Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma

Jaji kiongozi wa Tanzania

Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania (katikakati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa stashahada ya sheria

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Mahafali ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyia 18 Desemba, 2020

Tuesday, August 9, 2022

IJA YATOA MAFUNZO KWA MAKATIBU MUHTASI WA MAHAKAMA YA TANZANIA

Na Rosena Suka, Lushoto

Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo,  Jaji wa Mahakama ya Rufaa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  leo tarehe 9 Agosti, 2022 amefungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Mahsusi wapatao 56 wa Mahakama ya Tanzania  yanayohusu  Namna Bora ya Uendeshaji wa Ofisi. Mafunzo hayo yanayofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 09 Agosti ,2022 mpaka 13 Agosti, 2022 katika ukumbi wa Mafunzo uliopo Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Akifungua mafunzo hayo Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amewataka Makatibu Muhtasi  kutoa huduma bora zinazoendana na uwekezaji katika majengo ya Mahakama nchini.  Aliendelea kwa kusema  kuwa, Mahakama ya Tanzania iko katika maboresho ambayo yanagusa maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu ya majengo na raslimali watu hivyo mafunzo haya yana lengo la kuwaandaa watumishi hao ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea.

“Hivyo lengo la mafunzo yanayotolewa ni kujaribu kuwajengea uwezo na kubadilisha fikra za watumishi wa Mahakama ili huduma wanazozitoa mahakamani ziendane na ubora wa majengo ambayo yanaendelea kuboreshwa,” amesema.

Mhe. Dkt. Kihwelo aliwasihi watumishi hao kuwa waadilifu na wachapakazi ili kuipa sifa  nzuri  Mahakama ya Tanzania kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kuichafua Mahakama kama matumizi ya lugha mbaya. Pia aliwaomba watumishi hao watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi ni wajibu  kushirikiana na kuonyesha waliochojifunza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick amewaambia washiriki hao kuwa Mahakama imejipanga kuwajengea uwezo watumishi wake katika kada mbalimbali ili kuendana na maboresho yanayoendelea.

Bi. Beatrice Patrick amesema kundi hilo la washiriki wa mafunzo linajumuisha Makatibu Muhtasi 56, ambapo 50 wametoka katika Mahakama mbalimbali za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi,  washiriki  sita wakiwa ni waajiriwa wapya.

Amesema kuwa watumishi hao wanapewa mafunzo hayo kwa lengo la kuwakumbusha majukumu yao ya kazi za Ukatibu Muhtasi, utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi wa ofisi na mawasiliano ya kiofisi,  uzalendo na protokali, mipango ya Mahakama na uboreshaji, huduma kwa mteja, masuala ya saikolojia na ushauri, mwelekeo wa Mahakama kwa sasa katika mapinduzi ya viwanda kuelekea Mahakama Mtandao na matumizi ya TEHAMA.

 


Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akisisitiza jambo alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Muhtasi 56 yaliyoanza kufanyika leo tarehe 9 Agosti, 2022.


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick akizungumza kwa ufupi kumkaribisha Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo kufungua mafunzo hayo.


Sehemu ya Makatibu Muhtasi wanaoshiriki katika mafunzo (picha mbili juu na moja chini) ikifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Mkuu wa Chuo.


Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote wa mafunzo.

Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Mahakiumu wa Mahakama za Lushoto waliohudhuria kwenye ufunguzi wa Mafunzo hayo.



 Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya mafunzo 

Monday, August 1, 2022

KUWENI NA FIKRA CHANYA MNAPOTOA HUDUMA; PROF OLE GABRIEL

 Na Mary Gwera, Mahakama-Lushoto

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Waajiriwa wapya wa Mahakama nchini kubadili fikra hasi kwa kuwa na fikra chanya ili kuondokana na utoaji wa huduma kwa mazoea na badala yake watoe huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

Akizungumza na Watumishi hao leo tarehe mosi Agosti, 2022 mjini Lushoto wakati akifungua mafunzo elekezi ya awali kwa waajiriwa hao, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, Mahakama inatekeleza programu za maboresho yanayomlenga mwananchi. Kwa hivyo, kipaumbele ni kuhakikisha Mahakama inatoa huduma bora zitakazofanya wananchi kuwa na imani na chombo hicho cha haki pamoja na kuwaweka wananchi kuwa karibu na Mahakama.

