Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekipongeza Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kutoa wahitimu waliopikwa katika tanuri la vielelezo vya ubora na ufanisi wa huduma kwakuwa na uwezo wa kukabiliana na kumudu mabadiliko yoyote katika soko la ajira. Rai hiyo aliitoa leo tarehe 24 Novemba, 2023 wakati wa mahafali ya 23 kwa wahitimu 831 wa ngazi mbalimbali wa Chuo Cha Uongozi wa Mahakama yaliyofanyika Chuoni Lushoto.
Alisema kuwa kufanyika kwa mahafali ya Chuo ni uthibitisho
wa mafanikio makubwa kwa Wanafunzi waliohitimu kupitia juhudi kubwa za Uongozi
wa Chuo na wanataaluma. Aliendelea kwa kusema mahafali ni wakati mzuri wa
kujitathmini na kutambua kuwa Chuo chetu kimepiga hatua kubwa katika kutoa elimu bora, Mafunzo
Endelevu ya kimahakama, kufanya tafiti na ushauri elekezi kwa kushirikiana na wadau
mbali mbali wa sheria wa ndani na nje ya
nchi. Mahakama ya Tanzania imekuwa ikivunia kuwa na Chuo chenye kutekeleza
malengo yaliyokusudiwa.
Aidha,
Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha wahitimu kuwa ni muhimu kufahamu vyema
mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yanayogusa Tanzania na Dunia kwenye
matumizi ya Tecknolojia ya Habari na Mawasiliano yanayosukumwa na Akili Bandia
ambayo yamefanya mabadiliko katika utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia za
kisasa.
“Tahadhari muhimu hapa, kila mmoja wenu
anatakiwa kubadilika na kujiongezea ujuzi na umahiri katika matumizi ya
teknolojia katika kutoa huduma. Uwezo uliotokana na Astashahada ya Sheria
(Certificate), na Stashahada ya Sheria (Diploma in Law) peke yake
hautakuwezesha kupata ajira za kiushindani katika Tanzania na Dunia ya Dijitali”
alisema Mhe. Prof. Juma.
Pamoja na hayo Mhe. Prof. Juma amefarijika kwa
kuona Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto umefikia hatua nzuri ya
kukamilisha ujenzi wa jukwaa la ufundishaji wa elimu kwa njia ya
ki-elekitroniki (E-LEARNING PLATFORM). Akaendelea
kwa kutaja faida kadhaa zitakazotokana na ufundishaji wa njia hiyo ya ki-elekitroniki
ni pamoja na kuwafanya wanafunzi kuhudhuria masomo yao huko huko waliko huku wakiendelea na kazi zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi
wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dkt. Gerald Ndika alisema Chuo kimepata mafanikio
makubwa kwenye kutoa Mafunzo, warsha na
makongamano mbalimbali. Pamoja na mafunzo na makongamano yanayofanywa Chuo pia
kinafanya tafiti mbalimbali kukidhi mahitaji ya kuwajengea uwezo wataalamu wetu. Tafiti hizo
zimepelekea Chuo kuandaa machapisho mbalimbali kama vile kitabu cha mkusanyiko wa
maamuzi ya Mahakama kuhusu unyanyasaji na ukatili wa kingono kwa watoto. Hii inadhihirisha waziwazi Chuo
kinavyoshirikiana na jamii dhidi ya kupinga unyanyasi na kulinda na kutetea
haki ya mtoto.
Mhe. Dkt Ndika aliendelea kwa kumhakikishia Jaji Mkuu wa Tanzania kuwa Chuo kiko kwenye maandalizi ya kufatilia huduma zinaofanywa na wahitimu wake katika maeneo mbalimbali kwa kufanya tathimini mahususi. Hii imetokana na wahitimu wa Chuo kuhitajika katika maeneo mbalimbali.
Naye Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo, Mhe. Dkt. Paul F.
Kihwelo katika maelezo yake alimshukuru Mhe Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 20 Septemba 2023 kuridhia
mapendekezo ya Kamati ya Raisi ya Utekelezaji (PIC) na kuidhinisha Muundo wa
Mgawanyo wa Majukumu ya Chuo ili kuimarisha utendaji kazi. Katika muundo huo umeanzisha Kurugenzi ya
Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu ambayo jukumu lake kubwa litakuwa ni kuratibu mafunzo ya Kimahakama kwa maafisa wa
Mahakama na watumishi wengine wa Mahakama na wadau mbalimbali wa sekta ya
sheria nchini.
0 comments:
Post a Comment