Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma

Jaji kiongozi wa Tanzania

Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania (katikakati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa stashahada ya sheria

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Friday, June 24, 2022

IJA YASAINI MKATABA WA USHIRIKIANO NA TAASISI YA PAMS FOUNDATION

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kimeingia makubaliano ya Ushirikiano na Taasisi ya PAMS Foundation wenye lengo la kuwajengea uwezo maafisa wa Mahakama wa namna bora ya kuendesha mashauri yahusuyo makosa dhidi ya wanyamapori pamoja na makosa mengine ya uhalifu wa kimataifa (international serious crimes).

Makubaliano hayo yanalenga pia kuijengea uwezo IJA katika eneo la utafiti kwenye maeneo ya makosa makubwa ya kimataifa ikiwemo makosa ya ujangili wa wanyama pori na misitu.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo tarehe 23/06/2022 jijini Dar es Salaam kati ya Jaji Dkt. Paul Faustin Kihwelo, Jaji wa Rufani na Mkuu wa Chuo pamoja na Bi Krissie Clark, Mkurugenzi Mtendaji na miongoni mwa waasisi wa PAMS Foundation yenye Makao yake makuu jijini Arusha.

PAMS Foundation ni shirika lisilo la kiserikali  lenye dhamira ya kuwawezesha wale wote wanaolinda wanyamapori na misitu.




Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PAMS Foundation, Bi. Krissie   Clark (kushoto), wakibadilishana mkataba huo


Mkurugenzi wa Operationi na Mafunzo, Bw.Samson Kassala( wa kwanza kushoto)na na  Mkurugenzi wa Intelijensia na Uchambuzi,(wa pili kushoto) Bw.Elisifa  Ngowi wakisaini mkataba huo. 


Mkurugenzi wa Operationi na Mafunzo, Bw.Samson Kassala( wa kwanza kushoto)na na  Mkurugenzi wa Intelijensia na Uchambuzi,(wa pili kushoto) Bw.Elisifa  Ngowi wakifuatilia utiaji saini huo. 




Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto , Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (kulia) akimpatia machapisho mbalimbali ya Chuo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PAMS Foundation, Bi. Krissie   Clark (kushoto).


Wednesday, June 15, 2022

IJA YAENDESHA MAFUNZO YA NAMNA BORA YA UTOAJI WA ADHABU NA UTEKEZAJI WA AMRI ZA MAHAKAMA

 Na Ibrahim Mdachi – IJA Lushoto

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania chini ya ufadhili wa Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Tanzania zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (BSAAT) kimeendesha mafunzo ya siku tatu kwa Mahakimu 43 kuhusu namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama. Mafunzo hayo yalianza tarehe 13 Juni, na kuhitimishwa tarehe 15 Juni, 2022 Chuoni hapo.

Akifungua mafunzo hayo rasmi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma  aliwataka Mahakimu kuzingatia mwongozo wa adhabu na kujiepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kujenga jamii inayojali haki kwa kila mmoja na kuwafanya wananchi waendelee kuwa na imani na Mahakama.

Alitanabaisha pia kuwa kimsingi mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na uelewa wa mwongozo wa utoaji adhabu ambao ni miongoni mwa nyenzo za maafisa wa Mahakama katika mchakato wa utoaji wa adhabu kuwa halali na usiotiliwa shaka na wadaawa wanaohusika katika mashauri mahakamani wakiwemo washtakiwa, waathiriwa, wapelelezi, mawakili wa utetezi, waendesha mashtaka na umma kwa ujumla.

