Na Innocent Kansha – Mahakama.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama –
Lushoto Bw. Goodluck Chuwa amewakumbusha washiriki wa mafunzo ya Madalali na
Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuwa mafunzo hayo yameanzishwa mahsusi kwa lengo
la kuweka utaratibu rasmi wa kurasimisha namna ya kuwapata Madalali pamoja na
Wasambaza Nyaraka za Mahakama kitu ambacho hakikuwepo hapo awali.
Akifungua mafunzo ya siku 14 ya awamu ya nane
toka kuanzishwa kwake mwaka 2018, leo tarehe 6 Disemba 2021 katika Ukumbi wa
Shule ya Sheria kwa vitendo jijini Dar es salaam Bw. Chuwa alisema,
ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa Madalali na Wasambaza nyaraka za
Mahakama wenye sifa, Muhimili kupitia Mpango Mkakati wake wa kwanza wa mwaka
2015/2016 – 2019/2020 na Mradi wa Uboreshaji wa Mahakama kupitia mradi wa
huduma zinazomlenga mwananchi, iliandaa kanuni ziitwazo Kanuni za Uteuzi,
Gharama, Malipo na Nidhamu za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama,
Tangazo la Serikali Namba 363 la 2017 (The Court Brokers and Process
Servers (Appointment, Remuneration and Disciplinary) Rules, GN. 363 of 2017).
Kwa kuzingatia jina la kanuni linavyosomeka
kanuni hizo zinahusu uteuzi, gharama, malipo na nidhamu za Madalali na
Wasambaza Nyaraka za Mahakama ambapo mchakato huo ulikamilika mwaka 2017 baada
ya kupata kanuni hizo ambazo zilitolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, aliongeza Bw.
Chuwa.
“Kwa kuanzishwa mafunzo haya na kufuatiwa kwa
kutungwa kwa kanuni hizo, hivi sasa Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka
za Mahakama zimekuwa ni kada mbili tofauti na hivyo mtu ana uwezo wa kuchagua
moja kati ya kada hizo na ndiyo maana baadhi ya washiriki wa mafunzo haya
wanasomea kada zote wakati kuna baadhi wanasomea kada moja tu”, alifafanua
Kaimu Mkuu huyo.
Kaimu Mkuu huyo aliongeza kuwa, lengo kuu la
mafunzo hayo ni kuboresha utoaji huduma kwa jamii, kuongeza weledi na
kuhakikisha kuwa Mahakama inakuwa na Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama
wenye maadili, mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi. Ili kuweza kufikia huko
ni muhimu sana kuwa na utulivu wa kutosha na kuzingatia yale yote yaliyopangwa
katika ratiba ya mafunzo hayo, ushiriki kamilifu ndiyo utakaowafikisha kwenye utoaji
wa huduma bora.
Mafunzo hayo yanafanyika kwa mujibu wa Kanuni
ambapo kupitia kanuni hizo mtu yeyote mwenye nia ya kufanya kazi ya udalali na
Usambazaji Nyaraka za Mahakama anapaswa kupata mafunzo hayo.
Akiongelea ubora wa mafunzo Bw. Chuwa alisema,
kuanzishwa kwa mafunzo hayo ni mojawapo ya sehemu ya maboresho makubwa
yanayoendelea katika muhimili wa Mahakama. Ili kuondoa malalamiko mengi
yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi na moja ya eneo lenye kulalamikiwa sana ni
ukosefu wa uadilifu wakati wa utekelezaji wa majukumu ambapo kwa kufanya hivyo
kutawawezesha Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kufanya kazi kwa
uadilifu na kufuata kanuni zilizopo.
Akiwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo Bw.
Chuwa alisema, Madalali wa Mahakama ni wadau muhimu sana katika utekelezaji wa
jukumu la utoaji haki kwa wananchi. Endapo mtafanikiwa kuhitimu mafunzo yenu na
kusajiliwa mtakuwa maafisa wa Mahakama ambao mtapewa jukumu la kutekeleza amri
halali za Mahakama. Jukumu hilo msipolitekeleza vyema mtalalamikiwa kwa kutokuwatendea
haki wananchi na kwa hiyo ni dhahiri kuwa Mahakama pia itakuwa imelalamikiwa.
Niwasihi kuwa baada ya kupata mafunzo haya
mkazingatie kanuni na maadili mtakayofundishwa katika kutelekeleza majukumu
yenu. Nafahamu kuwa mtajifunza mambo mengi sana katika kipindi hiki cha wiki
mbili, yakiwemo masuala ya maadili katika fani ya udalali na usambazaji nyaraka
za Mahakama, “kila fani ina maadili yake, wale watakaopata nafasi ya kufanya
kazi ya udalali au usambazaji nyaraka za Mahakama ni muhimu kuzingatia maadili
ya kazi hiyo”, alitilia mkazo Kaimu Mkuu huyo.
Bw. Chuwa akatoa rai kwa washiriki wa mafunzo
hayo kuwa, wakati mnaendelea na mafunzo wekeni ndani yake pia mijadala huru
itakayowasaidia kuboresha utendaji kazi wenu ili kupunguza malalamiko
yanayotokana na wananchi kutokupata huduma bora. Msisite kuchangia uzoefu wenu
kwa lengo la kuboresha na kuwaeleza wengine kipi kinachotakiwa kufanyika au
kueleweka. Kwenu washiriki kosa hata liwe dogo sana katika utekelezaji wa
majukumu yenu linaweza kuleta madhara makubwa sana kwa mtu binafsi, Familia,
Mahakama na Taifa kwa ujumla.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa amewakumbusha washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama (hawapo pichani) kuwa mafunzo hayo yameanzishwa mahsusi kwa lengo la kuweka utaratibu rasmi wa kurasimisha namna ya kuwapata Madalali pamoja na Wasambaza Nyaraka za Mahakama.
Picha ya pamoja ya washiriki wa Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa na meza Kuu mara baada ya Mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Sheria kwa Vitendo Jijini Dar es salaam, (katikati) ni mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa, kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Masjala Kuu, Mhe. Victoria Nongwa na kushoto ni Mhadhiri na mratibu wa mafunzo ya Udalali na Usambazaji Nyaraka za Mahakama – Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bi. Hamisa Mwenegoha.
Picha ya pamoja ya washiriki wa Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa na meza Kuu mara baada ya Mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Sheria kwa Vitendo Jijini Dar es salaam, (katikati) ni mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bw. Goodluck Chuwa, kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Masjala Kuu, Mhe. Victoria Nongwa na kushoto ni Mhadhiri na mratibu wa mafunzo ya Udalali na Usambazaji Nyaraka za Mahakama – Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bi. Hamisa Mwenegoha.
0 comments:
Post a Comment