Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma

Jaji kiongozi wa Tanzania

Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania (katikakati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa stashahada ya sheria

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Saturday, February 24, 2024

UJUMBE WA BENKI YA DUNIA WATEMBELEA IJA

 Na: Rosena Suka, IJA

Leo tarehe 24 Februari, 2024 ujumbe wa Benki ya Dunia umetembelea mradi wa ujenzi wa studio ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ unaofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.  Mradi huo ni kati ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa Benki wa Benki ya Dunia.

Ziara hiyo imewakilishwa na Maafisa wanne kutoka Benki ya Dunia ukiwa unaongozwa na Bi. Christine Owuor na Maafisa wengine watatu. Pamoja na Maafisa hao pia kulikuwa na watumishi kadhaa wa Mahakama ya Tanzania akiwemo  Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha.

Baada ya kuwasili Chuoni ujumbe huo ulifika katika eneo la Mradi wa ujenzi wa Studio jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ ambao umeanza tarehe 18 Februari, 2024 na unategemea kumalizika tarehe 18 Mei. 

Ujumbe huo pia ulipata maelezo ya uundwaji na matumizi ya studio hiyo itakavyo fanya kazi kutoka kwa Mhandishi Emmanuel Mbosso wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo. Pia alieleza kwa ugeni kuwa Jukwaa la kujifunzia mtandaoni limetengenezwa na wataalamu wa ndani ya Tanzania ambao ni kutoka Mahakama ya Tanzania, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo).

Jukwaa la mafunzo ya mtandao litarahisisha utoaji wa mafunzo kwa watumishi  wengi wa mahakama, kwa  gharama nafuu na kupunguza umbali wa kufuata mafunzo. 


Picha ya pamoja ya Maafisa wa Benki ya Dunia waliotembelea mradi wa ujenzi wa studio ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ unaofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. Waliokaa katika ni Bi. Christine Owuor ambaye Kiongozi wa Ujumbe kutoka Benki ya Dunia. Kushoto ni Jaji wa Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Mhe. Dkt. Paul Faustin Kihwelo na Kulia ni Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha. na waliosimama nyuma ni Maafisa wa Benki ya Dunia.

Picha ya juu na ya chini ni watumishi wa IJA na Mahakama waliokuwa kwenye mapokezi ya ugeni wa wakilishi wa Benki ya Dunia wakifuatilia taarifa mbalimbali zilizokuwa zinatolewa kuhusu mradi ujenzi wa  wa studio ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ unaofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. 


Mhandishi Emmanuel Mbosso wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo akitoa maelezo ya uundwaji wa studio ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’



Picha ya juu na chini ni Wajumbe wa Benki ya Dunia na Viongozi wa Mahakama ya Tanzania  wakipata maelezo ya mradi wa ujenzi studio ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ kutoka kwa Mhandisi wa mradi huo.


Meza kuu na viongozi kutoka Mahakama ya Tanzania


Meza Kuu na Sekretarieti

Meza kuu na Baadhi ya watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


Meza Kuu na baadhi wa watalaamu walioshiri kutengeneza jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ 
















Saturday, January 27, 2024

SPKA WA BUNGE AZINDUA WIKI YA SHERIA

 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson amezindua maadhimisho ya wiki ya sheria leo tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

Katika uzinduzi huo Mhe. Dkt. Tulia  alikuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo na amewataka washiriki wa maonesho hayo kuelimisha wananchi kwenye mambo mbalimbali yahusuyo sheria.

Sambamba na uzinduzi wa wiki ya sheria, Mhe. Dkt. Tulia pia amezindua rasmi Mfumo wa Udukuzi na Tafsiri (TTS) wa Mahakama ya Tanzania ambao utatumika katika kutafsiri na kunukuu lugha zinazotumika mahakamani mbazo ni Kiswahili na Kingereza na utakaorahisisha zaidi huduma ya upatikanaji haki kwa wananchi.

