Desemba 1 kila mwaka ni siku ambayo dunia huadhimisha Siku ya UKIMWI. Nchini Tanzania kauli mbiu ya maadhimisho ya siku hiyo yalikuwa “Zingatia Usawa, Tokomeza Ukimwi, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko”.
Kitaifa maadhimisho haya yalifanyika
mkoani Mbeya wakati kwa upande wa mkoa wa Tanga yalifanyika wilaya ya Muheza na
katika ngazi ya wilaya ya Lushoto yalifanyika katika kata ya Mwangoi, jimbo la
Mlalo. Mgeni rasmi katika maadhimisho
hayo alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lushoto Bi Ikupa Mwasyoge.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
kilishiriki katika maadhimisho hayo kupitia klabu ya HeForShe. HeForShe ni
klabu ya wanachuo iliyoanzishwa na mwaka 2016 na Mkuu wa Chuo, Mhe. Dkt. Paul
F. Kihwelo Jaji wa Mahakama ya Rufani. Klabu hii ilianzishwa kwa lengo la kuhamasisha
masuala ya kijinsia Chuoni. Klabu hii inatumia mtoto wa kiume katika kuinua
nafasi ya mtoto wa kike. Klabu inafanya
shughuli mbalimbali za uhamasishaji na kutoa elimu katika shughuli nyingi
zinazofanyika wilayani Lushoto hususani katika mashule na maadhimisho.
Akizungumza na wananchi katika
maadhimisho hayo, Bi. Ikupa aliwakumbusha wananchi mambo mbalimbali ambayo bado
yanapelekea ongezeko la maambukizi mapya ambayo ni pamoja na vitendo vya
ukatili vinavyofanyika katika jamii, mila potofu za kurithi wake na vijana
wengi kujihusisha na ngono isiyo salama.
Bi. Ikupa alisisitiza kuepuka kuwanyanyapaa watu wenye maambukizi. Pia aliendelea kuwashawishi wananchi kujitokeza kupima na wale wote watakaopimwa na kukutwa na maambukizi kujitahidi kutumia dawa kwa uaminifu ili kuimarisha afya zao na kuwa na uwezo wa kuendelea na majukumu yao ya kila siku.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
kupitia klabu ya HeForShe inaungana na jamii ya wananchi wote wa
Lushoto katika kukemea vikali mambo yote yanayopelekea maambukizi ya UKIMWI.
0 comments:
Post a Comment