Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma

Jaji kiongozi wa Tanzania

Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania (katikakati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa stashahada ya sheria

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Thursday, May 4, 2023

WANACHUO IJA WAFANYA ZIARA BUNGENI

Wanachuo 50 wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) leo  Mei, 4 2023 wamefanyia ziara ya kimasomo ya  siku moja  katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

Sambamba na ziara hiyo  wanachuo hawa wamepata fursa ya kutembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki  cha Morogoro walipokuwa safarini kuelekea Dodoma ambapo kwenye kituo hicho walipata fursa ya kuona shughuli mbalimbali za kimahakama zinavyoendeshwa.

Wakiongea  baada ya ziara yao Bungeni  wanachuo hao wa IJA wameupongeza Uongozi wa Chuo, watumishi wa kituo Jumuishi cha Mahakama Morogoro kwa kufanikisha ziara hiyo.

Pia wametoa shukrani nyingi kwa Mbunge wa Lushoto Mhe. Shaban Shekilindi Kwa kuwa mwenyeji wao walipotembelea bungeni kwa kusema kwamba wamepata mafanikio makubwa na wamejifunza mambo mengi kuhusu mwenendo wa Bunge pamoja ma historia ya bunge hilo.

Wanachuo hao wakiwa wameambatana na walezi wao wa Chuo Bi. Frida  Nicholaus na Bw. George  Banoba kesho  tarehe Mei, 5 2023  watapata nafasi nyingine ya kutembelea  Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha  Dodoma.



Pichani ya juu na chini ni Wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakiwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakifuatilia mjadala Bungeni walipofanya ziara Bungeni Jijini Dodoma.




Wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakitoka  nje ya Ukumbi wa Bunge baada ya kuhudhuria kikao cha Bunge walipofanya ziara Bungeni Jijini Dodoma.

Picha mbalimbali za Wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge walipofanya ziara Bungeni Jijini Dodoma.


Picha mbalimbali za Wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge walipofanya ziara Bungeni Jijini Dodoma.



 


 Wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi walipofanya ziara Bungeni Jijini Dodoma.





 

Tuesday, May 2, 2023

IJA YAADHIMISHA MEIMOSI KWA KUMUAGA MTUMISHI ANAYESTAAFU

Na; Yusuphu Sungura IJA

Chuo cha Uongozi wa Mahakama  Lushoto(IJA) leo Mei, 1 2023 kimeungana na wafanyakazi duniani kote katika kuadhimisha siku ya wafanyakazi. Sherehe hizi zilizoandaliwa na Uongozi wa Chuo zilifanyika katika ukumbi wa Ibrahim Hamis Juma uliopo chuoni Lushoto.

 Watumishi wa IJA pamoja na watumishi kutoka Mahakama ya Wilaya ya Lushoto  waliungana pamoja katika kuadhimisha sherehe hii iliyoambatana na matukio mbalimbali ambayo ni kumwaga rasmi mtumishi wa muda mrefu Dokta Joseph Ismail Hokororo ambae amestaafu kwa hiara.  Pamoja na shughuli hiyo pia sherehe hii ilijumuisha kuwakaribisha watumishi wageni waliohamia na watumishi wapya katika utumishi wa umma.

 Akitoa neno katika sherehe hizo kwa niaba ya mkuu wa chuo,  makamu mkuu wa Chuo, taaluma, utafiti na ushauri, Bwana Goodluck Chuwa amewanasihi wafanyakazi wote kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na umoja. Aidha amewataka watumishi wapya waliyojiunga na IJA kufuata miongozo na kanuni za utumishi wa umma, pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kuleta tija kwa maendeleo ya chuo.

 Akielezea Kuhusu mtumishi anaegwa, Bwn. Chuwa amemsifu kuwa alikuwa mtumishi mwema, mvumilivu na aliyeipenda kazi yake kwa dhati. Vile vile, amesema kuwa Dokta Hokororo ni mtumishi aliyesaidia kuikuza lugha ya kiswahili IJA kwa kushajiisha  maneno kama udahili, mchakato na mdau.

Nae mtumishi aliyeagwa, Dkt. Hokororo amewashukuru watumishi wote wa IJA kwa ushirikiano wao mkubwa waliyompa katika kipindi chake chote cha utumishi chuoni hapa cha takribani miaka 20. Pia amemshukuru Mkuu wa Chuo, Mhe. Dkt.  Paul F. Kihwelo ambae ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, kwa ushauri na ushirikiano aliyempatia kwa kipindi chake chote cha kufanya kazi IJA.

