Na Ibrahim Mdachi – IJA Lushoto
Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania chini ya ufadhili wa
Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Tanzania zinazohusika
na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (BSAAT) kimeendesha mafunzo ya siku tatu kwa
Mahakimu 43 kuhusu namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za
Mahakama. Mafunzo hayo yalianza tarehe 13 Juni, na kuhitimishwa tarehe 15 Juni,
2022 Chuoni hapo.
Akifungua mafunzo hayo
rasmi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma aliwataka
Mahakimu kuzingatia mwongozo wa adhabu na kujiepuka kujihusisha na vitendo vya
rushwa ili kujenga jamii inayojali haki kwa kila mmoja na kuwafanya wananchi
waendelee kuwa na imani na Mahakama.
Alitanabaisha pia kuwa
kimsingi mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na uelewa wa mwongozo wa
utoaji adhabu ambao ni miongoni mwa nyenzo za maafisa wa Mahakama katika
mchakato wa utoaji wa adhabu kuwa halali na usiotiliwa shaka na wadaawa
wanaohusika katika mashauri mahakamani wakiwemo washtakiwa, waathiriwa,
wapelelezi, mawakili wa utetezi, waendesha mashtaka na umma kwa ujumla.
Mhe. Chuma alisema kuwa
ni matarajio ya Mahakama ya Tanzania kupitia mafunzo hayo washiriki watapata uelewa
wa mwongozo wa utoaji adhabu, hivyo kutumika ipasavyo katika mashauri hasa ya
rushwa, uzoefu utakaopatikana utafikishwa kwa maafisa wengine wa Mahakama ambao
hawakufanikiwa kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Mratibu wa Programu ya BSAAT ya Mahakama ya
Tanzania, Bw. Stephen Magoha akitoa maelezo
mafupi kuhusu mradi huo alisema kuwa, program hiyo inayofadhiliwa na Serikali
ya Uingereza kwa kushirikana na Umoja Ulaya (EU) na kuratibiwa na Ofisi ya
Rais, Ikulu ilianza kutekelezwa mwaka 2018/2019 ikijumuisha taasisi tisa
nufaika ambazo ni wadau katika mnyororo wa haki jinai ikiwemo Mahakama kama
mdau muhimu katika utiaji wa haki.
Bw. Magoha aliongeza kuwa
program hiyo imelenga kupunguza vitendo vya rushwa kama kikwazo cha kupunguza
kiwango cha umasikini kwa Watanzania, kuboresha uadilifu, kuboresha uwezo na
uratibu wa mfumo wa haki jinai katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na
kuongeza imani kwa umma juu ya utendaji kazi wa Mahakama.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo
Bw. Goodluck Chuwa alisema kuwa, ni takribana miaka mitano tangu chuo kimeamua
kujikita katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuundwa kwake kitahakikisha
kuwa kinaendelea kuyaratibu mafunzo mbalimbali kwa weledi mkubwa kwa lengo la
kuleta tija kwa Mahakama na wadau wengine wa sheria nchini.
Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021-2025, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja na Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wa miaka mitano wa mwaka 2018-2023.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Richard Kabate akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama.
Picha ya juu na chini ni picha ya washiriki wa Mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama wakiendelea na mijadala mbalimbali katika mafunzo hayo.






0 comments:
Post a Comment