Na: Yusuph Sungura IJA Lushoto
Wananchi mbalimbali wamekipongeza Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) kwa utoaji wa elimu bora ya sheria hapa nchini. Wananchi hao wametoa pongezi hizo walipotembelea banda la IJA katika maonesho ya pili ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi(NACTVET) ya mwaka 2023, yanayoendelea katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Erick Samwel ambae ni mkazi wa Arusha amesema kuwa IJA inatoa
elimu bora ya sheria nchini na kwamba kinastahili pongezi kwa kazi hiyo.
"Kuna ndugu yangu alisoma hapo IJA miaka ya nyuma,
anasema kuwa chuo hicho kinafundisha sana na kumfanya mwanafunzi awe vizuri sana
kwenye sheria," amesema Samwel.
Nae mzazi Martha Shirima aliyefika kwenye banda la chuo cha
IJA na binti yake, amesema kuwa wamefika ili kuulizia utaratibu wa kujiunga na
chuo hicho kwa kuwa anasikia walimu wanafundisha sana kiasi ambacho mwanafunzi
anakuwa mahiri sana.
"Nimekuwa nikisikia kutoka kwa baadhi ya watu wakikisifu
sana hiki chuo kwa elimu ya sheria nchini, ndio maana nimekuja hapa na binti
yangu ili tupate maelezo zaidi. Hongereni kwa hilo," amesema Martha.
Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi wa IJA Tundonde Mwihomeke
amebainisha kuwa IJA ni bora katika utoaji wa elimu ya sheria nchini kwa kuwa
walimu wake wamekuwa wakihakikisha mwanafunzi anaelewa zaidi.
"Walimu wa IJa tunahakikisha wanafunzi anaelewa, watu
wanasema hatuna blah blah, ni kweli, lengo letu ni kuhakikisha mwanafunzi
anapata elimu bora iendane na dunia inavyokwenda," amesimulia mhadhiri
huyo msaidizi Tundonde.
Pia ameongeza kuwa kila mwanachuo hupangiwa mhadhiri
anaewajibika kumuongoza na kumshauri katika masuala ya taalumu yake.
Nae Afisa Udahili wa chuo cha IJA, Magdalena Mlumbe amesema
kuwa chuo kina miundombinu muhimu na ya kisasa ikiwemo maktaba ambayo ina
vitabu muhimu katika maarifa ya sheria.
"Chuo chetu kina miundombinu ya kisasa ambayo ni muhimu
katika ufundishaji, mathalani kuna maktaba ya kisasa yenye vitabu vya ambavyo
si rahisi kuvipata kwenye maktaba zingine," amesema Magdalena.
Vile vile, Magdalena ameongeza kuwa chuo kina miundombinu
yote muhimu ikiwemo huduma ya malazi, zanahati na
viwanja vya michezo.
Pichani Bi Magdalena Mlumbe Afisa Udahili wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akitoa maelezo ya shughuli za Chuo kwa wananchi waliojitokeza katika banda la Chuo wakati wa Maonesho ya Pili ya ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi(NACTVET) ya mwaka 2023.
Pichani Bi Tundonde Mwihomeke Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akitoa maelezo ya shughuli za Chuo kwa wanafunzi waliojitokeza katika banda la Chuo wakati wa Maonesho ya Pili ya ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi(NACTVET) ya mwaka 2023.
Pichani wanafunzi waliotembelea banda la Chuo wakipata maelezo kuhusu shughuli za Chuo wakati wa Maonesho ya Pili ya ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi(NACTVET) ya mwaka 2023.
0 comments:
Post a Comment