 “Naipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa ya kuleta Mfumo huu, ambao naamini utarahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi,” amesema Mhe. Dkt. Tulia. 

 Aidha, Mhe. Dkt. Tulia ametoa rai kwa wadau wote wa Mahakama kufanya uwekezaji wa miundo mbinu ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya Mahakama katika kuboresha utendaji kazi na kuongeza ubora wa huduma.

 ‘‘Naamini kazi kubwa sasa, hasa wadau wa Mahakama ni utengenezaji wa mfumo hasa wa kitehama, utakaowasaidia wadau hawa kufungamanisha na kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai unaosomana, ili kubadilishana taarifa kuanzia hatua ya upelelezi, ufunguaji wa mashauri, msaada wa kisheria, uendeshaji wa mashtaka, kusikiliza mashauri na utoaji uamuzi,” amesema Mhe. Dkt. Tulia. 

 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, akiwa anamkaribisha mgeni rasmi amesema, Mahakama ya Tanzania imewekeza kwenye matumizi ya TEHAMA kwa kuweka  Mifumo mbalimbali ili kurahisisha  huduma za utoaji haki kwa wananchi.

Mhe. Prof. Juma aliendelea kwa kueleza faida za mfumo huo  kuwa  utawaapunguzia  kazi Majaji na Mahakimu waliyokuwa wanaifanya ya kuandika kwa mkono mienendo ya mashauri kwa mfumo huu utarahisha na kufanya wananchi kupata haki kwa wakati.

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ni miongoni mwa Wadau mbalimbali wa Mahakama, ambapo wanashiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza tarehe 24 Januari mpaka 30 Januari, 2024. Wadau wengine wa Mahakama wanaoshiriki katika maonesho hayo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Katika maadhimisho haya ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria, kauli mbiu ni  “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.

Maonesho haya yaliyozinduliwa leo yatafanyika kwa muda wa siku nane ambapo yanatarajiwa kukamilika tarehe 30 Januari, 2024 ambapo yatahitimishwa kwa kilele cha Siku ya Sheria itakayofanyika tarehe 01 Februari, 2024 na mgeni rasmi wa siku hiyo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson akihutubia wananchi kwenye uzinduzi wa  maadhimisho ya wiki ya sheria uliofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.


 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson akiwa na Viongozi wa Mahakama ya Tanzania kwenye matembezi kwa ajili ya uzinduzi wa  maadhimisho ya wiki ya sheria uliofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

Viongozi wakiwa katika matembezi maalum kwa ajili ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria yaliyofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.


Jaji wa Mahakama Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Chuo wakati wa  uzinduzi wa  maadhimisho ya wiki ya sheria uliofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.


 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson(katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson(katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa maonesho wiki ya sheria,

Baadi ya washiriki wa maonesho ya Wiki ya Sheria wakiwa wanafuatilia uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Sheria uliofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma


Aliyewahi kuwa mwanachuo IJA alipotembelea Banda la Chuo kwa ajili ya kupata taarifa mbalimbali kuhusiana na Chuo


Thursday, December 14, 2023

SERIKALI YA WANACHUO YAPATA MAFUNZO ELEKEZI

 Na Rosena Suka, IJA

Kaimu Mkuu wa Chuo na Naibu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Taaluma, Tafiti na Ushauri, Bw. Goodluck Chuwa leo tarehe 14 Desemba, 2023 amefungua mafunzo elekezi ya siku moja kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo wa IJA (IJASO) kwa mwaka wa masomo 2023/2024 yaliyofanyika Chuoni Lushoto.

Kwenye ufunguzi huo  Bwana Chuwa amewaeleza viongozi hao  kwamba lengo kuu la mafunzo hayo elekezi ni kuwajengea uwezo kwenye utekelezaji wa  majukumu yao ya uongozi kwa kufuata miongozo ya sheria, taratibu na kanuni za chuo na taifa kwa ujumla. 

