ya siku moja ambapo imekagua mradi wa ujenzi wa jengo la bweni la wavulana la Chuo cha Uongozi Mahakama Lushoto  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo ikiwemo kufanya ukaguzi wa miradi ya ujenzi inayosimamiwa na Mahakama ya Tanzania.




Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa maelezo mafupi juu ya ujenzi wa bweni la wavulana kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na viongozi wengi wa Wilaya waliohudhuria katika tukio hilo.



Meza Kuu katika picha ya pamoja naWajumbe waKamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria
Picha ya juu na chini ni mwonekano wa nje na wa ndani wa bweni la wavulana ambalo lipo katika hatua ya ujenzi.

(Picha na Ibrahim Mdachi - IJA Lushoto)


































0 comments:

Post a Comment