Mhe. Chuma alisema kuwa ni matarajio ya Mahakama ya Tanzania kupitia mafunzo hayo washiriki watapata uelewa wa mwongozo wa utoaji adhabu, hivyo kutumika ipasavyo katika mashauri hasa ya rushwa, uzoefu utakaopatikana utafikishwa kwa maafisa wengine wa Mahakama ambao hawakufanikiwa kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Mratibu wa Programu ya BSAAT ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha  akitoa maelezo mafupi kuhusu mradi huo alisema kuwa, program hiyo inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kwa kushirikana na Umoja Ulaya (EU) na kuratibiwa na Ofisi ya Rais, Ikulu ilianza kutekelezwa mwaka 2018/2019 ikijumuisha taasisi tisa nufaika ambazo ni wadau katika mnyororo wa haki jinai ikiwemo Mahakama kama mdau muhimu katika utiaji wa haki.

Bw. Magoha aliongeza kuwa program hiyo imelenga kupunguza vitendo vya rushwa kama kikwazo cha kupunguza kiwango cha umasikini kwa Watanzania, kuboresha uadilifu, kuboresha uwezo na uratibu wa mfumo wa haki jinai katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na kuongeza imani kwa umma juu ya utendaji kazi wa Mahakama.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo Bw. Goodluck Chuwa alisema kuwa, ni takribana miaka mitano tangu chuo kimeamua kujikita katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuundwa kwake kitahakikisha kuwa kinaendelea kuyaratibu mafunzo mbalimbali kwa weledi mkubwa kwa lengo la kuleta tija kwa Mahakama na wadau wengine wa sheria nchini.

Mafunzo haya  ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021-2025, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja  na Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wa miaka mitano wa mwaka 2018-2023.

                                                           

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma  akifungua mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama kwa Mahakimu 43 kutoka Mikoa Mbalimbali ya Tanzania yanayofanyika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.


 Hakimu Mkazi Mkuu  wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Richard Kabate akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya  namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama.



 Pichani ni baadhi ya washiriki wa mafunzo katika picha ya pamoja na Mhe. Wilbert Chuma, (Mgeni Rasmi) wakiwa ameketi na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya Lushoto, Mhe. Rose Ngoka na Kaimu Mkuu wa Chuo Bw. Goodluck Chuwa (upande wake wa kulia)  na Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha Na Utawala, Prof. Fatihiya Massawe na Naibu Mkurugenzi wa Utawala, Mahakama ya Tanzania na Mratibu wa Mradi wa BSAAT nchini Bwn. Stephen Magoha (Upande wa Kushoto)

 

Picha ya juu na chini ni picha ya washiriki wa Mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama wakiendelea na mijadala mbalimbali katika mafunzo hayo.

 



 

 


Wednesday, May 25, 2022

JAJI MKUU WA UGANDA AFANYA ZIARA IJA

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo leo tarehe 25 Mei, 2022 amefanya ziara ya kutembelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na kujionea shughuli mbalimbali zinafanywa na Chuo.

 

Katika ziara yake, Mhe. Owiny-Dollo ameambatana na Maafisa 12 kutoka nchini Uganda ambao  miongoni mwa aliombatana nao ni Jaji Kiongozi wa Uganda Mhe. Dkt. Flavian Zeija, Msajili ya Mahakama ya Uganda, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa JTI Uganda, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya JTI Uganda, Msajili waTaasisi ya JTI Uganda na viongozi wa International Development Law Organization Uganda(IDLO).

 

Akiongea akiwa kwenye ziara hiyo, Mhe. Owiny-Dollo alisema kuwa  lengo la ziara yao ni kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kuwandaa Maafisa Mahakama ambao wamepangiwa majukumu mapya na kujifunza jinsi ya kuijengea uwezo Taasisi ya Mafunzo ya Kimahakama ya nchini Uganda (JTI) pia  kujenga ushirikiano katika masuala mbalimbali yanayohusu vyuo na jinsi ya  kuiwezesha Mahakama ya Uganda kufanikisha katika maboresho yake kiutendaji.

Mhe. Owiny-Dollo aliendelea kwa kusema kuwa mafunzo ya kuwandaa Maafisa wa Mahakama wanaopewa majukumu mapya ni muhimu katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo huduma bora ya utaoji haki kwa wananchi.