Bwana Chuwa aliendelea kwa kusema viongozi hao wamebeba dhamana kubwa ya kuwahudumia wanachuo wenzao  kwa sababu wao ni kiungo  katika kuwafikisha maelekezo yote yanayotolewa na Menejimenti kwenda kwa wanachuo na kutoa mrejesho kutoka kwa wanaowangoza kuja kwenye menejimenti bila kuongeza au kupunguza uhalisia.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Fatihiya Massawe aliwasisitiza viongozi hao wa wanachuo kutendea haki nyadhifa walizonazo kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili waliowachugua kwani serikali ya wanachuo ni chombo muhimu katika musitakabali wa Chuo.

Prof. Masawe aliwakumbusha viongozi hao kusimamia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuonyesha mfano bora kwa wanachuo wenzao.

Katika semina hiyo elekezi viongozi hawa wamepitishwa katika mada mbalimbali zilizotolewa na watoa mada kutoka katika taasisi za umma Wilayani Lushoto ambao ni Mwakilishi kutoka Taasisi ya Kupambana na Rushwa (PCCB), Mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi na Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).  Mada nyingine zilitolewa na vitengo na Idara vya ndani ya Chuo ambavyo ni Mkaguzi wa ndani, Mhasibu Mkuu,Mdhibiti ubora, Msajili na Mshauri wa Wanachuo.

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kina utaratibu wa kutoa mafunzo elekezi kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kila mwaka mara tu serikali hiyo inapowekwa madarakani.


Kaimu Mkuu wa Chuo na Naibu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Taaluma, Tafiti na Ushauri, Bw. Goodluck Chuwa akifungua Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO


Naibu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Fatihiya Massawe akiwaelekeza Viongozi wa Serikali ya Wanachuo katika  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO


Inspecta wa Polisi kutoka Wilaya Lushoto Karim Bruno akiwasilisha mada kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO

Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Vya Taifa Wilayani Lushoto (NIDA) Bwana Francis Daniel akiwasilisha mada kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO


Mwakilishi kutoka Taasisi ya Kupambana na Rushwa  Wilayani Lushoto (PCCB) Bwana Norbert Massaba akiwasilisha mada kwa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO


Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO wakifuatilia mada

Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO wakifuatilia mada

Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO wakifuatilia mada

Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO wakifuatilia mada


Viongozi wa Serikali ya Wanachuo kwenye  Mafunzo Elekezi kwa Serikali ya Wanachuo  IJASO wakifuatilia mada











Friday, November 24, 2023

IJA NI TANURI LINALOPIKA WAHITIMU BORA

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekipongeza Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kutoa wahitimu waliopikwa katika tanuri la vielelezo vya ubora  na ufanisi wa huduma kwakuwa na uwezo wa kukabiliana na kumudu mabadiliko yoyote katika soko la ajira. Rai hiyo aliitoa leo tarehe 24 Novemba, 2023 wakati wa mahafali ya 23 kwa wahitimu 831 wa ngazi mbalimbali wa  Chuo Cha Uongozi wa Mahakama yaliyofanyika Chuoni Lushoto.

Alisema kuwa kufanyika kwa mahafali ya Chuo ni uthibitisho wa mafanikio makubwa kwa Wanafunzi waliohitimu kupitia juhudi kubwa za Uongozi wa Chuo na wanataaluma. Aliendelea kwa kusema mahafali ni wakati mzuri wa kujitathmini na kutambua kuwa Chuo chetu kimepiga  hatua kubwa katika kutoa elimu bora, Mafunzo Endelevu ya kimahakama, kufanya tafiti na  ushauri elekezi kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa sheria wa  ndani na nje ya nchi. Mahakama ya Tanzania imekuwa ikivunia kuwa na Chuo chenye kutekeleza malengo yaliyokusudiwa.

Aidha,  Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha wahitimu kuwa ni muhimu kufahamu vyema mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yanayogusa Tanzania na Dunia kwenye matumizi ya Tecknolojia ya Habari na Mawasiliano yanayosukumwa na Akili Bandia ambayo yamefanya mabadiliko katika utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia za kisasa.

