Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe, Dkt. Hussein Ali Mwinyi mapema leo amezidua maadhimisho ya Wiki ya Sheria na kuwakumbusha watumishi wa Mahakama ya Tanzania na wadau wote wa sekta ya sheria nchini umuhimu wa kuzingatia maadili katika utoaji haki na kuheshimu sheria hatua itakayosaidia kujenga umoja, amani na mshikamano ili kuhakikisha malengo waliyojiwekea yanatimia.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Mwinyi amebainisha
kuwa kwa nafasi yake kama Rais wa Zanzibar, ambaye ameitumikia Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa ngazi mbalimbali ikiwemo uwaziri, anatambua na
kuheshimu umuhimu wa sheria kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania pia anafahamu umuhimu wa sheria katika kujenga umoja, amani, udugu na
mshikamano, hivyo mafanikio ya kiuchumi, kibiashara na kiuwekezaji hutegemea
kuwepo kwa misingi imara ya utawala bora, sheria na uhuru wa Mahakama.
“Ni dhahiri kuwa ustawi wa wananchi wetu, kwa kiasi kikubwa
unategemea kuwepo kwa sheria madhubuti zinazotambua ukweli kuwa wananchi wengi
kutoka pande zote mbili za Muungano ni maskini. Hivyo, sheria zetu na taratibu
za kimahakama ndizo zitakazosaidia kuwainua na kufanikisha shughuli zao
kiuchumi na kijamii, kwa kuwa uwepo wa sheria bora zinazosimamiwa vyema ndio
kutafanikisha uchumi wao, biashara na shughuli zao za kila siku za kujitafutia
kipato,”amesema Dkt. Mwinyi.
Kiongozi huyo amesisitiza kuwa upo umuhimu wa kuheshimu sheria
zetu kwa kuzingatia ukweli kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya
utawala bora ni kuwepo kwa vitendo vya rushwa, ubadhirifu, uzembe, ikiwa ni
pamoja na kukosa uwajibikaji na kutofuata sheria hatua inayopelekea ukiukwaji
kwa maadili.
Kiongozi huyo amesisitiza kuwa upo umuhimu wa kuheshimu sheria
zetu kwa kuzingatia ukweli kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya
utawala bora ni kuwepo kwa vitendo vya rushwa, ubadhirifu, uzembe, ikiwa ni
pamoja na kukosa uwajibikaji na kutofuata sheria hatua inayopelekea ukiukwaji
kwa maadili.
“Nachukua fursa hii kupongeza jitihada mbalimbali
zinazochukuliwa na Mahakama ya Tanzania katika kuimarisha huduma za kutoa haki
kwa wananchi na kuhakikisha mnaongeza kasi ya kusikiliza mashauri mbalimbali
yanayowasilishwa katika ngazi zote za Mahakama,” amesema Dkt. Mwinyi.
Rais Mwinyi ameipongeza Mahakama kwa hatua ya kuanzisha Mahakama inayotembea kwani itasaidia kufikisha huduma ya utoaji haki kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini. Huku akipongeza hatua mbalimbali zilizochukuliwa ikiwemo kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili, jambo ambalo limewapa Watazania matumaini kama hatua mojawapo ya maendeleo ya sekta ya sheria nchini.
Aidha kiongozi huyo ameshauri kuongeza jitihada za kupata wataalam wa lugha ya alama pamoja na kuimarisha miundombinu inayozingatia uwepo wa Watanzania wenye mahitaji maalum, wakiwemo watu wenye ulemavu wa aina tofauti hatua itakayosaidia makundi maalum kupata haki zao bila kikwazo chochote.
Akizungumzia kuhusu ya ushirikiano iliyopo baina na Mahakama ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mahakama ya Zanzibar. Rais Mwinyi ameelezea
kuridhishwa na ushirikiano uliopo huku akiwasihi kuuendeleza ushirikiano huo
kwa manufaa mapana ya Taifa.
“Nimeelezwa kuwa uhusiano huo ni wa muda mrefu toka mwaka 1965,
nafurahi kuona kuwa ushirikiano huo unaendelezwa kwa kupeana uzoefu na utaalam
utakaoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yenu. Natoa wito kuendeleza
ushirikiano huo kwa lengo la kuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya utendaji na
kuongeza kasi na ufanisi katika Mahakama zetu,” alisema.
