Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Saturday, February 12, 2022

MAHAKIMU WAKAZI WATAKIWA KUWAJIBIKA KWA UMMA KWA MUJIBU WA KIAPO: MHE. MSAJILI GODFREY ISAYA

 Na. Rosena S. Suka IJA

Naibu Msajili na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Mhe. Godfrey Isaya, amewataka Mahakimu Wakazi   kuwajibika kwa umma kwa mujibu wa kiapo walichoapa cha uhakimu ambacho ni kutenda haki kwa wote bila kujali ni nani aliye mbele yake.

Hayo yalisemwa na  Mhe. Godfrey Isaya  leo tarehe 12 Februari, 2022 alipokuwa akifunga mafunzo kwa kundi la tatu na Mahakimu Wakazi sitini na moja kati ya Mahakimu Wakazi 200 ambao wamehudhuria  mafunzo ya kuwajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya haki jinai, hususani uendeshaji wa mashauri ya rushwa na urejeshaji mali yanayoendeshwa na  Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. (IJA) 

Aliongeza kuwa hivi sasa Tanzania iko katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda,  hivyo amewasisitiza washiriki hao kuwa waadilifu na wenye uelewa wa kutosha wa sheria, miongozo, kanuni na taratibu mbalimbali zitakazowaongoza katika utendaji wao wa kazi za kila siku.  

“Ni wajibu wetu kufanya kazi ya uhakimu kwa uweledi, umakini, uadilifu na kwa kuzingatia ushahidi, miongozo mbalimbali. Nje ya hapo ni kukiuka kiapo cha uhakimu. Ninatambua wazi mnafahamu jambo hili lakini niwaombe mwendelee kusimama kwenye mstari sahihi”. Alisema Mhe. Godfrey.

Mhe. Godfrey aliwakumbusha Mahakimu hao kuwa mafunzo waliyopata yana maana kubwa kwao sio tu  kuwapa nyenzo za namna ya kukabiliana na mashauri ya aina hiyo bali pia watakapoendesha mashauri hayo inavyostahiki watakuwa wametimiza nguzo ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ya kuongeza imani ya wananchi kwa mahakama ambapo itaweza kudumisha amani, utulivu na udugu na kuifanya serikali  kutekeleza majukumu yake ya kuleta maendeleo kwa wananchi.

Naye Mratibu wa Mafunzo na Hakimu Mkazi Mwandamizi  kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto , Mhe. Victor Bigambo amewataka mahakimu hao kuwa walimu kwa wenzao ambao wamebaki vituoni kutokana na ufinyu wa bajeti ambapo umefanya mahakimu hao wachache kuhudhuria kwenye mafunzo hayo, huku akisisitiza kuzingatia masuala ya TEHAMA  ili a kumaliza mashauri yote kwa haraka na kwa ubora kama ambavyo wanapaswa kufanya.

Akizungumza wakati wa kutoa neno la shukurani, Hakimu Mkazi, Bittony I Mwakisu kwa niaba ya washiriki wenzake alisema wanaishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na BSAAT  kuratibu Mafunzo hayo, ambayo yatawasaidia  katika utatuzi wa kesi zinazohusu namna bora ya kuendesha mashauri ya rushwa, utakatishaji fedha na urejeshaji wa mali iliyopatikana na fedha haramu.

Mafunzo haya yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto chini ya ufadhili wa Mradi wa Kujengea Uwezo Endelevu Taasisi za Umma zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Buildingi Sustainable Anti-Corruption Action in Tanzania) BSAAT.

Mafunzo hayo yamehuhusisha  jumla ya Mahakimu wakazi 200 kutoka katika mahakama mbalimbali za Tanzania Bara kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza yenye Mahakimu 61 walimaliza mafunzo tarehe 8 Februari, 2022.  Awamu ya pili ya mafunzo haya yenye jumla ya Mahakakumu Wakazi 69 ilimalizika tarehe 10 Feburari, 2022 na awamu ya tatu naya mwisho iliyojumuisha jumla ya Mahakimu Wakazi 61 imemalizika leo tarehe 12 Februari, 2022.



Naibu Msajili na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Mhe. Godfrey Isaya akiwa akitoa hotuba yake kwa kundi la tatu la Mahakimu Wakazi kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania wakati wa kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya haki jinai, hususani uendeshaji wa mashauri ya rushwa na urejeshaji mali yanayoendeshwa na  Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. (IJA) 

Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mratibu wa Mafunzo Mhe. Victor Bigambo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. (IJA)  akiongea na washiriki wa mafunzo wakati wa kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya haki jinai, hususani uendeshaji wa mashauri ya rushwa na urejeshaji mali  



Hakimu Mkazi  na mwakilishi wa washiri wa Mafunzo Mhe. Bittony I Mwakisu akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wa  mafunzo ya kuwajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya haki jinai, hususani uendeshaji wa mashauri ya rushwa na urejeshaji mali wakati wa kufunga mafunzo hayo





Baadhi ya  washiriki wa  mafunzo ya kuwajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya haki jinai, hususani uendeshaji wa mashauri ya rushwa na urejeshaji mali wakipokea vyeti vya ushiriki wa mafunzo wakati wa kufunga mafunzo hayo

(Picha na Ibrahim Mdachi)

0 comments:

Post a Comment