“Kwa dhamira hii, Mahakama inatutaka sote kwa pamoja kubadilika fikra zetu ili kuondokana na kutoa huduma kwa mazoea na badala yake kupitia mafunzo haya mnaelekezwa kuwa kila mmoja wenu katika nafasi yake ahakikishe anadhamiria kuunga mkono juhudi hizi za Mahakama kwa kwenda kutoa huduma bora kwa namna ambayo itawafanya wananchi na jamii kwa ukumla kuwa na imani nanyi na imani kwa Mahakama,” amesema Mtendaji Mkuu.

Prof. Ole Gabriel, amewaeleza pia Watumishi hao kuwa tayari kufanya kazi kwenye maeneo watakayopangiwa bila manung’uniko kwa kuwa ndiko wananchi wanataka kupatiwa huduma.

“Ni matarajio yangu kuwa mtakubaliana na vituo mtakavyopangiwa kwa kuwa huko ndiko kunakohitaji huduma zenu na ndio maana Serikali ilitoa kibali muajiriwe. Niwadokeze tu hapa kuwa, hakuna sehemu nzuri wala mbaya ndani ya Mahakama na badala yake kila Mahakama ipo kwenye maeneo ambayo wananchi wanaishi,” amesisitiza Prof. Ole Gabriel.

Amebainisha kuwa, Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo katika maeneo ambayo ni ya msingi katika kuwaandaa kuwa watumishi wema wenye haiba, tabia, mienendo na maadili ya kimahakama.

Akizungumzia suala la matumizi ya TEHAMA mahakamani, Mtendaji Mkuu amewaeleza Watumishi wao kulipa kipaumbele suala la matumizi ya teknolojia kwakuwa ndio Mahakama inapojielekeza kwa sasa.

“Mtakapokuwa mnajifunza hapa, mtaelezwa kuhusu mifumo mbalimbali ya KITEHAMA ambayo itatumika katika kuboresha utoaji haki na huduma mbalimbali katika Mahakama. Lengo la kuelekezwa hayo ni kuwataka mfahamu kuwa matumizi ya TEHAMA si hiari bali ni jambo la lazima kwa kuwa mtakutana na mifumo ya kiteknolojia na matumizi yake katika kutoa huduma za kimahakama na kugundua kuwa imeshika kasi katika kila kona ya Mahakama,” amesisitiza Mtendaji Mkuu.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu amesema kwamba, lengo kuu la mafunzo hayo ni kubadilisha mitazamo ya Watumishi wapya ili iendane na mitazamo ya Mahakama hatimaye kuwawezesha kufanya kazi inavyotakiwa.

“Kama tunavyofahamu Watumishi hawa wametoka mazingira tofauti tofauti, wamelelewa katika mazingira mbalimbali pamoja na mitazamo tofauti, kwahiyo lengo kubwa la mafunzo haya ni kuwaandaa ili waweze kuendana na kile ambacho Mahakama inatarajia,” amesema Bi. Patricia.

Mafunzo hayo ya siku tano (5) yamehusisha Watumishi wa Kada za Afisa Utumishi/Tawala, Wahasibu, Wakaguzi wa Ndani, Maafisa TEHAMA, Maafisa Ugavi pamoja na Madereva.

Mafunzo hayo ambayo imeelezwa kuwa yatakuwa endelevu kwa Waajiriwa wapya wa Mahakama, ni mwendelezo wa Mafunzo yaliyotolewa kwa kundi la Mahakimu na Wasaidizi wa Kumbukumbu yaliyomalizika tarehe 29 Julai, 2022. Aidha, yanafanyika kwa mara ya kwanza, kwa kuwa kabla ya hapo hakukuwa na mafunzo ya namna hii kwa watumishi hao.

