Na Rosena Suka IJA
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 30 Agosti, 2022
alifungua mafunzo elekezi yanayowaleta pamoja Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania wapya 21 na wengine wanne wa Mahakama Kuu Zanzibar ambapo amewahimiza
kuzingatia maadili wanapotekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Prof. Juma aliwataka Majaji
hao kusoma na kujadili miongoni mwao Kanuni za Maadili za Maafisa Mahakama
iliyochapishwa tarehe 20 Novemba, 2020 kupitia Tangazo la Serikali Namba 1001
la mwaka 2020 ambazo zitawasaidia kubaki ndani ya matarajio ya kimaadili.
“Uwezo na Maadili ni nguzomuhimu
ya kuaminiwa na kuaminika kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Uwezo, Ujuzi na
Maarifa yenu yatajenga Imani na kuaminiwa kwenu kwa namna ambavyo mtafanya
maamuzi yenu kwa haki, kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Taratibu,
Miongozo, Mila na Desturi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Jaji Mkuu akawakumbusha kuwa
pamoja na maadili ya Viongozi wa Umma; Majaji wa Mahakama Kuu, Majaji wa
Rufani, Wasajili, Mahakimu, na Wasaidizi wote wa Majaji, wanaongozwa na Kanuni
za Maadili za Maafisa wa Mahakama (Code of Conduct and Ethics for Judicial
Officers, 2020).
Amesema uongozi wa Mahakama
ukishirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), umeweka utaratibu
wa Mafunzo elekezi ya awali kwa wote walioapishwa kuwa Majaji wakiwemo wale
wanaojiunga na utumishi wa Mahakama kwa mara ya kwanza.
“Mafunzo elekezi yanalenga
kuwatayarisha kutumikia nafasi ya Jaji. Mafunzo elekezi yanawakaribisha rasmi
katika Utumishi wa Mahakama wenye maudhui, tamaduni, mitizamo na uzoefu
uliojengeka muda mrefu ambazo itawawekea misingi imara ya kuwasaidia katika
utoaji wa huduma za kimahakama,” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha pia kuwa
mafunzo hayo elekezi yanalenga kuwajengea msingi wa kuifahamu Mahakama,
kufahamu mwelekeo wa Mhimili wa Mahakama ndani ya maudhui ya mwelekeo wa nchi
ya Tanzania ndani dunia inayoizunguka.
Akaseama kuwa kwa upande wake
Mhimili wa Mahakama utafaidika na uwezo, uzoefu, ujuzi na umahiri wa Majaji hao
waliojijengea kutoka maeneo waliyopitia, hivyo mchanganyiko huo utakuwa wa
faida kubwa kwao binafsi, kwa Mahakama na pia kwa pande zote mbili za Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
“Jambo moja muhimu ambalo
litajitokeza katika Mafunzo haya elekezi ni dhamira dhahiri ya Mahakama ya
Tanzania kuwaingiza kuwa sehemu ya waboreshaji wa huduma za utoaji haki kupitia
Mipango Mkakati na Programu za Maboresho,” Mhe. Prof. Juma alisema.
Amesema kuwa Maboresho ya
Mahakama yanayoendelea hivi sasa yamewajengea watumishi wa Mahakama utamaduni
mpya, mitazamo mipya na mwelekeo mpya wa utoaji wa huduma za haki kwa kumlenga
na kumridhisha mwananchi (Citizen-Centric Judicial Modernization and Justice
Service Delivery).
“Ninawasihi muwe sehemu ya dhana
hii ya utoaji wa huduma za haki kwa kumlenga na kumridhisha mwananchi. Mafunzo
haya elekezi yanawatayarisha Majaji wapya kuifahamu Dira ya Mahakama ya
Tanzania—Timely and Accessible Justice for All,” Jaji Mkuu alisema.
Aidha, Mhe. Prof. Juma
akabainisha kuwa katika kumlenga na kumridhisha mwananchi, Jaji sio idadi bali
umuhimu wake kwa mwananchi ni huduma bora za haki, ujuzi, ufanisi, na uwazi wa
huduma za utoaji haki kwani wananchi wanafuata huduma mahakamani, wala hawaji
kumtembelea Jaji, wanafuata huduma za utoaji haki.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma akifungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu Zanzibar uliofanyika tarehe 30 Agosti, 2022 katika Ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto,(IJA) Mhe. Dkt. Gerald Ndika na kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Mustapher Siyani
0 comments:
Post a Comment