“Tahadhari muhimu hapa, kila mmoja wenu anatakiwa kubadilika na kujiongezea ujuzi na umahiri katika matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma. Uwezo uliotokana na Astashahada ya Sheria (Certificate), na Stashahada ya Sheria (Diploma in Law) peke yake hautakuwezesha kupata ajira za kiushindani katika Tanzania na Dunia ya Dijitali” alisema Mhe. Prof. Juma.

Pamoja na hayo Mhe. Prof. Juma amefarijika kwa kuona Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto umefikia hatua nzuri ya kukamilisha ujenzi wa jukwaa la ufundishaji wa elimu kwa njia ya ki-elekitroniki (E-LEARNING PLATFORM).  Akaendelea kwa kutaja faida kadhaa zitakazotokana na ufundishaji wa njia hiyo ya ki-elekitroniki ni pamoja na kuwafanya wanafunzi kuhudhuria masomo yao huko huko waliko  huku wakiendelea na kazi zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dkt. Gerald Ndika alisema Chuo kimepata mafanikio makubwa kwenye  kutoa Mafunzo, warsha na makongamano mbalimbali. Pamoja na mafunzo na makongamano yanayofanywa Chuo pia kinafanya tafiti mbalimbali kukidhi mahitaji ya  kuwajengea uwezo wataalamu wetu. Tafiti hizo zimepelekea Chuo kuandaa machapisho mbalimbali kama vile kitabu cha mkusanyiko wa maamuzi ya Mahakama kuhusu unyanyasaji na ukatili wa kingono kwa watoto.  Hii inadhihirisha waziwazi Chuo kinavyoshirikiana na jamii dhidi ya kupinga unyanyasi na kulinda na kutetea haki ya mtoto.

Mhe. Dkt Ndika aliendelea kwa kumhakikishia  Jaji Mkuu wa Tanzania kuwa Chuo kiko kwenye maandalizi ya kufatilia huduma zinaofanywa na wahitimu wake katika maeneo mbalimbali kwa kufanya tathimini mahususi.  Hii imetokana na wahitimu wa Chuo kuhitajika katika maeneo mbalimbali.

Naye Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo katika maelezo yake alimshukuru Mhe Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 20 Septemba 2023 kuridhia mapendekezo ya Kamati ya Raisi ya Utekelezaji (PIC) na kuidhinisha Muundo wa Mgawanyo wa Majukumu ya Chuo ili kuimarisha utendaji kazi.  Katika muundo huo umeanzisha Kurugenzi ya Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu ambayo jukumu lake kubwa litakuwa ni  kuratibu mafunzo ya Kimahakama kwa maafisa wa Mahakama na watumishi wengine wa Mahakama na wadau mbalimbali wa sekta ya sheria nchini.

Jumla ya wanachuo 851 wamehitimu masomo yao ambapo Astashahada ya Msingi ya Sheria (Basic Technician Certificate in Law) jumla ya wahitimu ni 336 ambapo wakike ni 177 na wakiume ni 159, Astashahada ya Sheria (Technician Certificate in Law) jumla ya wahitimu ni 242 ambapo wakike ni 101 na wa kiume ni 141 na kwa upande wa Stashada ya Sheria (Diploma in Law) jumla ya wahitimu ni 273 ambapo wakike ni 137 na wa kiume ni 136. 












Monday, August 14, 2023

Msajili mkuu wa Mahakama ya Tanzania afungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya 37

 

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amefungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo leo tarehe 14/08/2023.

Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yanafanyika hapa Chuoni IJA na yatadumu kwa siku tano hadi tarehe 18/08/2023.

Katika hotuba yake ya Ufunguzi Mhe. Chuma ambae ndiye alikuwa mgeni Rasmi  amewataka Mahakimu hao kwenda kusaidia kuondoa mrundikano wa mashauri katika Mahakama za mwanzo kama ambavyo Sera ya Mahakama ya Tanzania inavyotaka.