Mada zinazotarajiwa kutolewa katika Mafunzo hayo ni pamoja na Muundo na tamaduni za kimahakama, Mpango Mkakati wa Mahakam ana Mpango wa Uboreshaji Huduma za Mahakama, Huduma kwa wateja, Maadili ya Utumishi wa Umma na wa Mahakama, Ubunifu katika kazi na nyingine.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo alipokuwa akifungua rasmi Mafunzo elekezi kwa Waajiriwa wapya wa Mahakama ya Tanzania yanayofanyika leo tarehe Mosi Agosti, 2022 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.



           Washiriki wa wakifuatilia zoezi la Ufunguzi wa Mafunzo wa elekezi.


4.     Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Elia Baha akitoa neno la utangulizi katika zoezi la ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Mahakama. Aliyeketi wa pili kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo, Bw. Halid Magenda, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Morogoro, wa kwanza kulia ni Mhe. Rose Ngoka,  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto na wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo Mahakama ya Tanzania, Bi Patricia Ngunguru


5.     Hakimu Mfawidhi wa Wilaya Lushoto, Mhe. Rose Ngoka akitoa neno la ukaribisho         katika zoezi la ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Mahakama.



5.     Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Elia Baha akitoa neno la utangulizi katika zoezi  la ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Mahakama.


Monday, July 18, 2022

IJA YAENDESHA MAFUNZO ELEKEZI KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA

 

Mhe. Wilbard Chuma Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe 18/07/202 amefungua rasmi mafunzo elekezi kwa watumishi wapya 58 wa Mahakama Tanzania.  Mafunzo hayo yanaendeshwa na kufanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). Hili ni kundi la kwanza kati ya waajiriwa 227 waliofanyiwa usaili na kuajiriwa na  Tume ya Utumishi wa Mahakama hivi karibuni  ambapo kuna kada mbalimbali kama Mahakimu, Maafisa Utumishi, Maafisa TEHAMA, Makatibu Mahususi, Watunza Kumbukumbu Wasaidizi  na Madereva. 

Akitoa hotuba ya ufunguzi, Mhe. Chuma alianza kwa kuwapongeza waajiriwa hao wapya kwa kuwaeleza kuwa ajira waliyopata hawakupata kama hisani ila imepatikana kutokana na ubora waliouonesha wakati wa usaili hivyo wanapaswa kuwa waaminifu, waadilifu na wachapakazi kwa kuzingatia mikataba ya ajira, viapo  na sheria za nchi katika utumishi wao.

Mhe. Chuma aliendelea kwa  kuwasisitiza Watumishi hao wapya wa Mahakama kwa kumnukuu Jaji Mkuu wa Mahakama wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe Mei 31, 2021 katika hotuba yake aliyoitoa wakati akifungua rasmi Mafunzo elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Mahakama Kuu Zanzibar hapa Chuoni kwa kusema watumishi wa Mahakama wanatakiwa kuwa na uadilifu na maadili ili wafanye kazi kwa kuzingaia Katiba na masharti ya viapo.

“Watu husahau kuwa mara nyingi sheria sio mbaya bali ni nafsi, maadili na tabia za wanaotekeleza sheria hizo. Hivyo nawakumbusha kila jalada utakalokuwa ukilitolea uamuzi ukumbuke kuwa linagusa watu halisi, linagusa uhuru wao, biashara zao, mali zao na familia zao. Kumbukeni kuwa wananchi kupitia katiba wametupa sisi Majaji mamlaka ya utoaji haki lakini wananchi wamebaki na haki zao zote za msingi” alinukuu.

Mhe. Chuma aliendelea kwa kuwakumbusha watumishi hao kuwa maadili ni kiini cha haki, na hivyo wakati wa kutekeleza jukumu la utoaji haki na wanatakiwa kuzingatia maadili ya kazi na kutoa maamuzi kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.

Mhe. Chuma aliwaeleza watumishi hao wapya  kuwa malengo ya mhimili wa Mahakama yatafikiwa iwapo watakuwa na nia moja na ushirikiano baina yao na watumishi wengine watakaowakuta kwenye vituo vya kazi watakavyopangiwa. Alieleza kwamba ushirikiano huo utasaidia kufanikisha jitihada zinazoendelea za maboresho ya Mahakama ya Tanzania. Mhe. Chuma aliwasisitiza watumishi hao kuwa na ushirikiano na wadau wengine kwa kuchukua mawazo mazuri na bora kutoka kwenye taasisi au idara zingine kwa kuyafanyia kazi au kuyafikisha mahali panapostahili ili yalete mabadiliko kwa kuwa kazi ya kulijenga taifa ni wote.

