Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Tuesday, May 2, 2023

IJA YAADHIMISHA MEIMOSI KWA KUMUAGA MTUMISHI ANAYESTAAFU

Na; Yusuphu Sungura IJA

Chuo cha Uongozi wa Mahakama  Lushoto(IJA) leo Mei, 1 2023 kimeungana na wafanyakazi duniani kote katika kuadhimisha siku ya wafanyakazi. Sherehe hizi zilizoandaliwa na Uongozi wa Chuo zilifanyika katika ukumbi wa Ibrahim Hamis Juma uliopo chuoni Lushoto.

 Watumishi wa IJA pamoja na watumishi kutoka Mahakama ya Wilaya ya Lushoto  waliungana pamoja katika kuadhimisha sherehe hii iliyoambatana na matukio mbalimbali ambayo ni kumwaga rasmi mtumishi wa muda mrefu Dokta Joseph Ismail Hokororo ambae amestaafu kwa hiara.  Pamoja na shughuli hiyo pia sherehe hii ilijumuisha kuwakaribisha watumishi wageni waliohamia na watumishi wapya katika utumishi wa umma.

 Akitoa neno katika sherehe hizo kwa niaba ya mkuu wa chuo,  makamu mkuu wa Chuo, taaluma, utafiti na ushauri, Bwana Goodluck Chuwa amewanasihi wafanyakazi wote kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na umoja. Aidha amewataka watumishi wapya waliyojiunga na IJA kufuata miongozo na kanuni za utumishi wa umma, pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kuleta tija kwa maendeleo ya chuo.

 Akielezea Kuhusu mtumishi anaegwa, Bwn. Chuwa amemsifu kuwa alikuwa mtumishi mwema, mvumilivu na aliyeipenda kazi yake kwa dhati. Vile vile, amesema kuwa Dokta Hokororo ni mtumishi aliyesaidia kuikuza lugha ya kiswahili IJA kwa kushajiisha  maneno kama udahili, mchakato na mdau.

Nae mtumishi aliyeagwa, Dkt. Hokororo amewashukuru watumishi wote wa IJA kwa ushirikiano wao mkubwa waliyompa katika kipindi chake chote cha utumishi chuoni hapa cha takribani miaka 20. Pia amemshukuru Mkuu wa Chuo, Mhe. Dkt.  Paul F. Kihwelo ambae ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, kwa ushauri na ushirikiano aliyempatia kwa kipindi chake chote cha kufanya kazi IJA.

 "Binafsi amekuwa msaada mkubwa kwangu hasa nilipopata changamoto za kibinafsi, nimekuwa nikienda ofisini kwake kumshirikisha jambo lililonitatiza, nae bila kusita alinipa msaada mkubwa na wakati wote alinisisitiza kumtegemea Mungu kwa kila jambo," amesimulia Dkt. Hokororo.

 Shughuli hiyo imeambatana pia na tukio la kumtangaza na kumpa zawadi mfanyakazi bora wa IJA mwaka 2022/2023, ambae ni bwana Wilson Msoffe wa idara ya uhasibu.  Bwana Msoffe ametunukiwa fedha tasilimu shilingi milioni moja, Cheti na picha yake kubwa itakaa kwenye mbao ya matangazo kwa muda wa mwaka mmoja ili kutambulika kama mfanyakazi bora wa mwaka 2023. Sambamba na hilo,  chuo kimewapa zawadi wafanyakazi hodari wanne (4)  ambao ni George Masanja(Afisa Milki), Mustafa Maghembe(Dereva), Dorothea Kavuye(Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maktaba) na Cheusi Waziri(Katibu Mukhtasi). Kila mmoja amezawadiwa fedha taslimu  shilingi laki tatu.

Picha mbalimbali za Sherehe za Mei Mosi



















0 comments:

Post a Comment