Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Sunday, August 6, 2023

Naibu Waziri: IJA ni Chuo muhimu kwenye mambo ya haki






Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema kuwa Chuo cha Uongozi wa MahakamaLushoto(IJA) ni Chuo muhimu katika kuwajenga watu wanaosimamia masuala ya haki hapa nchini.
Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul amesema hayo leo Jumamosi tarehe 05/08/2023 wakati akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya IJA,  Halmashauri Tendaji ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti(RAAWU) tawi la Lushoto pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, hapa Chuoni wilayani Lushoto.
Amesema kuwa Chuo cha IJA kinapotoa maarifa kwa watu wa kada mbalimbali, basi kinasaidia katika masuala ya haki, akibainisha kuwa wananchi mbalimbali bado wanakabiliwa na ukosefu wa haki.
"IJA ni Chuo muhimu, nimefurahi kuona kumbe tuna Taasisi nzuri hapa," amesema Naibu Waziri na kuongeza,
"Sisi ambao tuna husika na wananchi moja kwa moja kama wabunge, madiwani na wenyeviti ni mashahidi kwamba wananchi wetu bado wana ukosefu wa haki zao hasa masuala ya kisheria, kwa hiyo nina imani ninyi mkiwapa maarifa watu wanaokuja kusoma hapa mnakuwa mnasaidia kwenye eneo la haki."
Pia Naibu Waziri huyo wa Katiba na Sheria ameongeza kuwa amejifunza masuala mengi ya Chuo cha IJA na 
kuhusu changamoto za Chuo Cha IJA, amebainisha kuwa atakwenda kuzifanyia kazi pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria na viongozi wengine.
"Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria alikuja hapa akapokea changamoto zenu, nami niwaambie tutakwenda kuzifanyia kazi na kazi yetu sisi ni kuwa kiungo ili kuona mnafanya kazi vizuri," amebainisha Mhe. Naibu Waziri.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha IJA ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F.Kihwelo amesema kuwa Chuo ni kitovu cha elimu na Utafiti kwa upande wa Mahakama na kwamba kimeendelea kuzalisha watu muhimu kwenye eneo la usimamizi wa haki.
Awali katika ziara hiyo, Mhe. Naibu Waziri huyo wa Katiba na Sheria alitembelea maeneo kadhaa ya Chuo, ikiwemo Maktaba, Hosteli ya Wanaume ya Benjamini Mkapa pamoja na viwanja vya michezo vya Chuo.
Katika hatua nyingine, Uongozi wa Chuo umempatia Mhe. Naibu Waziri zawadi za vitu mbalimbali yakiwemo machapisho ya Chuo.







 Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Pauline Gekul akisaini Kitabu cha wageni Ofisini kwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) alipofanya ziara Chuoni IJA.



Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul(katikati) akizungumza jambo wakati akiwa katika Maktaba  ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA)..

Kulia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo na kulia ni Mkutubi wa Chuo cha IJA, Bw, Jackson Chacha.



Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (kushoto) akiwa na   Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo(kulia) mara baada ya kukagua Hosteli ya wanaume ya Benjamin Mkapa alipofanya ziara hapa Chuoni IJA.



Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo(kulia) akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Pauline Gekul(hayupo pichani) aliyetembelea Chuo cha IJA hivi karibuni.


Wajumbe wa Halmashauri Tendaji ya Chama cha wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, habari na utafiti(RAAWU) Tawi la Lushoto wakimsikiliza Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul  alipofanya ziara Chuoni IJA.



Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo(kushoto) akimkabidhi machapisho ya Chuo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul alipofanya ziara hapa Chuoni IJA.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akizungumza na Wajumbe wa Menejimeti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) na Halmashauri Tendaji ya Chama cha wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, habari na utafiti(RAAWU) Tawi la Lushoto na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, alipofanya ziara hivi karibuni hapa Chuoni IJA.




0 comments:

Post a Comment