Mhe. Chuma aliendelea kwa kuwasisitiza watumishi hao kuwa dhana ya uhuru wa mahakama haina maana ya kuvunja sheria kwa kuwa kanuni hii ya kikatiba inaenda sanjari na kanuni ile ya Utawala wa Sheria. Hivyo, amewataka  Mahakimu kuwa ni wajibu wao kufanya kazi zao chini ya kivuli cha uhuru wa Mahakama, kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi na sio kwa kuzivunja. Aliendelea kwa kuwaasa watumishi wengine ambao sio  mahakimu wakawasaidie  maafisa wa Mahakama wa ngazi mbalimbali katika kufikia azma ya kutenda na kutoa haki kwa mujibu wa sheria ili wasiwe chanzo cha malalamiko au kusababisha uvunjifu wa amani kutokana na utendaji kazi  ambao unakiuka misingi ya utu na katiba.

Mafunzo  haya yanafanyika kwa makundi matatu ambapo kundi la kwanza la Mahakimu Wakazi na Maafisa Kumbukumbu Wasaidizi yamenza leo  tarehe 18 Julai ,2022.  Makundi mengine ya kada nyingine yatafuata na kutegemea kumalizika 12 Agosti, 2022.

IJA inajukumu la kuwajengea uwezo watumishi wote wa mahakama kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wao pia kwa mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma za utoaji haki  nchini.  Pamoja na mafunzo hayo Chuo kimebobea katika kutoa mafunzo ya Stashahada na Astashahada ya sheria. Vilevile Chuo kinafanya shughuli za kutoa ushauri wa kitalaamu, machapisho na tafiti mbalimbali.


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbard Chuma akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Mahakama ya Tanzania yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.





Picha za juu na chini ni watumishi wapya wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbard Chuma.







1.      


Thursday, July 14, 2022

TAASISI YA IRLI YAFANYA ZIARA IJA

Taasisi ya Irish Rule of Law International (IRLI) ya nchini Ireland imefanya ziara ya siku moja Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yenye lengo la kuendeleza hatua za utekelezaji wa mkataba wa mashirikiano uliofanywa kati yake na Chuo tarehe 10 Machi, 2022.  Ziara hiyo iliyofanyika Julai 13, 2022 ilihusisha viongozi watatu kutoka katika Taasisi hiyo ambao ni Mkurugenzi Mtendaji wa IRLI Bwana Aonghus Kelly, Mratibu wa Programu IRLI,  Bwana Sean McHale pamoja  na  Afisa Uhusiano Mwandamizi IRLI Tanzania na Zambia, Bwana  Norville Connolly.

Wakati wa ziara hiyo wageni hawa pia walipata maelezo ya kina ya shughuli  zinazofanywa na Chuo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Chuo Bwana Goodluck Chuwa.  Bwana Chuwa alianza kwa kuwaeleza historia fupi ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto toka kilipoanzishwa na malengo ya uanzishwaji wake.  Aliendelea kwa kusema kwamba Chuo kimekuwa, msaada mkubwa sana kwa Mahakama ya Tanzania na wadau mbalimbali wa sheria nchini kwa mafunzo na tafiti mbalimbali zinazofanywa na Chuo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa IRLI nchini Tanzania Bwana  Aonghus Kelly alitoa maelezo mafupi ya Taasisi hiyo kwa kusema kuwa, Taasisi hiyo inaendesha   programu na miradi katika nchi zinazoendelea yenye lengo la kuimarisha ulinzi na upatikanaji wa haki za binadamu, demokrasia na utawala bora na kukuza utawala wa sheria. Aliendelea kwa kusema kuwa, IRLI inafanya kazi na washirika wa ndani kwa kupitia mashirikiano ili kufikia malengo yake. Alieleza kwamba washirika wa IRLI ni pamoja na mashirika ya kiserikali, wanataaluma ya sheria, watumishi wa mahakama, vyama vya wanasheria, wanafunzi wa sheria na asasi za kiraia katika nchi ambazo taasisi hiyo inafanya kazi.

