Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kimeandaa na kuendesha mafunzo kwa Maafisa 27 kutoka Bodi ya Sukari Tanzania. Washiriki wa mafunzo hayo ni Maafisa wa Bodi ya Sukari Tanzania wa ngazi mbalimbali. Mafunzo hayo yanafanyika Chuoni Lushoto kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 23 Mei mpaka 27 Mei 2022.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, alielezea lengo la mafunzo hayo kuwa ni kuwajengea uwezo Maafisa hao kwenye ufafanuzi kuhusu Sheria ya Tasnia ya Sukari, 2002 na Kanuni zake katika kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Mhe. Dkt. Kihwelo alisema kuwa Mahakama ni chombo cha mwisho katika utoaji wa haki, kwani kuna wadau wengine wa sheria ambao wanafanya kazi hizo za kutoa haki kama Maafisa wa Bodi ya Sukari ambao wajibu wao ni kutoa leseni, kusimamia na kudhibiti soko la sukari nchini. Aliwataka kutumia kile watakachojifunza katika kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi wao ili kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Linus Bwegoge, alieleza kwamba Bodi ya Sukari Tanzania ina wajibu wa kutoa huduma za udhibiti na kuratibu maendeleo ya Tasnia ya Sukari Tanzania. Aliongeza kuwa ili kutekeleza kwa ufanisi zaidi sheria ya tasnia ya sukari na kanuni zake menejimenti iliona ni vema kuwaleta maafisa wake kwa ajili ya mafunzo hayo.
Chuo cha IJA kina jukumu la kuwajengea uwezo watumishi wote wa mahakama na mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma za utoaji haki nchini kwa lengo la kuboresha utendaji kazi. Sambamba na mafunzo hayo Chuo kimebobea katika kufanya mafunzo ya Stashahada na Astashahada ya sheria, kufanya tafIti mbalimbali na kutoa ushauri wa kitalaamu.











0 comments:
Post a Comment