Na: Rosena Suka, Lushoto
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kimeandaa na kuendesha mafunzo kuwajengea uwezo Mahakimu 36 namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia na jinsi ya kuwahudumia wahanga na mashahidi.
Mafunzo hayo
ambayo yameandaliwa na chuo hicho kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake
katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF) kupitia ufadhili wa USAID
kutoka kwa watu wa Marekani yamefunguliwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor, tarehe 22 Februari, 2022 na yanahusisha Mahakimu Mahakimu wa ngazi
mbalimbali kutoka Mikoa ya Mbeya, Njombe na Kilimanjaro.
Akizungumza na
washiriki wakati wa ufunguzi, Mhe. Mansoor amewafahamisha lengo
la mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi wa kutekeleza majukumu ya namna bora
ya kuendesha kesi za ukatili wa kijinsia na jinsi ya kuwahudumia manusuru wa
ukatili huo na kuhakikisha wanapata haki na watuhumiwa
kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Mhe. Mansoor amefafanua kuwa ukatili wa kijinsia ni tatizo kubwa ambalo linaikabili Dunia
kwa kuonesha tatifiti mbalimbali zinazotolewa na mashirika mengi yaliyofanya
tafiti hizo. Tafiti iliyofanywa na Shirika la Afya Duniani mwaka 2013
zimeonyesha asilimia 35 ya wanawake Duniani wamefanyiwa ukatili wa kupigwa au
kubakwa.
Amenainisha kuwa
katika tafiti iliyofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto
(UNICEF) ya mwaka 2017 imeonesha wasichana wapatao 750 milioni duniani
wanaolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18. Kwenye taarifa hiyo
imekadiria kuwa wasichana milioni 120, yaani msichana moja katika ya kumi
Duniani, wamekumbana na vitendo vya kulazimishwa kufanya ngono bila ridhaa yao.
Aidha, Mhe.
Mansoor alieleza kuwa rushwa ya ngono ni tatizo lililopo katika maeneo ya kazi
na vyuo vikuu nchini kutokana na utafiki uliofanywa na TAKUKURU katika vyuo
viwili nchini mwaka 2020 na asilimia 50 ya waliohojiwa walikiri
rushwa hii kuwepo katika vyuo vikuu.
Mhe. Mansoor
amezitaja hatua mbalimbali za Serikali katika kukabiliana na ukatili wa
kijinsia hapa nchini, ikiwemo kuanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika
vituo vya Polisi, kwa lengo la kuhakikisha wanawake na umma kwa ujumla wanakuwa
na mazingira mazuri bila vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Pia kuweka
wataalamu mbalimbali kwenye vituo vya Mkono kwa Mkono vya kutoa huduma kwa
wahanga wa ukatili wa kijinsia ambao ni wataalamu wa ustawi wa jamii,
wanasheria, madaktari na polisi.
Kumekuwepo na
huduma za simu bila malipo kwa watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na
unyanyasaji (Child Helpline), kamati za ulinzi wa wanawake na watoto katika
ngazi zote kuanzia kitaifa mpaka chini na hatua nyingine nyingi.
Mhe. Mansoor
amewasisitiza Mahakimu hao kuwa pamoja na juhudi mbalimbali za Serikali za
kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia haziwezi kuzaa matunda iwapo
hazitaungwa mkono na wadau muhimu kama Mahakama hususani Mahakimu.
“Katika
kupambana na tatizo la ukatili wa kijinsia, inabidi Mahakama ijikite katika
kubuni mikakati ya kisheria ambayo ndiyo italeta suluhisho la kudumu katika
kusikiliza kesi za ukatili na kuzitolea maamuzi,” alisema.
Mhe. Mansoor
ameainisha kuwa katika utekelezaji wa sera na sheria kwenye Sheria ya Kanuni ya
Adhabu inayoainisha makosa ya ukatili wa kijinsia kipengele cha (SOSPA) ni
mojawapo ya eneo linaohitaji kusimamiwa kikamilifu na Mahakama ili kulinda
ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
“Ni dhahiri kuwa
kwa kuwekeza katika sekta ya Mahakama itasaidia kupunguza na kuondoa kabisa
vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vina kwambisha juhusi za maendeleo ya
nchi” alisema Mhe. Mansoor.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika, Dkt. Monica Mhoja amesema
kuwa shirika hilo linatumia sheria kama nyenzo ya kuleta
mabadiliko.
Amesema Shirika
hilo limekuwa likifanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini ambao
ni Wizara ya Katiba na Sheria, Mahakama, Polisi, Kamati za MTAKUWWA, Ofisi ya
Bunge, Taasisi za elimu ya juu na kati, Shule za Msingi na
Sekondari, Viongozi wa Dini, Wana Habari, Makundi Maalumu kama watu
wenye ulemavu na mashirika mengine.
Dkt. Mhoja aliendelea kusema
kuwa mchango wa WiLDAF katika mabadiliko ya sheria kandamizi na mila na desturi
kandamizi ( sheria ya umiliki wa ardhi, sheria ya mirathi, sheria ya ndoa) ni
kutoa msaada wa kisheria na nafasi yao kama afisa wa Mahakama katika
kuwahudumia manusura wa ukatili wa kijinsia.
Amesema pia kuwa hutoa
mafunzo na kusimamia wasaidizi wa kisheria. Kwa kupitia mradi wa
Mwanamke Imara WiLDAF imepata fursa ya kuaandaa mafunzo kwa Mahakimu katika
mikoa ya Njombe, Mbeya na Kilimanjaro ili kuimarisha uwezo wao katika kuhudumia
manusura wa ukatili wa kijinsia.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika, Dkt. Monica Mhoja akiongea na Mahakimu wa ngazi mbalimbali kutoka Mikoa ya Mbeya, Njombe na Kilimanjaro wanaohudhuria mafunzo ya kujengewa uwezo wa namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia na jinsi ya kuwahudumia wahanga na mashahidi yanayofanyika Chuoni Lushoto
Hakimu Mkazi Mfawidhi (W) Lushoto, Mhe. Rose Ngoka akitoa neno la ukaribisho kwa Mahakimu wa ngazi mbalimbali kutoka Mikoa ya Mbeya, Njombe na Kilimanjaro wanaohudhuria mafunzo ya kujengewa uwezo wa namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia na jinsi ya kuwahudumia wahanga na mashahidi yanayofanyika Chuoni Lushoto
Mahakimu wa ngazi mbalimbali na washiriki wa mafunzo ya kujengewa uwezo wa namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia na jinsi ya kuwahudumia wahanga na mashahidi yanayofanyika Chuoni Lushoto wakiwa wanafuatilia mada zinazotolewa kwenye mafunzo.
0 comments:
Post a Comment