Alisema wanataka kupata uzoefu ambao utawasaidia yeye na ujumbe kutoka Chuo cha Mahakama cha Uganda kuwawezesha watumishi wanaopewa majukumu mapya kupata mafunzo ambayo yatasaidia katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Maafisa wa Mahakama walioandaliwa kwa kupewa mafunzo mazuri wataelewa vema majukumu yao na mambo ambayo anatakiwa kufanya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kupata haki wanapokuwa na mashauri” alisema

Alipokuwa akiwakaribisha wageni hao, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika alionyesha furaha yake kwa kuushuru ugeni huo kwa kusema kwamba ujio wao ni fursa muhimu ambapo wataitumia kwa kujifunza mambo mbalimbali na kubadilishana uzoefu jinsi vyuo vya Mahakama vinavyofanya kazi.

Naye Mkuu wa Chuo na  Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alipokuwa anaelezea historia ya Chuo kilianzishwa kwa Sheria ya Bunge, Sheria Namba 3 ya 1998. Kilianza kazi yake tarehe 23 Oktoba, 2000 na kilikuwa kinatoa Cheti na Diploma ya Kozi za Sheria. Uzinduzi rasmi ulifanywa na Rais Benjamin Mkapa tarehe 3 Agosti 2001.  Pamoja na historia hiyo Mkuu wa Chuo alieleza lengo la madhumuni ya kuanzishwa kwa Chuo ilikuwa ni kujengea uwezo watumishi wa Mahakama.

Ziara hiyo ni sehemu ya ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Uganda na ujirani mwema kati ya nchi hizi mbili. Sambamba na kutembelea maeneo mbalimbali ya Chuo, Wageni hawa wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vilivyopo katika Wilaya ya Lushoto.


Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo alipokuwa anatoa 
salamu kwa viongozi wa IJA

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika 
akitoa neno la ukaribisho kwa Jaji Mkuu wa Uganda na Viongozi wengine wa Mahakama ya Uganda.



Mkuu wa Chuo na  Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alipokuwa akiwaeleza wageni juu ya historia ya Chuo na shughuli Chuo kinazozifanya

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya JTI Uganda, Mhe. Damilie Lwanga akieleza kwa ufupi shughuli zinazoendeshwa na chuo hicho




Katika picha ni baadhi ya viongozi waliombatana katika Ziara ya Jaji Mkuu wa Uganda wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Uongozi wa IJA kuhusu utendaji kazi wa Chuo
Menejimenti ya IJA wakifuatialia maelezo yaliyokuwa yanawasilishwa na upande wa wageni kutoka Mahakama ya Uganda

Picha ya Mahakimu kutoka Wilaya ya Lushoto wakifuatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa inawasilishwa 
Picha ya pamoja ya Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owinyi- Dollo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Uganda.


Picha ya pamoja ya Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owinyi- Dollo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimienti ya IJA.

Monday, May 23, 2022

IJA YAENDESHA MAFUNZO KWA MAAFISA WA BODI YA SUKARI TANZANIA

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kimeandaa na kuendesha mafunzo kwa Maafisa 27 kutoka Bodi ya Sukari Tanzania. Washiriki wa mafunzo hayo ni Maafisa wa Bodi ya Sukari Tanzania wa ngazi mbalimbali.  Mafunzo hayo yanafanyika Chuoni Lushoto kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 23 Mei mpaka 27 Mei 2022. 

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, alielezea lengo la mafunzo hayo  kuwa ni kuwajengea uwezo Maafisa hao kwenye ufafanuzi kuhusu Sheria ya Tasnia ya Sukari, 2002 na Kanuni zake katika kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi. 