“Mpaka sasa bado Mahakama za Mwanzo zinaendelea kuongoza katika umalizaji wa Mashauri na kutokuwa na mrundikano wa mashauri, kwa hiyo tunategemea ongezeko lenu litaendelea kupunguza mzigo wa kazi wa kila hakimu na hatimaye kuendeleza sera ya Mahakama ya Tanzania kutaka kusiwe na mashauri yanayozidi miezi sita,” amesema Mhe. Chuma.

Pia Mhe. Chuma amewataka mahakimu wakazi hao wapya kujifunza matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano(TEHAMA) ili waweze kutekeleza vema majukumu yao hasa wakati huu Mahakama ya Tanzania ikiwa imejielekeza katika eneo hilo la Teknolojia.

“Karne hii ya 21 imetawaliwa na matumizi ya Teknolojia katika kuwahudumia wananchi, jifunzeni matumizi ya mifumo ya TEHAMA inayoendeshwa na Mahakama ili msipate ugumu mnapotekeleza majukumu yenu,” amesisitiza Mhe. Chuma.

Vile vile, Mhe. Chuma amewasisitiza washirika hao kuwa wanapotekeleza majukumu yao, basi hawana budi kuzingatia misingi ya haki za binadamu, maisha ya watu na ustawi wa Usalama wa nchi.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda amezungumzia muhimu wa mafunzo hayo kwa kubainisha kwamba yanalenga kuwapatia Mahakimu hao miongozo itakayowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Kimsingi umuhimu wa mafunzo haya ni kwa ajili ya kuwapatia muongozo Mahakimu wapya ambao wanaenda kuanza majukumu yao katika Mahakama za mwanzo, ukiwemo utoaji wa haki ambao ndio jukumu kubwa la Mahakimu hawa,” amesema Mhe. Dkt. Kisinda.

Ameongeza kuwa Mahakimu watapewa miongozo, maelekezo na miiko mbalimbali ambayo inahusiana na majukumu ya kule wanapokwenda kusimamia utoaji wa haki.

Nao baadhi ya Washiriki wa Mafunzo hayo akiwemo  Mhe. Aden William Ruvurahende ambae ni Hakimu Mkazi mpya amebainisha faida ya mafunzo hayo kwao wao washiriki.

“Kwa kweli suala hili la mafunzo kwetu sisi ni la muhimu sana kwa sababu ni mwanzo wa kujua majukumu yetu, na fursa ya kufahamu miongozo na kanuni  ya kimahakama  ili itusaidie kwa ajili ya utendaji haki pale tunapokwenda kuwahudumia wananchi,” amesema Mhe. Ruvurahende.

 Kuhusiana na mlundikano wa mashauri amebaininisha: “Kuhusiana na mrundikano wa mashauri Mahakamani, ni changamoto kwetu sisi ila tunakwenda kusaidia kutatua suala hilo.”

Nae Mshiriki Mhe. Salma Athuman Mwamende anabainisha kuwa Mahakama itarajie weledi, ufanisi, na uwajibikaji kutoka kwao.

 



Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akihutubia wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.


Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akizungumza wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.



Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma(katikati) wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.

Wa pili kushoto ni  Mhe. Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda, wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Bi. Patricia Ngungulu, wa kwanza kulia ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Kavumo Mndeme.




Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma(katikati) akiwa katika picha na baadhi ya baadhi ya Washiriki wa Mafunzo Elekezi ambao ni Wahe. Mahakimu Wakazi wapya wa mahakama za Mwanzo katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).

Wa pili kushoto ni  Mhe. Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda, wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu, wa kwanza kulia ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Kavumo Mndeme.




Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo Elekezi ambao ni Wahe. Mahakimu Wakazi wapya wa mahakama za Mwanzo wakiwa katika mafunzo hayo katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).





Jaji mstaafu ambae pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheira, Mhe. January Msoffe akiwasilisha mada kwa Washiriki wa Mafunzo Elekezi ambao ni Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akihutubia wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo yanayofanyika Chuoni IJA Lushoto.


