Na Faustine Kapama – Mahakama, Dodoma
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 31 Januari, 2022
amefungua Kongamano la wadau wa sheria na utoaji haki nchini ambapo amewahimiza
washiriki wote kujadili jinsi mfumo wa haki jinai uliopo unavyoathiri wahanga
na washitakiwa wa makosa ya jinai.
Amesema
kuwa Kongamano hilo linalofanyika katika ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma ni
fursa mwafaka kwa Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya
Uingereza kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali, hususani maeneo ya
mfumo wa haki jinai ambapo Mahakama zote mbili wanashiriki changamoto
zinazofanana.
"Kwa
mfano, hatua ya awali ya shauri la kijinai (committal proceeding) ni eneo
ambalo sisi sote tunashiriki. Madhumuni ya msingi ya kuendesha mwenendo huu ni
kuamua kama kuna ushahidi wa kutosha kumruhusu mtu anayetuhumiwa kwa kosa
kusikilizwa mbele ya Jaji. Kwa nini basi, kuwa na mwenendo huu wenye nia njema
ubadilike kuwa kichaka cha ucheleweshaji uliopitiliza nchini Tanzania?” amehoji
Mhe. Prof. Juma.
Jaji
Mkuu amesema kuwa wamekuwa wakikumbana na ucheleweshaji mkubwa wakati wa
kuendesha hatua hizo za awali za mashauri ya jinai yanayosikilizwa na Mahakama
Kuu, hivyo katika Kongamano hilo Mtaalamu kutoka Uingereza, Jaji Nic Madge
ataweza kutoa uzoefu wake na namna nchi yake inavyofanya ili kuepuka
ucheleweshaji huo.
Wawezeshaji
wengine katika Kongamano hilo ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Chande Othman, Majaji wengine wabobezi kutoka nchini Uingereza, Jaji Lain
Bonomy na Nicholas Blake, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Awamu
Mbangwa, Mhe. Edwin Kakolaki na Mhe. Dkt. Zainab Mango pamoja na Kamishna
Mstaafu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Bw. Laurean Tibasana.
Jaji
Mkuu ana imani kuwa washiriki wa Kongamano hilo watanufaika vya kutosha
kutokana na mada mbalimbali zitakazowasilishwa na Majaji na wadau
wengine ambao wamebobea katika maeneno kadhaa yananyohusu haki jinai. Ametoa
shukrani zake kwa Serikali ya Uingereza kwa kuendelea kutoa mchango wa kifedha
kupitia mpango endelevu wa kupambana na rushwa (BSAAT).
"Kongamano
la leo ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano ulioanza tangu mwaka 2017
katika Mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola (CMJA).
Licha ya janga la UVIKO-19, tunatarajia kuendeleza shughuli mbalimbali, ikiwa
pamoja na mafunzo, miaka mingi zaidi ijayo,” Jaji Mkuu amesema.
Awali,
akizungumza katika Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Gerald Ndika, ambaye ni Jaji wa
Mahakama ya Rufani amesema kuwa Programu hiyo iliyoandaliwa ni moja ya programu
nyingi za maendeleo ya kitaaluma ambazo zimeundwa na Chuo kwa kushirikiana na
washirika wake.
Mhe.
Dkt. Ndika amesema kuwa Kongamano hilo ni ushuhuda wa wazi kwamba Chuo hicho
kimekuwa kikijitahidi kutimiza majukumu yake chini ya Sheria ili kuboresha
utoaji wa haki nchini kwa kutoa mafunzo yanayofaa kwa maafisa wa Mahakama na
watumishi wengine.
Kongamano
hilo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Mahakama ya
Uingereza na kuratibiwa na Taasisi ya Majaji Wastaafu nchini Uingereza iitwayo
Slynn Foundation wakishirikiana na IJA kupitia ufadhili wa Programu ya Kitaifa
ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Tanzania zinazohusika na kuzuia na
kupambana na Rushwa (BSAAT).
Kuandaliwa
kwa Kongamano hilo ambalo litafanyika kwa siku moja ni sehemu ya hitihada za
Mahakama ya Tanzania katika kuwajengea uwezo maafisa wa Mahakama na wadau
wengine wa sheria ya haki nchini katika kutekeleza majukumu yao hususani utoaji
wa haki jinai.
Mbali
na maafisa wa Mahakama waliostafu na walioko kazini pamoja na Mahakama ya
Uingereza, washiriki wengine katika Kongamano hilo ni Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Katiba na Sheria na maafisa kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi
ya Wakili Mkuu wa Serikjali, ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU).
Kongamano
hilo ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini ambayo kilele
chake ni tarehe 2 Februari, 2022, pamoja na mambo mengine, limelenga kujadili
uboreshaji mbalimbali uliofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika utoaji wa haki
jinai pamoja na kubadilishana uzoefu wa namna haki jinai kwa wahanga na
washitakiwa unavyofanyika kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya
Uingereza.
Hii
ni mara ya pili Kongamano hili linafanyika baada ya lile la kwanza ambalo
lilifanyika katika Wiki ya Sheria mnamo mwezi Februari 2020 jijini Dar es
Salaam.
Maafisa Wandamizi wa Mahakama ya Tanzania, ambao ni Msajili Mkuu, Mhe. Wilbert Martin Chuma (kushoto) na Mtendaji Mkuu, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kutoka kushoto) wakiwa na Majaji Wastaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sauda Msafiri na Mhe. Januari Msoffe (kulia) wakifuatilia moja ya mada zilizokuwa zinawasilishwa kwenye Kongamano hilo.
0 comments:
Post a Comment