Sambamba na hayo, IRLI na IJA walijadili kuhusu mpango wa kuandaa kitabu chenye mkusanyiko wa mashauri yanayohusu unyanyasaji na ukatili wa kingono kwa mtoto.

 Mkataba wa mashirikiano kati ya IRLI na IJA ni kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2022 hadi 2027 ukiwa na lengo la  kuimarisha haki ya mtoto hususani katika kufanya tafiti na mafunzo yanayolenga eneo la  unyanyasaji na ukatili wa kingono dhidi ya mtoto.

Mkurugenzi Mtendaji wa IRLI Bw. Aonghus Kelly (katikati) akiwa na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bw. Goodluck Chuwa (kulia) na  Mratibu wa Programu IRLI,  Bw. Sean McHale (kushoto) wakipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Chuo walipotembelea Maktaba ya Chuo wakati wa ziara yao Chuoni.

Pichani ni wageni wa Taasisi ya IRLI na viongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wakiwa katika Maktaba ya Chuo  wakati wa ziara.

Pichani Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bw. Goodluck Chuwa akitoa maelezo kuhusu Chuo kwa wageni kutoka IRLI wakiwa kwenye kikao cha pamoja walipofanya ziara yao Chuoni.



Picha mbalimbali za kikao kati ya wagenikutoka IRLI na Viongozi wa IJA  

 Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bw. Goodluck Chuwa akitoa zawadi ya machapisho ya Chuo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa IRLI Bw. Aonghus Kelly.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bw. Goodluck Chuwa akitoa zawadi ya machapisho ya Chuo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa IRLI Bw. Sean McHale .

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Bw. Goodluck Chuwa akitoa zawadi ya machapisho ya Chuo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa IRLI Bw.Norville Connolly.

Picha ya pamoja kati ya wa wageni kutoka Taasisi ya IRLI na Viongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto 

Friday, June 24, 2022

IJA YASAINI MKATABA WA USHIRIKIANO NA TAASISI YA PAMS FOUNDATION

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kimeingia makubaliano ya Ushirikiano na Taasisi ya PAMS Foundation wenye lengo la kuwajengea uwezo maafisa wa Mahakama wa namna bora ya kuendesha mashauri yahusuyo makosa dhidi ya wanyamapori pamoja na makosa mengine ya uhalifu wa kimataifa (international serious crimes).

Makubaliano hayo yanalenga pia kuijengea uwezo IJA katika eneo la utafiti kwenye maeneo ya makosa makubwa ya kimataifa ikiwemo makosa ya ujangili wa wanyama pori na misitu.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo tarehe 23/06/2022 jijini Dar es Salaam kati ya Jaji Dkt. Paul Faustin Kihwelo, Jaji wa Rufani na Mkuu wa Chuo pamoja na Bi Krissie Clark, Mkurugenzi Mtendaji na miongoni mwa waasisi wa PAMS Foundation yenye Makao yake makuu jijini Arusha.

PAMS Foundation ni shirika lisilo la kiserikali  lenye dhamira ya kuwawezesha wale wote wanaolinda wanyamapori na misitu.




Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PAMS Foundation, Bi. Krissie   Clark (kushoto), wakibadilishana mkataba huo


Mkurugenzi wa Operationi na Mafunzo, Bw.Samson Kassala( wa kwanza kushoto)na na  Mkurugenzi wa Intelijensia na Uchambuzi,(wa pili kushoto) Bw.Elisifa  Ngowi wakisaini mkataba huo. 


Mkurugenzi wa Operationi na Mafunzo, Bw.Samson Kassala( wa kwanza kushoto)na na  Mkurugenzi wa Intelijensia na Uchambuzi,(wa pili kushoto) Bw.Elisifa  Ngowi wakifuatilia utiaji saini huo. 




Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto , Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (kulia) akimpatia machapisho mbalimbali ya Chuo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PAMS Foundation, Bi. Krissie   Clark (kushoto).