 "Binafsi amekuwa msaada mkubwa kwangu hasa nilipopata changamoto za kibinafsi, nimekuwa nikienda ofisini kwake kumshirikisha jambo lililonitatiza, nae bila kusita alinipa msaada mkubwa na wakati wote alinisisitiza kumtegemea Mungu kwa kila jambo," amesimulia Dkt. Hokororo.

 Shughuli hiyo imeambatana pia na tukio la kumtangaza na kumpa zawadi mfanyakazi bora wa IJA mwaka 2022/2023, ambae ni bwana Wilson Msoffe wa idara ya uhasibu.  Bwana Msoffe ametunukiwa fedha tasilimu shilingi milioni moja, Cheti na picha yake kubwa itakaa kwenye mbao ya matangazo kwa muda wa mwaka mmoja ili kutambulika kama mfanyakazi bora wa mwaka 2023. Sambamba na hilo,  chuo kimewapa zawadi wafanyakazi hodari wanne (4)  ambao ni George Masanja(Afisa Milki), Mustafa Maghembe(Dereva), Dorothea Kavuye(Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maktaba) na Cheusi Waziri(Katibu Mukhtasi). Kila mmoja amezawadiwa fedha taslimu  shilingi laki tatu.

Picha mbalimbali za Sherehe za Mei Mosi



















Monday, March 6, 2023

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA AFANYA ZIARA IJA

 

Leo tarehe 6 Machi, 2023 Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Waziri wa Katiba na Sheria amefanya ziara ya siku moja katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kutembelea maeneo mbalimbali na kuona shughuli zinazofanyika chuoni na alipata wasaa wa kuongea na Menejimenti ya Chuo na Watumishi katika ukumbi wa mafunzo wa Ibrahim Hamis Juma.   Katika ziara hjyo Mhe. Dkt. Ndumbaro ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Khatibu Kazungu

Akizungumza na Menejimenti na Watumishi Mhe. Dkt. Ndumbaro ametoa salamu za pongezi kwa Chuo kwa kufanya majukumu yake ya msingi kama sheria ya uanzishwaji wake ilivyotaka.  Kwani kwa sasa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ndicho Chuo pekee kilichobaki kwenye misingi yake hapa Tanzania.

Aliendelea kwa kusema kwamba, uimara na ubora wa Mhimili wa Mahakama umetokana na ubora Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kutoa mafunzo ya kujengea uwezo watumishi wa Kada mbalimbali wa Mhimili wa Mahakama na wadau wengine wa Sheria nchini, hivyo amekitaka Chuo kupanua wigo nje ya mipaka ya Tanzania ili kujipatia sifa chenyewe, Mhimili wa Mahakama na Tanzania kwa ujumla.

Mhe. Dkt. Ndumbaro aliendelea kwa kutoa wito kwa watumishi kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu haki na misingi ya mtumishi wa umma katika utendaji wa kazi zao za kila siku. Mhe. Dkt. Ndumbaro alisema “Utumishi wa Umma unaongozwa na Katiba, Miongozo  na mila na desturi” alisema Mhe. Dkt. Ndumbao.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Dkt. Gerald A. Ndika katika salamu zake amemshukuru Mhe. Dkt. Ndumbaro na Dkt. Kazungu kwa kufanya ziara hiyo ya kutembelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.  Mhe. Dkt. Ndika aliendelea kwa kusema kwamba matarajio ya Mhimili wa Mahakama kwa Chuo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa Chuo kuwa kitovu cha mafunzo ya watumishi wa mahakama na Chuo kimekuwa kikitoa machapisho mbalimbali yanayosaidia katika utendaji kazi wa kila siku wa watumishi wa mahakama hususani Majaji na Mahakimu.  

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo alisema Chuo kwa sasa kinaendesha mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo watumishi wa mahakama ili kuendana kasi ya Mhimili wa Mahakama. Na aliendelea kwa kusema Chuo kimefanya mafunzo mengi ya aina mbalimbali kwa njia ya mtandao, kwakufanya mafunzo kwa njia imekuwa ikitoa mafunzo idadi kubwa ya watumishi wa  mahakama  na kwa wakati hivyo kupelekea Mahakama  kupunguza mzigo mkubwa bajeti ya mafunzo kwa watumishi.

