Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo amewataka Naibu Wasajii na Watendaji kuwa waadilifu, wachapa kazi na kuheshimu kila mtu bila kujali umri, hadhi yake au nafasi yake katika Jamii. Aliyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo elekezi yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Dkt. Kihwelo aliwaeleza washiriki hao kuwa
hawakupata nafasi hiyo kwa bahati bali walistahili kutokana na sifa zao za utendaji kazi uliotukuka na kutokuwa na bila shaka
watazitumikia nafasi hizo kwa bidii na uadilifu huku wakiheshimu mamlaka,
madaraka na majukumu waliyonayo na yale ya wale watakaofanya nao kazi.
Aliendelea kuwasisitiza washiriki hao kuwa wao ni
injini ya Mahakama hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu ili
walio chini yao wafuate nyayo zao.
“Ni tegemeo la kila mmoja wetu kuwa nyinyi ndio
mtakuwa kioo cha tabia njema na sio kinyume chake” alisema Dkt. Kihwelo.
Hatahivyo, Dkt. Kihwelo aliwaasa viongozi hayo
kuwa wasimamizi wazuri wa maadili na nidhamu katika maeneo yao ya kazi na
kuongeza kuwa wao ni viongozi hivyo wanapaswa kuwa watu wenye uwezo wa kufanya
maamuzi yenye kuzingatia hekima na
busara kwa faida ya watumishi, wadau, Mahakama na Taifa.
Akitaja sifa kubwa iliyopo Mahakamani kuwa ni Upendo, Udugu na Mshikamano,
aliwatoa wasiwasi kwa kuwaeleza kwamba
wasiwe na shaka kwani watapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa watangulizi wao
pamoja na wale watakaowakuta vituoni.
Kwa upande wake Mhe. Happines Ndesamburo akitoa shukrani kwa niaba ya Naibu Wasajili kwa kuushukuru uongozi mzima wa mahakama kwa kuwawezesha kwa mara ya kwanza wasajili hao kupata mafunzo hayo elekezi.
Mhe. Ndesamburo alieleza kuwa mafunzo haya yatakuwa ni nyenzo muhimu katika utendaji wao wa kazi za kila siku ili kufikia dira na dhima ya mahakama ya utoaji haki kwa wote na kwa wakati.
Aliongeza kuwa mafunzo waliyopata yamewaandaa
vyema na kuahidi kwamba watakapokuwa kwenye vituo vyao vya kazi watatoa huduma za
kiwango cha juu na kuhakikisha kwamba
wateja wao watatoka wakiwa wameridhika.
Kwa upande wa Watendaji wa Mahakama Bw. Tutubi
Mangazeni Mtendaji wa Mahakama Kuu Tanga akitoa neno la shukrani kwa niaba ya
watendaji wa mahakama walioshiriki mafunzo hayo alisema kuwa mafunzo haya
yamekuwa ya umuhimu sana kwao kwani yamewajengea uwezo na kujifunza mambo mengi
ambayo walikuwa hawayafahamu.
Bw. Mangazeni alitoa pendekezo kwa uongozi wa
Chuo kwamba kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo ni vyema naibu wasajili na
watendaji wa mahakama ambao hawajapata mafunzo hayo wapewe fursa ya kupata
mafunzo kama hayo ili waweze kutekeleza
majukumu yao kwa ufanisi na weledi.
Mafunzo haya ya siku tano kwa naibu wasajili na
watendaji wa mahakama yalifunguliwa na Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mnamo tarehe 29 Novemba, 2021 ikiwa ni
sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013,
Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya
Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja na Mpango Mkakati wa miaka
mitano wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wa mwaka 2018/19-2022/23.
Picha ya juu na chini ni baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi ya Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama wakipokea vyeti vyao baadha kumalizika kwa mafunzo hayo ya siku tano.
Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akiwa katika picha cha pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi ya Naibu Wasajili na Watendani wa Mahakama.
0 comments:
Post a Comment