Wednesday, June 15, 2022

IJA YAENDESHA MAFUNZO YA NAMNA BORA YA UTOAJI WA ADHABU NA UTEKEZAJI WA AMRI ZA MAHAKAMA

 Na Ibrahim Mdachi – IJA Lushoto

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania chini ya ufadhili wa Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Tanzania zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (BSAAT) kimeendesha mafunzo ya siku tatu kwa Mahakimu 43 kuhusu namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama. Mafunzo hayo yalianza tarehe 13 Juni, na kuhitimishwa tarehe 15 Juni, 2022 Chuoni hapo.

Akifungua mafunzo hayo rasmi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma  aliwataka Mahakimu kuzingatia mwongozo wa adhabu na kujiepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kujenga jamii inayojali haki kwa kila mmoja na kuwafanya wananchi waendelee kuwa na imani na Mahakama.

Alitanabaisha pia kuwa kimsingi mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na uelewa wa mwongozo wa utoaji adhabu ambao ni miongoni mwa nyenzo za maafisa wa Mahakama katika mchakato wa utoaji wa adhabu kuwa halali na usiotiliwa shaka na wadaawa wanaohusika katika mashauri mahakamani wakiwemo washtakiwa, waathiriwa, wapelelezi, mawakili wa utetezi, waendesha mashtaka na umma kwa ujumla.

Mhe. Chuma alisema kuwa ni matarajio ya Mahakama ya Tanzania kupitia mafunzo hayo washiriki watapata uelewa wa mwongozo wa utoaji adhabu, hivyo kutumika ipasavyo katika mashauri hasa ya rushwa, uzoefu utakaopatikana utafikishwa kwa maafisa wengine wa Mahakama ambao hawakufanikiwa kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Mratibu wa Programu ya BSAAT ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha  akitoa maelezo mafupi kuhusu mradi huo alisema kuwa, program hiyo inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kwa kushirikana na Umoja Ulaya (EU) na kuratibiwa na Ofisi ya Rais, Ikulu ilianza kutekelezwa mwaka 2018/2019 ikijumuisha taasisi tisa nufaika ambazo ni wadau katika mnyororo wa haki jinai ikiwemo Mahakama kama mdau muhimu katika utiaji wa haki.

Bw. Magoha aliongeza kuwa program hiyo imelenga kupunguza vitendo vya rushwa kama kikwazo cha kupunguza kiwango cha umasikini kwa Watanzania, kuboresha uadilifu, kuboresha uwezo na uratibu wa mfumo wa haki jinai katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na kuongeza imani kwa umma juu ya utendaji kazi wa Mahakama.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo Bw. Goodluck Chuwa alisema kuwa, ni takribana miaka mitano tangu chuo kimeamua kujikita katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuundwa kwake kitahakikisha kuwa kinaendelea kuyaratibu mafunzo mbalimbali kwa weledi mkubwa kwa lengo la kuleta tija kwa Mahakama na wadau wengine wa sheria nchini.

Mafunzo haya  ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021-2025, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja  na Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wa miaka mitano wa mwaka 2018-2023.

                                                           

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma  akifungua mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama kwa Mahakimu 43 kutoka Mikoa Mbalimbali ya Tanzania yanayofanyika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.


 Hakimu Mkazi Mkuu  wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Richard Kabate akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya  namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama.



 Pichani ni baadhi ya washiriki wa mafunzo katika picha ya pamoja na Mhe. Wilbert Chuma, (Mgeni Rasmi) wakiwa ameketi na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya Lushoto, Mhe. Rose Ngoka na Kaimu Mkuu wa Chuo Bw. Goodluck Chuwa (upande wake wa kulia)  na Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha Na Utawala, Prof. Fatihiya Massawe na Naibu Mkurugenzi wa Utawala, Mahakama ya Tanzania na Mratibu wa Mradi wa BSAAT nchini Bwn. Stephen Magoha (Upande wa Kushoto)

 

Picha ya juu na chini ni picha ya washiriki wa Mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama wakiendelea na mijadala mbalimbali katika mafunzo hayo.

 



 

 


Wednesday, May 25, 2022

JAJI MKUU WA UGANDA AFANYA ZIARA IJA

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo leo tarehe 25 Mei, 2022 amefanya ziara ya kutembelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na kujionea shughuli mbalimbali zinafanywa na Chuo.