Mhe. Dkt. Kihwelo aliendelea kwa kusema Chuo kimekuwa kikifanya vizuri katika utoaji wa mafunzo toka kilipoanzishwa na kupelekea wahitimu wengi kupata teuzi mbalimbali na kuajiriwa katika taasisi mbalimbali za utoaji haki na Mhimili wa Mahakama.

 

Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Waziri wa Katiba na Sheria akihutubia Watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto alipofanya ziara ya Chuoni
 


Mkuu wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akitoa historia fupi ya Chuo 


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Khatibu Kazungu akitoa salamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria alipokuwa ameambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt Damas Ndumbaro.

Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Waziri wa Katiba na Sheria akipanda mti kwenye bustani ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto alipofanya ziara ya Chuoni.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Dkt. Gerald A. Ndika akimkabidhi zawadi ya machapisho yanayozalishwa na Chuo Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu.

Pichani ni baadhi ya Watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro alipofanya ziara chuoni.


Picha ya pamoja ya meza kuu na wajumbe wa Menejimenti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto

Picha ya pamoja ya meza kuu na wajumbe wa Halmashauri ya RAAWU Tawi la IJA


Picha ya pamoja ya meza kuu na watumishi waliofanya kazi Chuoni toka Chuo kilipoanzishwa


Picha ya juu na chini meza kuu  na watumishi waliohudhuria kikao wakati wa ziara ya Waziri


























Thursday, February 16, 2023

IJA YAENDESHA MAFUNZO YA WASHAURI WALEZI KWA MAJAJI 12 WA MAHAKAMA KUU

Na Innocent Kansha - Mahakama

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo jana tarehe 30 Januari, 2023 alifungua mafunzo kwa Majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliteuliwa kushiriki kwenye programu ya majaribio ya namna bora ya kujengeana uwezo wa kiushauri kwa Majaji na Mahakimu hasa wakati wa kuamua mashauri bila kuingilia uhuru wa Mahakama “Pilot Mentorship Programme”.

Akizungumza katika hafla fupi ya ufunguzi wa mafunzo hayo uliyofanyika katika ukumbi wa mikutano ulipo jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Kihwelo alisema mafunzo hayo yanatokana na matunda ya ushirikiano baina ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Mzunguko ya Uingereza na Wales kubuni mpango wa majaribio wa namna ya kujengeana uwezo kishauri ili kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wakati wa kutoa maamuzi ya mashauri kwa Maafisa wa Mahakama.

“Kupitia mafunzo haya ya na namna bora ya kujengeana uwezo wa kiushauri kwa Majaji na Mahakimu tutakubaliana namna ya uandaaji kitabu cha Mwongozo utakao tumika katika shughuli za namna ya kuanzisha mahusiano kushauriana kwa njia rasmi na zisizo rasmi ‘Mentor & Mentee Relationship’ wakati wa kuamua mashauri na migogoro inapowasilishwa Mahakamani” alisema Jaji Kihwelo

Mhe. Dkt. Kihwelo alisema program hiyo itategemea zaidi ushirikishwaji wa uzoefu na weledi mkubwa walionao Majaji hao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku hasa katika eneo la kutatua migogoro ama mashauri yanayolenga kupambana na rushwa kubwa zenye thamani ya kuanzia milioni 200 na kuendelea kwa ustawi wa Taifa.

“Program hii msingi wake utazingatia uhuru wa Mahakama kwa asilimia mia moja katika kufanya maamuzi ‘Mentorship programme’ haitamaanisha mshauriwa anapaswa kufuata yale yote aliyoelekezwa na mshauri katika kufikia maamuzi kama msingi wa maamuzi yake juu ya jambo fulani lililopo mbele yake. Programu hii inalenga kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu wa namna bora ya kuongeza ufanisi na weledi kupitia uzoefu walionao wakati wa kutoa maamuzi ya kimahakama”, alisisitiza Jaji Dkt. Kihwelo.

Mhe. Dkt. Kihwelo alisema kupitia Programu hiyo itakuwa ya msaada mkubwa kwa Mahakama ya Tanzania na kutoa matokeo chanya kwa maendeleo ya kazi kwa maafisa wa Mahakama. Kupitia forumu hiyo akawashauri Majaji  kuchangia mawazo yao kwa kutumia uzoefu mkubwa walionao ili kufanikisha mwongozo bora wa programu ya ushauri.