Mhe. Dkt. Kihwelo alisema kuwa Mahakama ni chombo cha mwisho katika utoaji wa haki, kwani kuna wadau wengine wa sheria ambao wanafanya kazi hizo za kutoa haki kama Maafisa wa Bodi ya Sukari ambao wajibu wao ni kutoa leseni, kusimamia na kudhibiti soko la sukari nchini. Aliwataka kutumia kile watakachojifunza katika kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi wao ili kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Linus Bwegoge, alieleza kwamba Bodi ya Sukari Tanzania ina wajibu wa kutoa huduma za udhibiti na kuratibu maendeleo ya Tasnia ya Sukari Tanzania. Aliongeza kuwa ili kutekeleza kwa ufanisi zaidi sheria ya tasnia ya sukari na kanuni zake menejimenti iliona ni vema kuwaleta maafisa wake kwa ajili ya mafunzo hayo. 

Chuo cha IJA kina jukumu la kuwajengea uwezo watumishi wote wa mahakama na mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma za utoaji haki nchini kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.  Sambamba na mafunzo hayo Chuo kimebobea katika kufanya mafunzo ya Stashahada na Astashahada ya sheria, kufanya tafIti mbalimbali na  kutoa ushauri wa kitalaamu.


Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, akifungua mafunzo kwa Maafisa wa Bodi ya Sukari Tanzania 

Naibu Mkuu  Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Fatihiya Massawe akitoa neno la ukaribisha kwa  Maafisa wa Bodi ya Sukari Tanzania kwenye mafunzo ya ufafanuzi kuhusu Sheria ya Tasnia ya Sukari, 2002 na Kanuni zake 

Meza Kuu katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo  mafunzo ya ufafanuzi kuhusu Sheria ya Tasnia ya Sukari, 2002 na Kanuni zake 


                         Bi. Zakia Stephano Lwamala,Wakili wa Serikali, Wizara ya Kilimo na mwezeshaji wa  mafunzo ya ufafanuzi kuhusu Sheria ya Tasnia ya Sukari, 2002 na Kanuni zake  akiwasilisha mada kwa washiriki     




Thursday, May 5, 2022

CHUO CHA UONGOZI MAHAKAMA LUSHOTO CHAZINDUA BARAZA JIPYA LA WAFANYAKAZI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Mary Makondo ametoa pongezi kwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuwa miongoni mwa taasisi chache zinazoongoza nchini kuendesha mafunzo kwa njia ya Mtandao. Ametoa kauli hiyo leo tarehe 5 Mei, 2022 Jijini Dar es Salaam katika Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la Nne la Chuo ambapo amesema Chuo kimekuwa kikifanya vizuri kwenye eneo la mafunzo kwa njia ya mtandao sio tu nchini bali pia katika ukanda wa Afrika na nje ya mipaka ya Afrika. 

Mhe. Makondo alieleza kwamba katika kipindi hiki cha Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambapo matumizi ya TEHAMA na Akili Bandia yamezidi kushika kasi, hali hiyo imetokana na ukweli kuwa Mahakama ya Tanzania ni Mhimili unaofanya vizuri kwenye matumizi ya TEHAMA katika utendaji kazi wa kila siku ikiwemo uendeshaji wa mashauri. 

 Aliendelea kusema kuwa Chuo kama wakala wa mafunzo kwa kutumia TEHAMA kupitia mfumo wa virtualcourt umeweza kuendesha mafunzo kwa zaidi ya watumishi 1500 wa mahakama ya Tanzania mpaka sasa na idadi hiyo inaendelea kuongezeka. Amesema njia hiyo imeweza kukisaidia Chuo kuwafikia watumishi wa Mahakama popote walipo bila usumbufu wa kusafiri ambapo njia hiyo imeweza kupunguza gharama za kuwalipa watumishi kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo mbalimbali.

Mhe.Makondo ameonyesha  kufarijika kwa jitihada zinazofanywa na chuo cha uongozi wa mahakama Lushoto kwa kuendesha  mafunzo mbalimbali kwa kutumia mifumo ya Tehama iliyotengenezwa na wataalamu wa ndani .

