Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Monday, August 14, 2023

Msajili mkuu wa Mahakama ya Tanzania afungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya 37

 

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amefungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo leo tarehe 14/08/2023.

Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yanafanyika hapa Chuoni IJA na yatadumu kwa siku tano hadi tarehe 18/08/2023.

Katika hotuba yake ya Ufunguzi Mhe. Chuma ambae ndiye alikuwa mgeni Rasmi  amewataka Mahakimu hao kwenda kusaidia kuondoa mrundikano wa mashauri katika Mahakama za mwanzo kama ambavyo Sera ya Mahakama ya Tanzania inavyotaka.

“Mpaka sasa bado Mahakama za Mwanzo zinaendelea kuongoza katika umalizaji wa Mashauri na kutokuwa na mrundikano wa mashauri, kwa hiyo tunategemea ongezeko lenu litaendelea kupunguza mzigo wa kazi wa kila hakimu na hatimaye kuendeleza sera ya Mahakama ya Tanzania kutaka kusiwe na mashauri yanayozidi miezi sita,” amesema Mhe. Chuma.

Pia Mhe. Chuma amewataka mahakimu wakazi hao wapya kujifunza matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano(TEHAMA) ili waweze kutekeleza vema majukumu yao hasa wakati huu Mahakama ya Tanzania ikiwa imejielekeza katika eneo hilo la Teknolojia.

“Karne hii ya 21 imetawaliwa na matumizi ya Teknolojia katika kuwahudumia wananchi, jifunzeni matumizi ya mifumo ya TEHAMA inayoendeshwa na Mahakama ili msipate ugumu mnapotekeleza majukumu yenu,” amesisitiza Mhe. Chuma.

Vile vile, Mhe. Chuma amewasisitiza washirika hao kuwa wanapotekeleza majukumu yao, basi hawana budi kuzingatia misingi ya haki za binadamu, maisha ya watu na ustawi wa Usalama wa nchi.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda amezungumzia muhimu wa mafunzo hayo kwa kubainisha kwamba yanalenga kuwapatia Mahakimu hao miongozo itakayowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Kimsingi umuhimu wa mafunzo haya ni kwa ajili ya kuwapatia muongozo Mahakimu wapya ambao wanaenda kuanza majukumu yao katika Mahakama za mwanzo, ukiwemo utoaji wa haki ambao ndio jukumu kubwa la Mahakimu hawa,” amesema Mhe. Dkt. Kisinda.

Ameongeza kuwa Mahakimu watapewa miongozo, maelekezo na miiko mbalimbali ambayo inahusiana na majukumu ya kule wanapokwenda kusimamia utoaji wa haki.

Nao baadhi ya Washiriki wa Mafunzo hayo akiwemo  Mhe. Aden William Ruvurahende ambae ni Hakimu Mkazi mpya amebainisha faida ya mafunzo hayo kwao wao washiriki.

“Kwa kweli suala hili la mafunzo kwetu sisi ni la muhimu sana kwa sababu ni mwanzo wa kujua majukumu yetu, na fursa ya kufahamu miongozo na kanuni  ya kimahakama  ili itusaidie kwa ajili ya utendaji haki pale tunapokwenda kuwahudumia wananchi,” amesema Mhe. Ruvurahende.

 Kuhusiana na mlundikano wa mashauri amebaininisha: “Kuhusiana na mrundikano wa mashauri Mahakamani, ni changamoto kwetu sisi ila tunakwenda kusaidia kutatua suala hilo.”

Nae Mshiriki Mhe. Salma Athuman Mwamende anabainisha kuwa Mahakama itarajie weledi, ufanisi, na uwajibikaji kutoka kwao.

 



Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akihutubia wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.


Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akizungumza wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.



Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma(katikati) wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.

Wa pili kushoto ni  Mhe. Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda, wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Bi. Patricia Ngungulu, wa kwanza kulia ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Kavumo Mndeme.




Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma(katikati) akiwa katika picha na baadhi ya baadhi ya Washiriki wa Mafunzo Elekezi ambao ni Wahe. Mahakimu Wakazi wapya wa mahakama za Mwanzo katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).

Wa pili kushoto ni  Mhe. Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda, wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu, wa kwanza kulia ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Kavumo Mndeme.




Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo Elekezi ambao ni Wahe. Mahakimu Wakazi wapya wa mahakama za Mwanzo wakiwa katika mafunzo hayo katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).





Jaji mstaafu ambae pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheira, Mhe. January Msoffe akiwasilisha mada kwa Washiriki wa Mafunzo Elekezi ambao ni Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akihutubia wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.


0 comments:

Post a Comment