Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma amefungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za
Mwanzo leo tarehe 14/08/2023.
Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya
Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)
yanafanyika hapa Chuoni IJA na yatadumu kwa siku tano hadi tarehe 18/08/2023.
Katika hotuba yake ya Ufunguzi Mhe. Chuma ambae ndiye
alikuwa mgeni Rasmi amewataka Mahakimu
hao kwenda kusaidia kuondoa mrundikano wa mashauri katika Mahakama za mwanzo
kama ambavyo Sera ya Mahakama ya Tanzania inavyotaka.
“Mpaka sasa bado Mahakama za Mwanzo zinaendelea
kuongoza katika umalizaji wa Mashauri na kutokuwa na mrundikano wa mashauri,
kwa hiyo tunategemea ongezeko lenu litaendelea kupunguza mzigo wa kazi wa kila hakimu
na hatimaye kuendeleza sera ya Mahakama ya Tanzania kutaka kusiwe na mashauri
yanayozidi miezi sita,” amesema Mhe. Chuma.
Pia Mhe. Chuma amewataka mahakimu wakazi hao wapya
kujifunza matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano(TEHAMA) ili waweze
kutekeleza vema majukumu yao hasa wakati huu Mahakama ya Tanzania ikiwa
imejielekeza katika eneo hilo la Teknolojia.
“Karne hii ya 21 imetawaliwa na matumizi ya Teknolojia
katika kuwahudumia wananchi, jifunzeni matumizi ya mifumo ya TEHAMA inayoendeshwa na Mahakama ili msipate ugumu mnapotekeleza majukumu yenu,”
amesisitiza Mhe. Chuma.
Vile vile, Mhe. Chuma amewasisitiza washirika hao kuwa
wanapotekeleza majukumu yao, basi hawana budi kuzingatia misingi ya haki za
binadamu, maisha ya watu na ustawi wa Usalama wa nchi.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa
Mafunzo ya Kimahakama IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda
amezungumzia muhimu wa mafunzo hayo kwa kubainisha kwamba yanalenga kuwapatia
Mahakimu hao miongozo itakayowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Kimsingi umuhimu wa mafunzo haya ni kwa ajili ya kuwapatia
muongozo Mahakimu wapya ambao wanaenda kuanza majukumu yao katika Mahakama za mwanzo,
ukiwemo utoaji wa haki ambao ndio jukumu kubwa la Mahakimu hawa,” amesema Mhe.
Dkt. Kisinda.
Ameongeza kuwa Mahakimu watapewa miongozo, maelekezo
na miiko mbalimbali ambayo inahusiana na majukumu ya kule wanapokwenda
kusimamia utoaji wa haki.
Nao baadhi ya Washiriki wa Mafunzo hayo akiwemo Mhe. Aden
William Ruvurahende ambae ni Hakimu Mkazi mpya amebainisha faida ya mafunzo
hayo kwao wao washiriki.
“Kwa kweli suala hili la mafunzo kwetu sisi ni la muhimu
sana kwa sababu ni mwanzo wa kujua majukumu yetu, na fursa ya kufahamu miongozo
na kanuni ya kimahakama ili itusaidie kwa ajili ya utendaji haki pale
tunapokwenda kuwahudumia wananchi,” amesema Mhe. Ruvurahende.
Kuhusiana na
mlundikano wa mashauri amebaininisha: “Kuhusiana na mrundikano wa mashauri
Mahakamani, ni changamoto kwetu sisi ila tunakwenda kusaidia kutatua suala
hilo.”
Nae Mshiriki Mhe. Salma Athuman Mwamende anabainisha
kuwa Mahakama itarajie weledi, ufanisi, na uwajibikaji kutoka kwao.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akihutubia wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma(katikati) wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa
Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.
Wa pili kushoto ni
Mhe. Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika
Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda, wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa
Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Bi. Patricia Ngungulu, wa
kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka na wa kwanza kushoto ni Hakimu
Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Kavumo Mndeme.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma(katikati) akiwa katika picha na baadhi ya baadhi ya Washiriki wa Mafunzo
Elekezi ambao ni Wahe. Mahakimu Wakazi wapya wa mahakama za Mwanzo katika Chuo Cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).
Wa pili kushoto ni
Mhe. Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika
Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda, wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa
Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu, wa
kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka na wa kwanza kushoto ni Hakimu
Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Kavumo Mndeme.
Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo Elekezi ambao ni Wahe. Mahakimu Wakazi wapya wa mahakama za Mwanzo wakiwa katika mafunzo hayo katika
Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).
Jaji mstaafu ambae pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheira,
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma akihutubia wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa
Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.