Na Mary Gwera, Mahakama-Lushoto
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Waajiriwa wapya wa Mahakama
nchini kubadili fikra hasi kwa kuwa na fikra chanya ili kuondokana na utoaji wa
huduma kwa mazoea na badala yake watoe huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.
Akizungumza na Watumishi
hao leo tarehe mosi Agosti, 2022 mjini Lushoto wakati akifungua mafunzo elekezi
ya awali kwa waajiriwa hao, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, Mahakama
inatekeleza programu za maboresho yanayomlenga mwananchi. Kwa hivyo, kipaumbele
ni kuhakikisha Mahakama inatoa huduma bora zitakazofanya wananchi kuwa na imani
na chombo hicho cha haki pamoja na kuwaweka wananchi kuwa karibu na Mahakama.
“Kwa dhamira hii,
Mahakama inatutaka sote kwa pamoja kubadilika fikra zetu ili kuondokana na
kutoa huduma kwa mazoea na badala yake kupitia mafunzo haya mnaelekezwa kuwa
kila mmoja wenu katika nafasi yake ahakikishe anadhamiria kuunga mkono juhudi
hizi za Mahakama kwa kwenda kutoa huduma bora kwa namna ambayo itawafanya
wananchi na jamii kwa ukumla kuwa na imani nanyi na imani kwa Mahakama,”
amesema Mtendaji Mkuu.
Prof. Ole Gabriel,
amewaeleza pia Watumishi hao kuwa tayari kufanya kazi kwenye maeneo
watakayopangiwa bila manung’uniko kwa kuwa ndiko wananchi wanataka kupatiwa
huduma.
“Ni matarajio yangu kuwa
mtakubaliana na vituo mtakavyopangiwa kwa kuwa huko ndiko kunakohitaji huduma
zenu na ndio maana Serikali ilitoa kibali muajiriwe. Niwadokeze tu hapa kuwa,
hakuna sehemu nzuri wala mbaya ndani ya Mahakama na badala yake kila Mahakama
ipo kwenye maeneo ambayo wananchi wanaishi,” amesisitiza Prof. Ole Gabriel.
Amebainisha kuwa, Mafunzo
hayo yanalenga kuwajengea uwezo katika maeneo ambayo ni ya msingi katika
kuwaandaa kuwa watumishi wema wenye haiba, tabia, mienendo na maadili ya
kimahakama.
Akizungumzia suala la
matumizi ya TEHAMA mahakamani, Mtendaji Mkuu amewaeleza Watumishi wao kulipa
kipaumbele suala la matumizi ya teknolojia kwakuwa ndio Mahakama inapojielekeza
kwa sasa.
“Mtakapokuwa mnajifunza
hapa, mtaelezwa kuhusu mifumo mbalimbali ya KITEHAMA ambayo itatumika katika
kuboresha utoaji haki na huduma mbalimbali katika Mahakama. Lengo la kuelekezwa
hayo ni kuwataka mfahamu kuwa matumizi ya TEHAMA si hiari bali ni jambo la
lazima kwa kuwa mtakutana na mifumo ya kiteknolojia na matumizi yake katika
kutoa huduma za kimahakama na kugundua kuwa imeshika kasi katika kila kona ya
Mahakama,” amesisitiza Mtendaji Mkuu.
Naye Mkurugenzi Msaidizi
wa Mafunzo, Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu amesema kwamba, lengo
kuu la mafunzo hayo ni kubadilisha mitazamo ya Watumishi wapya ili iendane na
mitazamo ya Mahakama hatimaye kuwawezesha kufanya kazi inavyotakiwa.
“Kama tunavyofahamu
Watumishi hawa wametoka mazingira tofauti tofauti, wamelelewa katika mazingira
mbalimbali pamoja na mitazamo tofauti, kwahiyo lengo kubwa la mafunzo haya ni
kuwaandaa ili waweze kuendana na kile ambacho Mahakama inatarajia,” amesema Bi.
Patricia.
Mafunzo hayo ya siku tano
(5) yamehusisha Watumishi wa Kada za Afisa Utumishi/Tawala, Wahasibu, Wakaguzi
wa Ndani, Maafisa TEHAMA, Maafisa Ugavi pamoja na Madereva.
Mafunzo hayo ambayo
imeelezwa kuwa yatakuwa endelevu kwa Waajiriwa wapya wa Mahakama, ni mwendelezo
wa Mafunzo yaliyotolewa kwa kundi la Mahakimu na Wasaidizi wa Kumbukumbu
yaliyomalizika tarehe 29 Julai, 2022. Aidha, yanafanyika kwa mara ya kwanza,
kwa kuwa kabla ya hapo hakukuwa na mafunzo ya namna hii kwa watumishi hao.
Mada zinazotarajiwa
kutolewa katika Mafunzo hayo ni pamoja na Muundo na tamaduni za kimahakama,
Mpango Mkakati wa Mahakam ana Mpango wa Uboreshaji Huduma za Mahakama, Huduma
kwa wateja, Maadili ya Utumishi wa Umma na wa Mahakama, Ubunifu katika kazi na
nyingine.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante
Ole Gabriel akisisitiza jambo alipokuwa akifungua rasmi Mafunzo elekezi kwa
Waajiriwa wapya wa Mahakama ya Tanzania yanayofanyika leo tarehe Mosi Agosti,
2022 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Washiriki wa wakifuatilia zoezi la Ufunguzi wa Mafunzo
wa elekezi.
4.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Elia Baha
akitoa neno la utangulizi katika zoezi la ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa
waajiriwa wapya wa Mahakama. Aliyeketi wa pili kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo,
Bw. Halid Magenda, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi Morogoro, wa kwanza kulia ni Mhe. Rose Ngoka, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya
ya Lushoto na wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo Mahakama ya
Tanzania, Bi Patricia Ngunguru
5.
Hakimu Mfawidhi wa Wilaya Lushoto, Mhe.
Rose Ngoka akitoa neno la ukaribisho katika zoezi la ufunguzi wa Mafunzo
Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Mahakama.
5.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Elia Baha
akitoa neno la utangulizi katika zoezi la ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa
wapya wa Mahakama.










0 comments:
Post a Comment