Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais
wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson amezindua maadhimisho
ya wiki ya sheria leo tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
Katika uzinduzi huo Mhe.
Dkt. Tulia alikuwa mgeni rasmi wa
shughuli hiyo na amewataka washiriki wa maonesho hayo kuelimisha wananchi kwenye
mambo mbalimbali yahusuyo sheria.
Sambamba na uzinduzi wa wiki ya sheria, Mhe. Dkt. Tulia pia
amezindua rasmi Mfumo wa Udukuzi na Tafsiri (TTS) wa Mahakama ya Tanzania ambao
utatumika katika kutafsiri na kunukuu lugha zinazotumika mahakamani mbazo ni
Kiswahili na Kingereza na utakaorahisisha zaidi huduma ya upatikanaji haki kwa
wananchi.
“Naipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa ya kuleta Mfumo huu, ambao naamini
utarahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi,” amesema Mhe. Dkt. Tulia.
Aidha, Mhe. Dkt. Tulia
ametoa rai kwa wadau wote wa Mahakama kufanya uwekezaji wa miundo mbinu ya
TEHAMA ili kuendana na kasi ya Mahakama katika kuboresha utendaji kazi na kuongeza
ubora wa huduma.
‘‘Naamini
kazi kubwa sasa, hasa wadau wa Mahakama ni utengenezaji wa mfumo hasa wa
kitehama, utakaowasaidia wadau hawa kufungamanisha na kuboresha Mfumo Jumuishi
wa Haki Jinai unaosomana, ili kubadilishana taarifa kuanzia hatua ya upelelezi,
ufunguaji wa mashauri, msaada wa kisheria, uendeshaji wa mashtaka, kusikiliza
mashauri na utoaji uamuzi,” amesema Mhe. Dkt. Tulia.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, akiwa anamkaribisha mgeni rasmi amesema,
Mahakama ya Tanzania imewekeza kwenye matumizi ya TEHAMA kwa kuweka Mifumo mbalimbali ili kurahisisha huduma za utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Prof. Juma aliendelea kwa kueleza faida za mfumo huo kuwa utawaapunguzia
kazi Majaji na Mahakimu waliyokuwa
wanaifanya ya kuandika kwa mkono mienendo ya mashauri kwa mfumo huu utarahisha
na kufanya wananchi kupata haki kwa wakati.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto ni miongoni mwa Wadau mbalimbali wa Mahakama, ambapo wanashiriki katika
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza tarehe 24 Januari mpaka 30 Januari,
2024. Wadau wengine wa Mahakama wanaoshiriki katika maonesho hayo ni Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa
ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama
cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza na Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS).
Katika maadhimisho haya ya Wiki
ya Sheria na Siku ya Sheria, kauli mbiu ni “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa:
Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.
Maonesho haya
yaliyozinduliwa leo yatafanyika kwa muda wa siku nane ambapo yanatarajiwa
kukamilika tarehe 30 Januari, 2024 ambapo yatahitimishwa kwa kilele cha Siku ya
Sheria itakayofanyika tarehe 01 Februari, 2024 na mgeni rasmi wa siku hiyo
anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson akihutubia wananchi kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria uliofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson akiwa na Viongozi wa Mahakama ya Tanzania kwenye matembezi kwa ajili ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria uliofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
Viongozi wakiwa katika matembezi maalum kwa ajili ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria yaliyofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
Jaji wa Mahakama Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Chuo wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria uliofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa
Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson(katikati) ikiwa katika picha ya pamoja
na Majaji wa Mahakama ya Rufani.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson(katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa maonesho wiki ya sheria,
Baadi ya washiriki wa maonesho ya Wiki ya Sheria wakiwa wanafuatilia uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Sheria uliofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma
Aliyewahi kuwa mwanachuo IJA alipotembelea Banda la Chuo kwa ajili ya kupata taarifa mbalimbali kuhusiana na Chuo