"Nimefarijika sana kuona chuo kimetumia mfumo uliojengwa na watalaamu wetu badala ya kutumia mifumo kama Microft teams , zoom hii inatuhakikishia usalama wa mifumo pamoja na kujenga uwezo wa ndani ,nitoe rai kwa chuo kuharakisha kuanzisha mafunzo ya muda mfupi ya komputa kwa wanasheria" alisema Makondo.

 Aidha Mhe.Makondo amewataka wajumbe walioteuliwa katika Baraza la wafanya kazi kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri kwa wafanyakazi wanaowawakilishi na siyo kuwa mizigo kwa uongozi na wafanyakazi katika kutatua kero zao.

 Aidha Mhe. Makondo ameupongeza uongozi wa Chuo kwa jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kununua viwanja jijini Mwanza na Mkoani Simiyu na kusema kufanya hivyo ni hatua kubwa kwa Chuo. "Wizara inaamini kwamba uendelezaji wa viwanja hivyo utafanyika kwa haraka ili kufikisha huduma karibu na wananchi kama ilivyokusudiwa,"alisema.

Mhe. Makondo ameahidi kuwa Wizara anayoiongoza iko tayari kutoa ushirikiano unaostahili kwa Chuo wakati wowote watakapouhitaji.

Mhe. Makondo àlitumia hafla hiyo kutoa wito kwa waajiri wote wanaoajiri wanasheria katika utumishi wa umma kuwapeleka watumishi hao kupata mafunzo katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa mujibu wa matakwa ya Waraka wa Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Waraka Namba 5 wa mwaka 2012. 

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi  Mhe.Dkt. Paul Kihwelo amesema kuwa kwa kanuni ya 108 ya sheria za utumishi wa umma 2003 kanuni zinaelekeza kuwepo kwa chombo ambacho kitahakikisha kuwepo kwa mahusiano mazuri kazini pamoja na kuhakisha masilahi ya watumishi yanazingatiwa kwa mjibu wa sheria.

Mhe. Dkt. Kihwelo aliendelea kusema kuwa wajibu wa Chuo ni kuwajengea uwezo watumishi wa mahakama kwa kada mbalimbali Tanzania ili kuboresha utendaji wa kazi kwa maafisa. 

Hafla hiyo ya uzinduzi ilikamilika kwa wajumbe kupewa mafunzo ya siku moja ya Haki na Wajibu wa Mtumishi wa Umma pamoja na Maadili ya Utumishi wa Umma mafunzo ambayo yameendeshwa na wawezeshaji wabobezi kutoka Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi ya Umma.

Lengo la mafunzo hayo ni kuleta tija kwa watumishi, taasisi na taifa ili kuweza kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza katika utumishi wa mma kwa kuwa Baraza la wafanyakazi ni kioo na mwanga wa taasisi. 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Mary Makondo akiongea na Wajumbe wa Baraza Jipya la Wafanyakazi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama wakati wa uzinduzi wa Baraza hilo.





Picha mbalimbali za  Wajumbe wa Baraza Jipya la Wafanyakazi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama wakiwa wanafuatilia hotuba wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Mary Makondo akipokea zawadi ya Tisheti kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi  Mhe. Dkt. Paul Kihwelo katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la Nne la Chuo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Mary Makondo akipokea zawadi kutoka kwa Mhe. Dr. Benhajj S. Masoud, Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Sheria kwa Vitendo katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la Nne la Chuo


Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi  Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akipokea zawadi kutoka kwa Mhe. Dr. Benhajj S. Masoud, Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Sheria kwa Vitendo  katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la Nne la Chuo





Monday, March 21, 2022

WANAWAKE IJA WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE KWA KUTEMBELEA WAFUNGWA

Watumishi wanawake wa Chuo cha uongozi wa Mahakama Lushoto katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani kama ilivyo ada, mapema leo machi 8, 2022 wametembelea wafungwa wa Gereza la Wilaya ya Lushoto na kutoa msaada wa mahitaji ya kibinadamu wa vifaa mbalimbali vikiwemo taulo za usafi kwa Wanawake, Sabuni za kufulia na kuogea, dawa za meno na miswaki, mafuta ya kupaka na dawa za mbu.