Sunday, August 6, 2023

Naibu Waziri: IJA ni Chuo muhimu kwenye mambo ya haki






Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema kuwa Chuo cha Uongozi wa MahakamaLushoto(IJA) ni Chuo muhimu katika kuwajenga watu wanaosimamia masuala ya haki hapa nchini.
Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul amesema hayo leo Jumamosi tarehe 05/08/2023 wakati akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya IJA,  Halmashauri Tendaji ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti(RAAWU) tawi la Lushoto pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, hapa Chuoni wilayani Lushoto.
Amesema kuwa Chuo cha IJA kinapotoa maarifa kwa watu wa kada mbalimbali, basi kinasaidia katika masuala ya haki, akibainisha kuwa wananchi mbalimbali bado wanakabiliwa na ukosefu wa haki.
"IJA ni Chuo muhimu, nimefurahi kuona kumbe tuna Taasisi nzuri hapa," amesema Naibu Waziri na kuongeza,
"Sisi ambao tuna husika na wananchi moja kwa moja kama wabunge, madiwani na wenyeviti ni mashahidi kwamba wananchi wetu bado wana ukosefu wa haki zao hasa masuala ya kisheria, kwa hiyo nina imani ninyi mkiwapa maarifa watu wanaokuja kusoma hapa mnakuwa mnasaidia kwenye eneo la haki."
Pia Naibu Waziri huyo wa Katiba na Sheria ameongeza kuwa amejifunza masuala mengi ya Chuo cha IJA na 
kuhusu changamoto za Chuo Cha IJA, amebainisha kuwa atakwenda kuzifanyia kazi pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria na viongozi wengine.
"Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria alikuja hapa akapokea changamoto zenu, nami niwaambie tutakwenda kuzifanyia kazi na kazi yetu sisi ni kuwa kiungo ili kuona mnafanya kazi vizuri," amebainisha Mhe. Naibu Waziri.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha IJA ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F.Kihwelo amesema kuwa Chuo ni kitovu cha elimu na Utafiti kwa upande wa Mahakama na kwamba kimeendelea kuzalisha watu muhimu kwenye eneo la usimamizi wa haki.
Awali katika ziara hiyo, Mhe. Naibu Waziri huyo wa Katiba na Sheria alitembelea maeneo kadhaa ya Chuo, ikiwemo Maktaba, Hosteli ya Wanaume ya Benjamini Mkapa pamoja na viwanja vya michezo vya Chuo.
Katika hatua nyingine, Uongozi wa Chuo umempatia Mhe. Naibu Waziri zawadi za vitu mbalimbali yakiwemo machapisho ya Chuo.







 Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Pauline Gekul akisaini Kitabu cha wageni Ofisini kwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) alipofanya ziara Chuoni IJA.



Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul(katikati) akizungumza jambo wakati akiwa katika Maktaba  ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA)..

Kulia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo na kulia ni Mkutubi wa Chuo cha IJA, Bw, Jackson Chacha.



Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (kushoto) akiwa na   Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo(kulia) mara baada ya kukagua Hosteli ya wanaume ya Benjamin Mkapa alipofanya ziara hapa Chuoni IJA.



Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo(kulia) akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Pauline Gekul(hayupo pichani) aliyetembelea Chuo cha IJA hivi karibuni.


Wajumbe wa Halmashauri Tendaji ya Chama cha wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, habari na utafiti(RAAWU) Tawi la Lushoto wakimsikiliza Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul  alipofanya ziara Chuoni IJA.



Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo(kushoto) akimkabidhi machapisho ya Chuo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul alipofanya ziara hapa Chuoni IJA.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akizungumza na Wajumbe wa Menejimeti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) na Halmashauri Tendaji ya Chama cha wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, habari na utafiti(RAAWU) Tawi la Lushoto na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, alipofanya ziara hivi karibuni hapa Chuoni IJA.