Na: Rosena Suka IJA Lushoto
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zainabu Mango amewataka Mahakimu kushirikiana ili kuendeleza jukumu kuu la Mahakama la kutoa haki kwa wakati kwani umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.
Katika hotuba yake, Mhe. Dkt. Mango alitoa pongezi kwa uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuweza kuratibu mafunzo hayo chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Mhe. Dkt. Mango aliwasisitiza washiriki hao kuwa wananchi wengi ni wahanga wa makosa ya rushwa na utakatishaji fedha hivyo wanapoamua kesi hizo wanapaswa kutambua maendeleo na ustawi wa nchi yetu na maisha ya mmoja mmoja yako hatarini kutokana na vitendo hivyo.
Jaji Mango aliendelea kuwaomba washiriki hao kutumia uhuru
walionao kuamua mashauri ya aina hii bila kuonea mtu kwa hisia au pasipo na Ushahidi wa kutosha wa kumtia
hatiani
“Hii ni kanuni mojawapo ya utoaji haki na ni imani
yangu mtaendelea kuitumia ipasavyo” alisema Mhe. Dkt. Mango.
Aidha, aliwapongeza washiriki hao kwa utulivu wao wakati
wote wa mafunzo na kuwataka kwenda kuyafanyia kazi yale yote waliyofundishwa na
kuendelea kujifunza zaidi mambo mengine ambayo hayakufundishwa ili wawe na
uelewa wa kutosha na kuboresha utendaji
wenye ufanisi kwa maslahi mapana ya taifa letu na mahakama kwa ujumla.
Mhe. Dkt. Mango
aliendelea kwa kuwakumbusha washiriki hao kuwa ili kufikia
malengo ya Mpango Mkakati wa Mahakama na kuzitimiza nguzo zake zote tatu lazima
kuzingatia C tatu ambazo ni consultation,
coordination na cooperation.
“Hapa nisisitize nyote kuwa na ushirikiano kwa kuwa
umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Heshima na upendo pamoja na mapenzi mema
ya taifa letu yawe ni mambo ya msukumo yatakayotufanya tusimame kwa pamoja ili
Mahakama iweze kutekeleza vema jukumu lake la utoaji haki kwa wakati.
Mabadiliko na maboresho tunayoyataka hayawezi kufikiwa kwa kiwango
tunachokusudia kama hatutakuwa kitu kimoja” alikumbusha Mhe. Dkt. Mango.
Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki Hakimu Mkazi, Mhe. Respicius R. Katabi, ameupongeza uongozi
mzima wa Mahakama na Mradi wa BSAAT kwa kuandaa mafunzo hayo ambapo wameweza
kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo mashauri ya rushwa na kutakatisha fedha
hususani uchukuaji ushahidi kwa kutumia TEHAMA. Ameahidi elimu waliyoipata wataifikisha kwa
watumishi wengine wa kada yao ambao hawakuweza kuhudhuria mafunzo hayo.
Mafunzo haya yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na
kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto chini ya ufadhili wa Mradi
wa Kujengea Uwezo Endelevu Taasisi za Umma zinazohusika na Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Buildingi Sustainable Anti-Corruption Action in Tanzania) BSAAT.
Jumla ya Mahakimu Wakazi 200 kutoka katika Mikoa
mbalimbali ya Tanzania wanatarajiwa kupata mafunzo haya katika awamu tatu
ambapo awamu ya kwanza yenye Mahakimu 61 wamemaliza mafunzo tarehe 8 Februari,
2022. Awamu ya pili ya mafunzo haya itaanza tarehe 9 – 10 Feburari, 2022
na awamu ya tatu naya mwisho itakuwa tarehe 11-12 Februari, 2022.
0 comments:
Post a Comment