 Akikabidhi msaada huo, mwenyekiti wa watumishi wanawake wa chuo alisema kuwa, lengo la kwenda gerezani hapo ni kuwafariji na kuwatia moyo ili wasikate tamaa kwani hakuna binaadamu aliye mkamilifu hivyo na kuongeza kuwa, pamoja na kuwa wako katika kutumikia adhabu zao ni vyema kuwakumbuka na kuwakumbusha kuwa wao ni sehemu ya jamii na inawathamini kama walivyo binaadamu wengine.


Baada ya zoezi la kutembelea wafungwa, wanawake wa IJA walipata nafasi ya kukaa pamoja na Uongozi wa Chuo kwenye tafrija fupi iliyoandaliwa na Chuo kwenye hotel ya Mullers Lodge iliyoko Wilayani Lushoto.  Akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Chuo kwenye ufunguzi wa tafrija hiyo, Mhadhiri Dkt. Ismail Hokororo aliwapongeza wanawake hao kwa kujitokeza na kuenzi maadhimisho ya siku ya Wanawake na kusema kuwa Chuo kinatambua na kuthamini  mchango wa Mwanamke katika jamii na  kipo  tayari kuwasikiliza na kutoa ushirikiano unaostahili pale utakapohitajika  na kuwahakikishia mazingira mazuri ya kufanya kazi yanayozingatia usawa kwa maendeleo ya mwanamke.


Dkt. Hokororo aliendelea kusema kuwa Menejimenti ya Chuo inaunga mkono jitihada zote zinazoibuliwa na wanawake zinazolenga kujenga umoja, uzalendo, mshikamano kwa ustawi wa chuo na Taifa kwa ujumla.

“Nyote ni mashahidi wa jitihada zinazoendelea katika kuboresha uwiano wa kiutumishi kwa wanawake na wanaume chuoni, hasa katika maeneo yale yaliyo chini ya mamlaka ya Menejimenti ya Chuo” alisema Dkt. Hokororo.


Dkt. Hokororo aliwatia moyo wanawake hao kuendelea kushirikiana na kubadilisha uzoefu huku wakiandaa mipango endelevu kwa mustakabali wa Maendeleo ya Wanawake na jamii kwa ujumla.

Katika kuadhimisha siku hiyo pia wanawake wa IJA walipitishwa kwenye mada mbili ambazo ziliandaliwa na Chuo kwa ajili ya kuwapa uelewa zaidi juu ya masuala ya siku ya wanawake ambazo zilikuwa ni mada ya Nafasi ya Mwanamme katika kumkomboa mwanamke na mada ya pili iliyohusu Umuhimu wa Wanawake Kujiunga Pamoja.

 

Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani hufanyika Machi 8 kila mwaka, kiwilaya maadhismisho haya yamefanyika katika kijiji cha Gare ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria na kutoa salamau zao kuhusu masuala mbalimbali ya haki na usawa kwa jinsia na pia kusisitiza juu ya umuhimu wa kuhesabiwa sambamba na dhima ya mwaka huu isemayoKizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu: Tujitokeze kuhesabiwa’’. Dhima hii inaenda sambamba na mpango wa serikali wa kuendesha zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi septemba, 2022 nchini.


Dkt. Joseph Hokororo Ismail, Mhadhiri wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akitoa Salamu za Siku ya wanawake kwa niaba ya Mkuu wa Chuo, pembeni kwake ni Mwenyekiti wa watumshi wanawake wa Chuo Bi. Mariamu George.


Picha ya pamoja ya baadhi ya watumishi wanawake wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto waliohudhuria kwenye tafrija fupi iliyoandaliwa na Uongozi wa Chuo kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya wanawake ulimwenguni.