Mafunzo kama hayo shabaha yake kubwa ni kutoa msaada, kwatia moyo na kuwapatia mwongozo Maafisa wa Mahakama wale ambao hawakupata bahati ya kushiriki moja kwa moja programu ya mafunzo ya ‘Mentorship programme’. Majaji waliohudhuria mafunzo watatumika kutoa elimu hiyo na kuwajengea uwezo Maafisa wengine katika maeneo yao ya kiutawala

Programu itaangazia maeneo ambayo yanaathirika na kugubikwa kwa kiwango kikubwa na vitendo vya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kama vile Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha na Mbeya. Takwimu za mwezi mei, 2022 zinaonyesha kuwa mashauri 147 ya makosa hayo yanayoendelea katika Mahakama za Hakimu Mkazi katika miji tajwa, makosa 21 ni ya mtandao mkubwa wa makosa ya rushwa na yamebainishwa na mtandao wa Programu Endelevu wa Mapambano ya kuzuia Vitendo vya Rushwa Tanzania (BSAAT).

Jaji Dkt. Kihwelo alihitimisha kwa kuwashukuru wabia waliowezesha kufanikishwa kwa programu hiyo ambao ni Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania na Ofisi ya Maendeleo ya Jumuiya ya Madola, kupitia Programu yake endelevu ya kupambana na Vitendo vya Rushwa Tanzania “The British High Commission (Foreign, Commonwealth & Development Office – FCDO through the Building Sustainable Anti – Corruption Action in Tanzania (BSAAT)”.  








 


Sunday, January 22, 2023

IJA YASHIRIKI MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amezindua maadhimisho ya wiki ya sheria leo tarehe tarehe 22 Januari, 2023 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

Katika uzinduzi huo ambapo Mhe. Dkt. Mpango  alikuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo amewataka watoa haki na washiriki wa maonesho hayo kuelimisha wananchi kuhusu njia bora za utatuzi wa migogoro  hususani njia ya usuluhishi ambayo ina faida nyingi ikiwemo kuokoa muda, kupunguza mlundikano wa mashauri na kukuza uchumi wa Taifa.

Mhe. Dkt. Mpango aliendelea kwa kuwaomba Viongozi wa dini mbalmbali kuwakumbusha waumini wanawaongoza juu ya umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi pia aliwahamasisha wananchi wote kutembelea  Maonesho ya wiki ya sheria yanayoendelea nchi nzima ili kupata elimu inayotolewa na wadau hao wa utoaji haki.

Aidha, Mhe. Dkt. Mpango amewataka viongozi wa Mahakama kuzifanyia kazi changamoto kadhaa zilizopo katika Mahakama kwa baadhi ya watumishi ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili pamoja na kuwawajibisha.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakama ya Tanzania na Wadau wa utoaji haki kutumia maadhimisho ya wiki ya sheria kwa madhumuni ya kuwaelimisha wananchi ili kufahamu taratibu mbalimbali za kupata haki na kuwaelimisha juu ya haki na wajibu wao katika kupata haki.

Mhe. Prof. Juma pia alizungumzia suala la Usuluhishi kwa kusema wananchi wana wajibu wa kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi na  akatoa wito kwa wananchi kutembelea maonesho ya wiki ya sheria yanayotolewa maenneo mbalimbali nchi nzima. 

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ni miongoni mwa Wadau mbalimbali wa Mahakama, ambapo watashiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na wadau wengine wakiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Katika maadhimisho haya ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria, kauli mbiu itakuwa Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.

Maonesho haya yaliyozinduliwa leo yatafanyika kwa muda wa siku nane ambapo yanatarajiwa kukamilika tarehe 29 Januari, 2023 ambapo yatahitimishwa kwa kilele cha Siku ya Sheria itakayofanyika tarehe 01 Februari, 2023 huku mgeni rasmi wa siku hiyo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akihutubia kwenye Maadhimisho ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria yaliyofanyika leo tarehe 22 Januari, 2023 katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na viongozi mbalimbali baada ya kuwasili katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma kwa ajili ya  matembezi kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria.

Wahadhili kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama wakiwa wanajiandaa kwa ajili ya matembezi ya kilometa 5 kutoka Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kumalizikia katika Viwanja vya Nyerere Squarewakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Sheria.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa pamoja na viongozi wa Mahakama ya Tanzania  katika matembezi  kwenye Maadhimisho ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria yaliyofanyika leo tarehe 22 Januari, 2023 katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.








Picha za juu ni Wahadhili kutoka IJA wakitoa elimu kwa wananchi mbalimbali waliopita kwenye banda kutaka kujua shughuli zinazofanywa na  IJA