Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Wednesday, December 1, 2021

WATUMISHI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUTOA ELIMU YA MAHAKAMA KWA WANANCHI – JAJI CHANDE

Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman amewataka Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama Tanzania kutoa elimu kwa wananchi juu ya utendaji kazi wa mahakama na kuacha kuwa na hisia hasi kwani Mahakama ndicho chombo cha mwisho katika utoaji haki.

Akitoa mada kwa viongozi hao wakati wa mafunzo elekezi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Novemba 30, 2021, Mhe. Othman aliwapongeza kwa kuteuliwa na kuwakumbusha kuwa mwananchi wa kawaida anatamanani kuona shauri lake linamalizika mapema ili ajue hatma yake.

Mhe. Othman aliendelea kwa kuwaasa Naibu Wasajili na Watendaji hao  kuzingatia maadili na kuiishi miiko ya Mahakama na kutokuwa na makundi maofisini kwani wao wanaenda kutatua migogoro na sio kutengeneza.

Aidha, Mhe. Othmani aliwasisitiza viongozi hao kuwa na maono mazuri juu ya maendeleo ya Mahakama ili kurudisha imani kwa jamii juu ya utendaji wa shughuli za Mahakama ya Tanzania na kuleta mabadiliko ya kweli. Mhe. Othman alitumia wasaa huo kusisitiza uwajibikaji, kujenga utamaduni wa kufikika na kutoa maamuzi kwa wakati na kwa weledi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

 “ Kila mmoja wenu ni Kiongozi atumie maarifa yake kuisaidia Taasisi na kumsaidia Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi”.

Mhe. Othman aliendelea kwa kusema kuwa uboreshaji mkubwa na ufanisi umetokana na kuanzishwa Tume huru ya Utumishi wa Mahakama na pia kutenganisha kada mbili za taaluma ya watendaji na wasajili, kwa maana ya Watendaji kushughulika na masuala ya utawala na fedha na Wasajili kushughulikia masuala ya utaratibu wa mashauri mahakamani.

Jaji Mkuu huyo mstaafu aliwaelezea washiriki hao kuwa matokeo chanya ya uboreshaji wa huduma za mahakama yameonekana katika utendaji kazi ambapo hivi sasa kuna mahakama  inayotembea, mfumo wa kieletroniki wa utowaji wa haki  ikiwemo kusajili mashauri kwa njia ya mtandao.

Mafunzo haya  ni yale yaliyofunguliwa na Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mnamo tarehe 29 Novemba, 2021 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja  na Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama wa miaka mitano wa mwaka 2018/19-2022/23.



Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akiwasilisha mada ya Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania kwenye mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Picha ya baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Pichani  washiriki wa mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Naibu Wasajili wapya na watendaji  wa Mahakama kwenye picha  wakifuatilia mada iliyotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani) ambayo yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


0 comments:

Post a Comment