PICHA ZA CHINI NI PICHA MBALIMBALI ZA MATUKIO YA SIKU YA WANAWAKE 









Wednesday, March 16, 2022

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA ZIARANI IJA

Na: Rosena Suka IJA Lushoto

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wamefanya  ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la ghorofa nne la wavulana lenye thamani ya shilingi za kitanzania billioni 2.64  lenye uwezo wa kulaza wanachuo 320. Mradi huu unasimamiwa na Mahakama ya Tanzania katika mpango wa Maboresho ya Mahakama.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa jengo hilo la bweni la wavulana Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa ufafanuzi wa ujenzi wa jengo hilo kuwa umefanyika katika awamu tatu tofauti ambazo zilisimamiwa na wakandarasi watu watatu kwa nyakati tofauti toka kuanza kwa mradi wa ujenzi huo mwaka 2011.  

Prof. Elisante alitoa maelezo hayo kwa kusema kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo ilikuwa chini ya mkandarasi Beijini Construction Engineering Group ambaye alijenga kuanzia msingi hadi boma. Hatua ya pili ilikuwa ni uwekaji wa mifumo mbalimbli katika jengo hilo chini ya usimamizi wa Mkandarasi Froton Afrika Limited na Mkandarasi aliyepo kwa sasa ni  MS-Works Construction Limited ambaye anaendelea na umaliziaji wa jengo hilo  ambalo litakapokamilika litakuwa na       miundombinu ambayo itawezesha wanafunzi kutoka katika makundi maalum kulitumia.

Pamoja na mengine Prof. Elisante alimalizia kwa kusema kuwa, jengo hilo litakabidhiwa ifikapo Mei, 2022 na linatarajiwa kutumiwa na wanachuo watakaosajiliwa katika mwaka wa masomo 2022/2023 ambapo litapunguza idadi kubwa ya wanachuo wakiume wanaoishi nje ya mazingira ya Chuo.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Tabora Mjini Mhe. Emmanuel Mwakasaka ameipongeza Serikali kwa hatua iliyofikia ya ukamilishwaji wa ujenzi wa Jengo la Bweni la Wavulana la Chuo cha Uongozi wa Mahakama. Hatua ya ujenzi wa bweni hili litakuwa ni mkombozi kwa Chuo kwani litawezesha wanachuo kuweza kuishi ndani ya chuo badala ya kuchanganyika na wenyeji.

“Miradi ya ujenzi wa majengo haya imeenda kwa haraka sana na tumeridhishwa sana na kazi iliyofanyika, pongezi kwa watendaji wote wa Mahakama”, alisema Mhe. Mwakasaka.

Naye, Naibu Waziri, Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Geogrey Pinda (MB) alishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa kutembelea mradi huo na kuahidi kuwa hoja zote zilizotolewa na wajumbe zimepokelewa na zitafanyiwa kazi. Mhe. Pinda pia alitoa mapendekezo kwa Chuo kutumia nafasi waliyonayo kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa mahakama ili kusaidia mabadiliko ya mahakama kwenda sambamba na wataalamu.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri Bw. Goodluck Chuwa ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Chuo kwa kukiwezesha mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa kada mbalimbali wa Mahakama pamoja na wadau wa sheria nchini.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imefanya  ziara ya siku moja ambapo imekagua mradi wa ujenzi wa jengo la bweni la wavulana la Chuo cha Uongozi Mahakama Lushoto  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo ikiwemo kufanya ukaguzi wa miradi ya ujenzi inayosimamiwa na Mahakama ya Tanzania.




Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa maelezo mafupi juu ya ujenzi wa bweni la wavulana kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na viongozi wengi wa Wilaya waliohudhuria katika tukio hilo.



Meza Kuu katika picha ya pamoja naWajumbe waKamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria
Picha ya juu na chini ni mwonekano wa nje na wa ndani wa bweni la wavulana ambalo lipo katika hatua ya ujenzi.

(Picha na Ibrahim Mdachi - IJA Lushoto)