 

Katika ziara yake, Mhe. Owiny-Dollo ameambatana na Maafisa 12 kutoka nchini Uganda ambao  miongoni mwa aliombatana nao ni Jaji Kiongozi wa Uganda Mhe. Dkt. Flavian Zeija, Msajili ya Mahakama ya Uganda, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa JTI Uganda, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya JTI Uganda, Msajili waTaasisi ya JTI Uganda na viongozi wa International Development Law Organization Uganda(IDLO).

 

Akiongea akiwa kwenye ziara hiyo, Mhe. Owiny-Dollo alisema kuwa  lengo la ziara yao ni kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kuwandaa Maafisa Mahakama ambao wamepangiwa majukumu mapya na kujifunza jinsi ya kuijengea uwezo Taasisi ya Mafunzo ya Kimahakama ya nchini Uganda (JTI) pia  kujenga ushirikiano katika masuala mbalimbali yanayohusu vyuo na jinsi ya  kuiwezesha Mahakama ya Uganda kufanikisha katika maboresho yake kiutendaji.

Mhe. Owiny-Dollo aliendelea kwa kusema kuwa mafunzo ya kuwandaa Maafisa wa Mahakama wanaopewa majukumu mapya ni muhimu katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo huduma bora ya utaoji haki kwa wananchi.

Alisema wanataka kupata uzoefu ambao utawasaidia yeye na ujumbe kutoka Chuo cha Mahakama cha Uganda kuwawezesha watumishi wanaopewa majukumu mapya kupata mafunzo ambayo yatasaidia katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Maafisa wa Mahakama walioandaliwa kwa kupewa mafunzo mazuri wataelewa vema majukumu yao na mambo ambayo anatakiwa kufanya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kupata haki wanapokuwa na mashauri” alisema

Alipokuwa akiwakaribisha wageni hao, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika alionyesha furaha yake kwa kuushuru ugeni huo kwa kusema kwamba ujio wao ni fursa muhimu ambapo wataitumia kwa kujifunza mambo mbalimbali na kubadilishana uzoefu jinsi vyuo vya Mahakama vinavyofanya kazi.

Naye Mkuu wa Chuo na  Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alipokuwa anaelezea historia ya Chuo kilianzishwa kwa Sheria ya Bunge, Sheria Namba 3 ya 1998. Kilianza kazi yake tarehe 23 Oktoba, 2000 na kilikuwa kinatoa Cheti na Diploma ya Kozi za Sheria. Uzinduzi rasmi ulifanywa na Rais Benjamin Mkapa tarehe 3 Agosti 2001.  Pamoja na historia hiyo Mkuu wa Chuo alieleza lengo la madhumuni ya kuanzishwa kwa Chuo ilikuwa ni kujengea uwezo watumishi wa Mahakama.

Ziara hiyo ni sehemu ya ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Uganda na ujirani mwema kati ya nchi hizi mbili. Sambamba na kutembelea maeneo mbalimbali ya Chuo, Wageni hawa wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vilivyopo katika Wilaya ya Lushoto.


Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo alipokuwa anatoa 
salamu kwa viongozi wa IJA

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika 
akitoa neno la ukaribisho kwa Jaji Mkuu wa Uganda na Viongozi wengine wa Mahakama ya Uganda.



Mkuu wa Chuo na  Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alipokuwa akiwaeleza wageni juu ya historia ya Chuo na shughuli Chuo kinazozifanya

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya JTI Uganda, Mhe. Damilie Lwanga akieleza kwa ufupi shughuli zinazoendeshwa na chuo hicho




Katika picha ni baadhi ya viongozi waliombatana katika Ziara ya Jaji Mkuu wa Uganda wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Uongozi wa IJA kuhusu utendaji kazi wa Chuo
Menejimenti ya IJA wakifuatialia maelezo yaliyokuwa yanawasilishwa na upande wa wageni kutoka Mahakama ya Uganda

Picha ya Mahakimu kutoka Wilaya ya Lushoto wakifuatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa inawasilishwa 
Picha ya pamoja ya Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owinyi- Dollo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Uganda.


Picha ya pamoja ya Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owinyi- Dollo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimienti ya IJA.