Na Rosena Suka –Lushoto
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA) kinaendesha mafunzo kwa Mahakimu Wakazi 200 ili kuwajengea uwezo katika
masuala mbalimbali ya haki jinai, hususani uendeshaji wa mashauri ya rushwa na
urejeshaji mali.
Akifingua mafunzo leo tarehe 7
Februari, 2022, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Edwin Kakolaki amesema anafahamu
kuwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Kitengo cha
mafunzo cha Mahakama ya Tanzania wameendelea kushirikiana katika eneo la
mafunzo.
“Ushirikiano huu ni sehemu tu ya
jitihada zinazoendelea katika utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya
mwaka 2019 ambayo inatambua Chuo hiki kama kitovu cha utoaji wa mafunzo kwa
watumishi wa Mahakama kwa lengo la kuongeza tija na kuboresha utendaji wa
Mahakama ya Tanzania,” amesema.
Kwa mujibu wa Jaji Kakolaki, mafunzo
hayo kwa Mahakimu hao ni muhimu sana kwao kwani yatawaongezea mbinu na uelewa
juu ya masuala mbalimbali ambayo yatawasaidia katika utendaji wa kazi, hivyo
amewaomba kushirikiana na wawezeshaji wote katika kupata yale yaliyokusudiwa.
Jaji Kakolaki amebainisha kuwa kesi
za rushwa na utakatishaji fedha zipo katika maeneo mengi ikiwemo uchumi na elimu,
hivyo Mahakimu Wakazi hawana budi kuwa na uelewa, maarifa na uwezo wa
kukabiliana nazo, hasa kwenye suala la kusikiliza na kufikia uamuzi.
“Miongoni mwa madhara yanayoweza
kusababishwa na rushwa pamoja na utakatishaji fedha ni kuzuia ukuaji wa uchumi
wa mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa zima kwa ujumla. Kwa kuzingatia uwepo wa
vitendo vya rushwa na utakatishaji fedha katika Idara na Taasisi mbalimbali za
Umma na binafsi, serikali imeweka mfumo wa kuzuia na kupambana na vitendo hivyo
ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinafikia malengo ya kuwahudumia Watanzania
kwa haki na usawa,” amesema.
Jaji Kakolaki anamshukuru Jaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kutoa kibali cha
kufanyika kwa mafunzo hayo yatakayowapatia Mahakimu waliotoka sehemu mbalimbali
hapa nchini elimu na ujuzi stahiki katika maeneo ya utekelezaji wa majukumu yao
pamoja na mahusiano sahihi kiutendaji kati yao na wadau wengine ndani na nje ya
Mahakama.
Aidha, ameishukuru serikali kupitia
Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Zinazohusika na Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (BSAAT) kwa kudhamini mafunzo hayo ya Mahakimu wakazi
200. Amesema kuwa programu hiyo imekuwa msaada mkubwa katika kuwajengea uwezo
Mahakimu kupitia mafunzo yahusuyo Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini
Tanzania.
Jaji Kakolaki pia ameushukuru Uongozi
wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) chini ya Mhe. Dkt. Paul Kiwhelo, ambaye
pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Kitengo cha Mafunzo cha Mahakama ya
Tanzania chini ya Bi. Patricia Ngungulu kwa kushirikiana kwa ukaribu kuratibu
uandaaji wa mafunzo hayo kwa ufanisi mkubwa.
Akitoa neno la utangulizi katika
mafunzo hayo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma
aliwakumbusha Mahakamu hao kuwa kazi ya kutoa haki ni kazi ya Mungu na kwa kuwa
yeye ni mtakatifu ni lazima kuifanya kwa uadilifu na utakatifu wake.
“Hoja hii ndiyo imelazimu uongozi wa
Mahakama kutoa kibali ili mafunzo haya yafanyike. Kwa msingi huo, kupambana na
rushwa, utakatishaji fedha na uhujumu uchumi kwa ujumla, si tu unataka weledi
wa hali ya juu, lakini pia unahitaji ujuzi na uelewa wa kutosha wa sheria na
kanuni zinazohusika na masuala haya,” amesema.
Kwa mujibu wa Mhe. Chuma, rushwa,
uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ni hatarishi kwenye jamii pamoja na
maendeleo ya taifa kwa ujumla, hivyo washiriki hawana budi kusikiliza kwa
makini na kushiriki kikamilifu wakati wote wa mafunzo ili kuungana na jitihada
zinazoendelea za Mahakama ya Tanzania za kujenga imani na kuwa karibu zaidi na
wananchi.
“Ni dhahiri kwamba kila mmoja wetu
akiwa na utamaduni wa uadilifu, uchumi wetu utakua, sekta ya umma itakuwa bora
na kustawi na taasisi zetu zitaaminika zaidi. Vilevile jamii zetu zitafaidi
matokeo ya ukuaji wa uchumi. Zaidi, ustawi wa watu wetu unategemea sana
uadilifu wetu na wa viongozi wenzetu. Kwa ufupi uadilifu utaboresha maisha ya
watu,” amesema.
Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa
Utawala na Rasilimaliwatu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha
aliwapitisha washiriki wa mafunzo hayo katika maelezo mafupi juu ya Programu ya BSAAT ambayo imejikita katika
kujenga mfumo endelevu wa mapambano dhidi ya rushwa unaofadhiliwa na Serikali
ya Uingereza kupitia Ofisi ya “Foreign Commonwealth Development (FCDO)” kwa
kushirikiana na Umoja wa Ulaya na hapa nchini kuratibiwa na Ofisi ya Rais,
IKULU.
“Programu hii ni ya miaka mitano na
imeanza kutekelezwa mwaka 2018/2019 – 2022/2023 kwa kunufaisha taasisi na
wizara mbalimbali, ambapo Mahakama ya Tanzania wakiwa ni moja wapo. Programu hii
inatekeleza malengo yake makuu, ikiwemo kupunguza vitendo vya rushwa kama kikwazo
cha kupunguza kiwango cha umasikini kwa Watanzania, kuboresha uadilifu, kuboresha
uwezo na uratibu wa mfumo wa haki ya jinai katika vita dhidi ya vitendo vya
rushwa na kuongeza imani kwa umma juu ya utendaji kazi wa Mahakama,” amesema.
Kwa mujibu wa Bw. Magoha, tangu
program hiyo ianze kutekelezwa, kumekuwa na viashiria mbalimbali vya mafanikio
ambavyo vimeonekana katika maeneo mbalimbali kama kuongezeka kwa utoaji wa
taarifa za ubadhirifu au vitendo vya rushwa kwenye mamlaka husika, kupunguza
muda wa usikilizwaji wa mashauri ya rushwa na urejeshaji wa mali.
Wakati wote wa mafunzo, washiriki
watapitishwa katika mada mbambali zilizoandaliwa na Wawezeshari mahiri katika
maeneo juu ya Rushwa, Utakatishaji Fedha na Urejeshaji Mali. Wawezeshaji hao ni
pamoja na Mhe. Kakolaki na Majaji wengine wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Dkt Zainab Mango na Mhe. Awamu Mbagwa pamoja na Naibu Msajili, Mhe.
Godfrey Isaya, ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mafunzo haya yameandaliwa na
Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
chini ya ufadhili wa Mradi wa Kujengea Uwezo Endelevu Taasisi za Umma
zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Buildingi Sustainable
Anti-Corruption Action in Tanzania) BSAAT. Jumla ya Mahakimu Wakazi 200 kutoka
katika Mikoa mbalimbali ya Tanzania wanategemewa kupewa mafunzo haya katika
awamu tatu ambapo awamu ya kwanza yenye Mahakimu 61 wameanza mafunzo tarehe 7 –
8 Februari, 2022. Awamu ya pili ya
mafunzo haya itaanza tarehe 9 – 10 Feburari, 2022 na awamu ya tatu naya mwisho
itakuwa tarehe 11-12 Februari, 2022.
Mhe. Edwin Kakolaki, Jaji wa
Mahakama Kuu Ya Tanzania akifungua Mafunzo kwa Mahakimu Wakazi kuhusu
Uendeshaji Wa Mashauri Ya Rushwa, Utakatishaji Fedha Na Urejeshaji Mali zilizopatikana
kwa Fedha Haramu yanayofanyika Chuo Cha Uongozi Wa Mahakama Lushoto (IJA) Kuanzia
Tarehe 7- 12 Februari, 2022.
Mhe. Victor Bigambo Hakimu Mkazi na Mratibu wa
Mafunzo ya kuhusu Uendeshaji Wa Mashauri Ya Rushwa, Utakatishaji Fedha Na
Urejeshaji Mali zilizopatikana kwa Fedha Haramu akiwatambulisha washiriki kwenye mafunzo yanayofanyika
Chuo Cha Uongozi Wa Mahakama Lushoto (IJA) Kuanzia Tarehe 7- 12 Februari, 2022.
Picha za washiriki
wa mafunzo ya namna bora ya Uendeshaji Wa Mashauri Ya Rushwa, Utakatishaji
Fedha Na Urejeshaji Mali zilizopatikana kwa Fedha Haramu wakifuatialia hotuba
ya mgeni rasmi alipokuwa anafungua mafunzo hayo yanayofanyika Chuo Cha Uongozi
Wa Mahakama Lushoto (IJA) Kuanzia Tarehe 7- 12 Februari, 2022.
Picha za washiriki wa mafunzo ya namna bora ya Uendeshaji Wa Mashauri Ya Rushwa, Utakatishaji Fedha Na Urejeshaji Mali zilizopatikana kwa Fedha Haramu wakifuatialia hotuba ya mgeni rasmi alipokuwa anafungua mafunzo hayo yanayofanyika Chuo Cha Uongozi Wa Mahakama Lushoto (IJA) Kuanzia Tarehe 7- 12 Februari, 2022.
Baadhin ya picha za washiriki wa mafunzo ya namna bora ya Uendeshaji Wa Mashauri Ya Rushwa, Utakatishaji Fedha Na Urejeshaji Mali zilizopatikana kwa Fedha Haramu wakifuatialia hotuba ya mgeni rasmi alipokuwa anafungua mafunzo hayo yanayofanyika Chuo Cha Uongozi Wa Mahakama Lushoto (IJA) Kuanzia Tarehe 7- 12 Februari, 2022.
0 comments:
Post a Comment