Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Friday, November 25, 2022

IJA YATOA MAFUNZO ELEKEZI KWA SERIKALI YA WANACHUO

 Na Rosena Suka, IJA

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo leo tarehe 25 Novemba, 2022 amefungua mafunzo elekezi ya siku moja kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo wa IJA (IJASO) yaliyofanyika Chuoni Lushoto.

Katika ufunguzi huo  Mkuu wa Chuo amewaeleza viongozi hao  kwamba wanawajibu mkubwa wa kuwahudumia kwa uadilifu wanachuo wenzao  kwani wao ni kiungo  katika kufikisha yale ambayo yanatoka kwenye Uongozi wa Chuo kwenda kwa wanachuo na kutoka kwa wanachuo kwenda kwenye Uongozi wa Chuo.

Mkuu wa Chuo aliwasisitiza viongozi hao wa wanachuo kutumia vikao mbalimbali watakavyokuwa navyo ili kutatua changamoto zao na sio kulalamika au kupeleka changamoto zao kwenye mamlaka zisizohusika. Aliendelea kwa kuwataka viongozi hao kusimamia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuonyesha mfano bora kwa wanachuo wenzao,

Mkuu wa Chuo, aliwakumbusha viongozi hao kuwa na ushirikiano kati ya wao wenyewe, watumishi wa Chuo na  wanachuo wenzao bila kusahau mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka.

Kwa upande wake Rais wa Wanachuo, Bw. Meshack D. Tupa alipokuwa akitoa shukrani zake ameushukuru Uongozi wa Chuo kwa kuandaa na kuwapatia semina hiyo elekezi na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watumishi wa Chuo na wanachuo wanaowawakilisha.

Viongozi hawa wa wanafunzi katika semina hiyo elekezi wamepitisha katika mada mbalimbali ambazo ni Masuala ya Usalama na Maadili, Unyanyasaji na Ukatili wa Kijinsia, Uongozi na Taaluma, Usimamizi wa Rasilimali za IJASO na Usitawi wa Wanachuo.

IJA imekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo elekezi kwa Serikali ya Wanachuo mara tu inapowekwa madarakani.


Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akihutubia Viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi ya siku moja yaliyofanyika Chuoni Lushoto

 Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chuo na wawezeshaji wa mafunzo elekezi. 












Pichani juu ni washiriki wa mafunzo elekezi ambao ni viongozi wa nafasi mbalimbali katika serikali ya wanachuo wakifuatilia mafunzo hayo.

0 comments:

Post a Comment