Mhe. Dkt Mwinyi amepongeza mafanikio makubwa aliyoyaona wakati akitembelea maonesho yaliyoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria, ambapo ameelezwa kuwa huduma zitakazotolewa kwa siku zote za maonesho ni moja ya utekelezaji wa nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama na malengo makuu ya nguzo hiyo ni pamoja na kuimarisha imani ya wananchi na kuongeza uelewa na ufahamu wao wa taratibu na shughuli za utoaji haki nchini.
Katika hatua nyingine Rais Mwinyi amekubaliana na uamuzi wa
kuzidi kutoa taaluma kuhusu huduma za Mahakama kwani bado haijawafikia wananchi
walio wengi. Amebainisha kuwa ni wazi wananchi watanufaika na huduma hiyo,
hivyo ametoa wito kwa wananchi wote kuitumia fursa iliyopo vizuri kwa kufika
kwa wingi kwenye maonesho hayo.
“Kupitia maenesho haya pia nimeshuhudia uboreshaji makubwa
unaofanywa na unaoendelea kufanywa katika mnyororo mzima wa utoaji haki. Ni
dhahiri kuwa uboreshaji mkubwa niliyoshuhudia ya matumizi ya TEHAMA ni dalili
njema ya matayarisho makubwa ya kupokea na kuendeleza matumizi ya TEHAMA ndani
ya Mahakama zetu. Natoa pongezi za kipekee kwa uongozi wa Mahakama ya Tanzania
na watumishi wote kwa kuendeleza uboreshaji huu mkubwa,” amesema.
Mhe. Dkt Mwinyi pia alitumia fursa hiyo adhimu ya uzinduzi wa
Wiki ya Sheria kutoa wito kwa wanasheria na wataalam wote wa sheria, viongozi
wa Mahakama na Watumishi wote wa sekta ya sheria kuielewa na kuifanyia kazi
mipango mikuu ya uchumi inayotekelezwa na Serikali zote mbili nchini katika
jitihada za kupunguza umasikini na kuwa na uchumi unaolingana na ushindani wa
karne ya 21, hivyo kuwa huru kutoa ushauri wao wa kisheria kwa lengo la
kuifanikisha.
Ameeleza kuwa anatambua kuwa zipo sheria ambazo huenda zikawa ni kikwazo cha kufikia matarajio yetu ya kiuchumi na hasa uchumi wa bluu na ustawi wa jamii, hivyo Sheria hizo zitahitaji kufanyiwa marekebisho ili zifanikishe mipango yetu ya uchumi wa kisasa hivyo naomba tumieni utaalam wenu kuzishauri Serikali zetu kuchukua hatua za kurekebisha sheria ambazo zinakasoro, nasi tutafanya hivyo kwa maslahi mapana ya nchi yetu na Watanzania wote.
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yamezinduliwa leo Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali yakiwa na kauli mbiu isemayo Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho kuelekea Mahakama Mtandao.
Baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi pamoja na mkewe Mama Mariam Mwinyi wakijiandaa kushiriki matembezi ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma tarehe 23 Januari, 2022.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi (wa tatu kulia) akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakipasha viungo kabla ya kuanza matembezi kuadhimisha Wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma tarehe 23 Januari, 2022.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt.
Hussein Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi pamoja na viongozi wengine wa
Serikali katika matembezi kuadhimisha Wiki ya Sheria yanayofanyika katika
viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma kuanzia tarehe 23 Januari, 2022.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein
Mwinyi (wa tatu kulia) akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi pamoja na viongozi
wengine wa Serikali wakinyoosha viungo baada ya kukamilisha matembezi ya
kilometa saba wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Sheria inayofanyika katika viwanja
vya Nyerere Square Jijini Dodoma tarehe 23 Januari, 2022.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein
Mwinyi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika
katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma tarehe 23 Januari, 2022.
Baadhi ya wadau kutoka
Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali wakimsikiliza Mgeni rasmi Dkt. Hussein
Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia katika ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya
Sheria yaliyoanza leo Januari 23,2022 katika viwanja vya Nyerere Square Jijini
Dodoma na yanatarajiwa kukamilika Februari Mosi mwaka huu katika kilele cha
Siku ya Mahakama.
0 comments:
Post a Comment